Sikukuu ya Kuongoka Kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa neema yake, Rej. Gal 1:15, akakutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea kwa kina wito wa Sauli, jinsi alivyoitwa na Kristo Yesu, akamwongokea Mungu, toka katika upofu mwili, akabahatika kuuona Mwanga wa kweli, Kristo Yesu Mfufuka, akawa kweli ni chombo kiteule cha Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Jina la Mungu kwa watu wa Mataifa. Rej. Mdo 9:15. Shuhuda ni mtu anayejitahidi kumuiga Kristo Yesu kila siku ya maisha yake, hadi siku ile kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, atakapokamatwa, kuhukumiwa na kufa nje ya mji, Yesu anasali kuwaombea watesi wake na hatimaye, kuwasamehe. Wakati wakimpiga kwa mawe Shemasi Stefano, Shahidi, naye aliomba akisema: “Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala.” Mdo. 7:60. Baba Mtakatifu Francisko anasema katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya Kanisa kuwa na mashuhuda wanaothubutu kuendelea kusali na kusamahe, kama mfano bora wa kuigwa. Kati ya watu walioombewa msamaha na Shemasi Stefano alikuwepo pia kijana Sauli aliyeona na kushuhudia vyema kuuawa kwake. Lakini baadaye kwa njia ya neema ya Mungu, Sauli akatubu na kumwongokea Mungu, akageuka kuwa ni Mtume na Mwalimu wa Mataifa; mmisionari aliyejisadaka bila ya kujibakiza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Paulo amezaliwa upya kwa neema ya Mungu na kwa njia ya ushuhuda wa msamaha wa Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi, kiasi kwamba, amekuwa ni mbegu ya toba na wongofu wake wa ndani.
Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Januari sanjari na kilele cha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayotangazwa, kushuhudiwa na hatimaye, kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu. Juma la 57 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2024 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, linanogeshwa na kauli mbiu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lk 10:27. Tafakari ya Mwaka 2024 imetungwa na Jumuiya ya Kiekumene kutoka Burkina Faso, ambayo imejikita katika umuhimu wa kumwilisha: Upendo, amani na upatanisho kama njia mahususi ya kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu katika maisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema Wakristo wote wanawajibika kushiriki katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kufikia umoja kamili na timilifu mintarafu fadhila za Kimungu katika Biblia na Liturujia, Mahubiri ya Neno la Mungu na Katekesi, Utume wa waamini walei, mtindo wa maisha ya kitawa na maisha ya kiroho katika ndoa; mambo yote haya ni muhimu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.
Hakuna uekumene wa kweli pasi na toba na wongofu wa kweli; sadaka na upendo kwa jirani na hatimaye, ni fadhila ya unyenyekevu. Dhambi dhidi ya umoja wa Wakristo inaendelea kuwatafuna taratibu. Waamini wakumbuke kwamba, kadiri watakavyo jitahidi kuishi matakatifu, kufuatana na tunu za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile, watahamasishwa na watatekeleza umoja wa Wakristo, ikiwa kama wameungana na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ushirikiano huu ujengeke katika: sala, huku Wakristo wenyewe wakijitahidi kufahamiana; kufundisha kwa kuzingatia mchakato kiekumene na kwamba, majadiliano ya kiekumene hayana budi kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha. Rej. Lumen gentium 5-11. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa kiinjili kati yao na kati ya watu wa Mataifa, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadam alama yenye mvuto na mashiko kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake, na kama sehemu muhimu sana ya mapambano dhidi ya changamoto mamboleo. Wakristo kama ilivyokuwa kwa nyakati za Mtakatifu Paulo, Mtume wanapaswa kujitahidi kuungana pamoja kwa mawazo na maneno na kwamba, umoja wa Wakristo si mkakati wa kibinadamu bali ni changamoto kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe, anayewavuta wafuasi wake kuungana sanjari na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kutenda kadiri ya mapenzi yake yanayojikita katika upendo kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu ndiye kiini, sababu na kikolezo cha umoja miongoni mwa Wakristo.
Utengano miongoni mwa Wakristo si jambo la kawaida anasema Baba Mtakatifu Francisko, linahitaji kufanyiwa marekebisho ya kina, kwani utengano kati ya Wakristo una madhara makubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Unahatarisha ushuhuda unaopaswa kutolewa na Wakristo duniani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ndiye msingi wa Kanisa na urithi wa wakristo wote. Lakini inasikitisha kuona kwamba, bado Wakristo wenyewe wamegawanyika kinyume kabisa cha utashi wa Kristo mwenyewe na utengano huu unaendelea kuwa ni kielelezo cha kashfa ya ushuhuda wa utangazaji wa Injili duniani. Baba Mtakatifu anawatia shime Wakristo kufanya hija pamoja na kutegemezana ili kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo. Katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, dhana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro imejidhihirisha wazi, mwaliko wa kuendelea kufahamiana zaidi kwa ajili ya majadiliano ya Kiekumene kwa kutambua utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hata kwa siku za usoni. Changamoto na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza katika majadiliano ya Kiekumene ni mambo ambayo hayawezi kufichika, lakini kuna haja kwa Wakristo kupiga moyo konde na kuanza kujivika utashi wa Kristo kwa ajili ya umoja miongoni mwa Wakristo. Wawe tayari kuvuka vikwazo vyote vinavyosababisha utengano na hivyo kujivika nguvu ya upendo inayotolewa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa.