Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, sanjari na Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo ameadhimisha Masifu ya Pili ya Jioni. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, sanjari na Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo ameadhimisha Masifu ya Pili ya Jioni.  (Vatican Media)

Kuongoka Kwa Mtakatifu Paulo: Upendo Unaomwilishwa Katika Matendo ya Huruma

Papa Francisko, tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo sanjari na Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo ameadhimisha Masifu ya Pili ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta. Katika mahubiri yake, amejikita zaidi katika amri ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma kama njia ya uzima wa milele; jirani yako ni nani? Na kile ambacho unapaswa kutenda ili kuufikia uzima wa milele na wongofu wa ndani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Januari anaadhimisha Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa ambaye anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa neema yake, Rej. Gal 1:15, akakutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea kwa kina wito wa Sauli, jinsi alivyoitwa na Kristo Yesu, akamwongokea Mungu, toka katika upofu wa mwili, akabahatika kuuona Mwanga wa kweli, Kristo Yesu Mfufuka, akawa kweli ni chombo kiteule cha Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Jina la Mungu kwa watu wa Mataifa. Rej. Mdo 9:15. Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lk 10:27. Tafakari ya Mwaka 2024 imetungwa na Jumuiya ya Kiekumene kutoka Burkina Faso, ambayo imejikita katika umuhimu wa kumwilisha: Upendo, amani na upatanisho kama njia mahususi ya kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu katika maisha.

Masifu ya Jioni, Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume
Masifu ya Jioni, Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema Wakristo wote wanawajibika kushiriki katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kufikia umoja kamili na timilifu mintarafu fadhila za Kimungu katika Biblia na Liturujia, Mahubiri ya Neno la Mungu na Katekesi, Utume wa waamini walei, mtindo wa maisha ya kitawa na maisha ya kiroho katika ndoa; mambo yote haya ni muhimu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hakuna uekumene wa kweli pasi na toba na wongofu wa kweli; sadaka na upendo kwa jirani na hatimaye, ni fadhila ya unyenyekevu. Dhambi dhidi ya umoja wa Wakristo inaendelea kuwatafuna taratibu. Waamini wakumbuke kwamba, kadiri watakavyo jitahidi kuishi matakatifu, kufuatana na tunu za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile, watahamasishwa na watatekeleza umoja wa Wakristo, ikiwa kama wameungana na Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Uekumene wa sala unaomwilishwa katika huduma kwa maskini
Uekumene wa sala unaomwilishwa katika huduma kwa maskini

Ushirikiano huu ujengeke katika: maisha ya sala, huku Wakristo wenyewe wakijitahidi kufahamiana; kufundisha kwa kuzingatia mchakato kiekumene na kwamba, majadiliano ya kiekumene hayana budi kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha. Rej. Lumen gentium 5-11. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, sanjari na Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo ameadhimisha Masifu ya Pili ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta. Katika mahubiri yake, amejikita zaidi katika amri ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma kama njia ya uzima wa milele; jirani yako ni nani? Na kile ambacho unapaswa kutenda ili kuufikia uzima wa milele na kwamba, majadiliano ya kiekumene yanakita mizizi yake katika wongofu wa ndani na kwamba, wakristo wanawajibika kutembea kwa pamoja katika sala. Baba Mtakatifu anasema Amri ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma ni njia ya kufikia maisha ya uzima wa milele, kwa kumpenda Mungu na jirani kama unavyojipenda mwenyewe na kamwe waamini wasitumbukie katika kishawishi cha kuwagawa watu wale wanaowapenda na kundi jingine la wale wanaowachukia. Watu wale ambao waliomwona yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi walikuwa ni: Makuhani na Walawi, lakini Msamaria mwema alipomwona, alimhurumia, akakaribia, akafunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai: Msamaria mwema ni kielelezo cha upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma na kwamba, Wakristo wataweza kuwa wamoja ikiwa kama watajisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao badala ya kila Mkristo kulinda miundo mbinu ya dhehebu lake.

Uekumene unasimikwa katika toba na wongofu wa ndani
Uekumene unasimikwa katika toba na wongofu wa ndani

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kila mbatizwa ni sehemu ya fumbo la Mwili wa Kristo na kwamba, watu wote ni watoto wateule wa Mungu na kuwa, Kristo Yesu ndiye mzaliwa wa kwanza wao na kwamba, jambo la msingi la kuzingatia ni umoja na kutenda kama jirani mwema katika: jumuiya, Kanisa na kama sehemu ya tasahufi ya maisha, ili hatimaye, kufyekelea mbali wivu na mafao binafsi, kinyume cha wito wa Kiinjili. Ili kuweza kuurithi uzima wa milele, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa ni toba na wongofu wa ndani; unyenyekevu na upole, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu. Hii ni hija ya maisha ya kiroho inayosimikwa katika huduma kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika sala, kwa kujikana kikweli, unyenyekevu na upole; ukarimu na moyo wa kidugu. Kwa maana waamini kwa kadiri wanavyokuwa katika ushirika na Mungu Baba, Neno na Roho Mtakatifu ndivyo watakavyoweza kukuza udugu kati yao kwa undani na kwa urahisi zaidi. Rej. Unitatis redintegratio, 7.

Uekumene unaosimikwa katika Injili ya upendo kwa maskini zaidi
Uekumene unaosimikwa katika Injili ya upendo kwa maskini zaidi

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo pamoja na Tume ya Pamoja ya Kiekumene Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki wanaosherehekea kumbukizi ya miaka ishirini ya majadiliano ya kiekumene. Kwa kushirikiana na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani wamewakabidhi wajumbe wa Tume hii, dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia umoja wa Wakristo katika maeneo yao, kwa kuwapelekea watu wa Mungu huruma na amani; mambo ambayo walimwengu wanayatamani sana katika maisha yao. Kamati ya Ushirikiano wa Kitamaduni kati ya Kanisa Katoliki, Makanisa ya Kiorthodox pamoja na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki bila kuwasahau wanafunzi wanaofadhiliwa na Kamati hii. Huu ni mwaliko kwa waamini kudumisha uekumene wa sala, kama sehemu muhimu sana ya wajibu wa hija hii ya pamoja, waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kulikirimia Kanisa zawadi ya umoja. Wasisahau kuwaombea wote wanaoathirika kwa vita. Ni mwaliko wa kusimama na kuambata umoja wa Kanisa, ili ulimwengu upate kusadiki! Yn 17:21.

Upendo usaidie kujenga na kudumisha umoja wa Wakristo
Upendo usaidie kujenga na kudumisha umoja wa Wakristo

Kwa upande wake, Kardinali Kurt Koch, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo katika hotuba yake ya shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaongozea maadhimisho ya Masifu ya Jioni, Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa sanjari na kufunga Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika majadiliano ya kiekumene na kwamba, uekumene wa sala ni kati ya zawadi kubwa kutoka kwa Mungu na kama waamini wanaweza kuongea na Mungu kwa njia ya sala, wanaweza kuhamasika vivyo hivyo kuzungumza kati yao. Upendo wa dhati ni kielelezo kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa wakristo kujizatiti zaidi katika majadiliano ya kidugu, urafiki na uekumene wa huduma ya upendo pamoja na kuandaa mazingira ya majadiliano ya kiekumene katika taalimungu. Uekumene wa upendo umewawezesha waamini kugundua tena udugu wa kibinadamu na Ubatizo mmoja unaowasaidia kuunda mtandao wa urafiki. Upendo usaidie kujenga na kudumisha umoja.

Umoja wa Wakristo
26 January 2024, 14:36