Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana: Umuhimu wa Ubatizo wa Watoto Wachanga: Imani ya Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho “vitae spiritualis ianua” na kwa njia hii, mwamini anaweza kupata Sakramenti nyingine zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanafanywa huru toka dhambi na wanazaliwa upya kama watoto wa Mungu, viungo vya Kristo Yesu, wanaingizwa katika Kanisa na kufanywa washiriki katika utume wa Kristo. Kimsingi Mababa wa Kanisa wanasema, Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji na katika neno. Ni kutokana na umuhimu huu, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha kwa ari na moyo mkuu Sikukuu ya Ubatizo wao, alama ya kufa na kufufuka na Kristo Yesu, kwa njia ya Maji ya Ubatizo na Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni viumbe wapya, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Sakramenti ya Ubatizo inachota utajiri wake kutoka katika Fumbo la Pasaka. Hii ni Sakramenti ya imani inayomwezesha mwamini kuingia katika maisha ya kiimani, kwa kuwekwa huru dhidi ya mitego ya Shetani, Ibilisi. Kuhusu Ubatizo wa Watoto wachanga, Kanisa linapania kuwasaidia watoto hawa kuzaliwa upya kwa “Maji na Roho Mtakatifu” ili kuwaweka huru dhidi ya nguvu za giza na hatimaye, kuingizwa katika utawala wa uhuru wa watoto wa Mungu. Kutokana na utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, malezi na makuzi ya watoto na vijana yamekuwa ni changamoto kubwa kwa wazazi na walezi wengi. Kuna watoto wengi hawana tena fursa ya kupokea Sakramenti za Kanisa kutokana na shule wanakosoma na kuishi.
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Barani Afrika wanasema kutokana na huruma na neema ya Mwenyezi Mungu, hakuna mtoto anayepaswa kunyimwa Sakramenti ya Ubatizo, kwani ni sehemu ya utekelezaji wa Agizo la Kristo Yesu aliyesema “Basi, enendeni, mkawafanye Mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Mt. 28:19. Rej Mk. 16:15-16. Hii ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa na mlango wa wokovu kwa watoto wa Mungu, ambao hata kama hawawezi kukiri imani kwa vinywa vyao wenyewe, lakini wazazi na wasimamizi wao, wanakiri imani ya Kanisa kwa niaba yao. Ni kwa njia hii, watoto hawa wanapata neema na uhuru wao unakuzwa na kudumishwa. Wazazi na walezi wajitahidi kuwa ni mashuhuda wa imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kutambua kwamba, Sakramenti ya Ubatizo ni muhimu kwa wokovu wa mtu binafsi na ni njia ya huruma na upendo wa Mungu unaomwokoa mwanadamu kutoka katika dhambi ya asili na hivyo kuwashirikisha watoto maisha ya uzima wa Kimungu. Kumbe, ushiriki mkamilifu wa wazazi na walezi ni muhimu sana kwa Ubatizo wa watoto wachanga. Maandalizi ya kina yanapaswa kufanyika ili wazazi na walezi watambue tangu mwanzo dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya watoto wao. Jumuiya ya waamini inahamasishwa kushiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto katika imani. Haya ni baadhi ya mambo muhimu yaliyopewa uzito wa pekee na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu Mwongozo wa Ubatizo kwa Watoto Wachanga wa tarehe 20 Oktoba 1980 ujulikanao kama “Sacred Congregation for the Doctrine of the Faith. INSTRUCTION ON INFANT BAPTISM. Pastoralis action.”
Tangu nyakati za zamani sana, Ubatizo umetolewa kwa watoto wachanga, kwani kwa neema na kipaji cha Mungu ambacho hakitegemei mastahili ya kibinadamu: watoto wachanga hubatizwa katika imani ya Kanisa. Kuingia katika maisha ya Kikristo huwezesha kuingia katika uhuru wa kweli. Katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, kumekuwepo na Mapokeo ya kuwabatiza watoto wachanga kwenye Kikanisa cha Sistina kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 7 Januari 2024 amewabatiza watoto wachanga kumi na sita, ili kuwapatia watoto hawa zawadi ya imani na kwamba, watoto hawa ndio wahusika wakuu katika maadhimisho ya Ibada hii ya Misa Takatifu. Watoto hawa ni mashuhuda wa jinsi ya kupokea, kuitangaza na hatimaye kuishuhudia imani; katika unyoofu na uwazi wa moyo. Baba Mtakatifu amewataka wazazi, walezi na wasimamizi wa Ubatizo wa watoto hawa kuwasaidia kukua na kukomaa katika imani; waendelee kuwa ni mashuhuda amini wa imani inayomwilishwa katika matendo mema, adili na matakatifu. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wazazi na wasimamizi wa Ubatizo, kwa kuwaanzishia watoto wao safari ya imani. Amewataka kuikumbuka tarehe hii, ili kuwajulisha watoto wao watakapokuwa wakubwa, kwamba tarehe 7 Januari 2024 wamepokea neema ya Mungu na hivyo kuwa ni Wakristo. Hii ni tarehe inayopaswa kusherehekewa na kuadhimishwa kila mwaka!
Ikumbukwe kwamba, imani ni kipaji cha bure kinachotolewa na Mwenyezi Mungu, hali inayodhihirishwa kwa namna ya pekee, katika ubatizo wa watoto wachanga. Baba Mtakatifu Francisko daima anawataka wazazi, walezi na wasimamizi wa Ubatizo kushiriki kikamilifu katika kuwarithisha vyema watoto wao imani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwa njia ya ushuhuda wa maisha, yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anasema, ni kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanaitwa kuwa Wakristo, kwa kushirikishwa katika maisha na utume wa Kristo yaani: Ufalme, Unabii na Ukuhani wake, tayari kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa! Baba Mtakatifu anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu nguvu ya kuweza kuwa kweli ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!