Ufunguzi wa Mwaka wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa: Kifungo cha Ndoa na Huruma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana”, imezindua rasmi Mwaka wa Mahakama 2024 kwa kukutana na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 25 Januari 2024. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia kuhusu: Mang’amuzi katika mchakato wa kubatilisha ndoa; huruma katika utume wa familia; uhuru katika kutoa maamuzi pamoja na fadhila za busara na haki pamoja na mtazamo wa kisinodi. Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana” kwa huduma makini wanayoitoa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kusimamia haki katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, huduma hii inapaswa kusimikwa katika mchakato wa mang’amuzi katika shughuli za maisha ya ndoa na familia, ili hatimaye, kuweza kufikia uamuzi wa kubatilisha ndoa. Mang’amuzi ni tema ambayo inapaswa kufanyiwa kazi katika mchakato wa kubatilisha ndoa za Kikristo sanjari na kuimarisha utume wa familia kwa waamini ambao wanakabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha ya ndoa; huruma ipewe msukumo wa pekee ili kuongeza kasi ya ufafanuzi wa hukumu, kwani kuna waamini wanaoongojea ufafanuzi wa hali yao ya maisha ya ndoa, ili kuondoa giza la mashaka linalotanda katika maisha yao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa kufuata nyayo za watangulizi wake, anataka sababu za ubatili wa ndoa zishughulikiwe kwa njia ya mahakama na wala si kwa njia za kiutawala, ili kulinda kiwango cha juu zaidi juu ya ukweli wa kifungo kitakatifu na hii inahakikishwa haswa na dhamana ya utaratibu wa mahakama.
Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” sura ya Nane anakazia umuhimu wa kusindikiza, kutambua na kuubeba udhaifu wa wanandoa, kwani Ndoa ya Kikristo ni kama sura inayoakisi muungano kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake inatekelezwa kwa makini katika muungano kati ya mwanamume na mwanamke wanaojitoa mmoja kwa mwenzake kwa upendo ulio huru, wenye uaminifu na kupendana hadi kifo kitakapowatenganisha. Anakazia kwenda kwa utartibu katika huduma za kichungaji; utafiti wa hali zisizokuwa za kawaida, ili kuhurumia na kusimika upya; vipengele vinavyopunguza makali ya sheria za Kanisa; Sheria na utambuzi; mantiki ya huruma ya kichungaji. Kumbe, kwa mwanga wa huruma ya Mungu, iwe ni msaada katika kufanya mang’amuzi ya kutengua ndoa, kwa kuzingatia kwamba, huruma haiondoi haki na ukweli, lakini huruma ni utimilifu wa haki na udhihirisho unaong’ara zaidi wa ukweli wa Mungu. Kazi ya kuhukumu talaka si jambo rahisi na kwamba, mang’amuzi ya mchakato huu ni dhamana na wajibu mkubwa wa Kanisa unaopaswa kutekeleza kwa ujasiri na ukweli angavu wa Roho Mtakatifu anayewafundisha yale wanayopaswa kutenda na njia ya kuweza kutembea kwa pamoja ili hatimaye kufahamu ukweli na hivyo kutenda haki. Ni vyema ikiwa kama Mahakimu watatoa hukumu zao katika mwanga wa Roho Mtakatifu, ili maamuzi yao yawe ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu husika na familia ya watu wa Mungu katika ujumla wao.
Utekelezaji huu, unawataka wawe huru na kamwe wasielemewe na maamuzi mbele, kwa kujikita katika haki na ukweli, ili kuwasogeza watu kwa Mungu na wala si vinginevyo. Mang’amuzi ya mahakama yapambwe na fadhila za busara na haki inapojishughulisha na watu walio kwenye matatizo ya kuishi kikamilifu sheria ya Mungu, hapa wito ni kufuata njia ya upendo, kwani upendo wa kidugu ni kanuni ya kwanza ya Wakristo; upendo ni kwa ajili ya ustawi wa ndoa. Juhudi za kichungaji ziwe ni kwa ajili ya kustawisha na kuimarisha ndoa ili kuziepusha kuvunjika ni ya muhimu zaidi kuliko huduma ya kichungaji kwa ndoa zilizokwisha kuvunjika. Utambuzi juu ya uhalali wa kifungo cha ndoa ni mchakato mgumu sana na kwamba, tafsiri ya Sheria za Kanisa inapaswa kufanywa katika mwanga wa ukweli juu ya ndoa isiyoweza kuvunjika, ambayo Mama Kanisa huihifadhi kama ukweli na kuusimika katika mahubiri na utume wake. Ikumbukwe kwamba, tafsiri ya Sheria na kanuni lazima zifanyike katika Kanisa, ili kuweza kujisikia pamoja na Kanisa: Sentire cum Ecclesia.” Hii kanuni ina mantiki yake katika nidhamu, kanuni na Sheria za Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anakazia pia mtazamo wa Kisinodi katika mchakato wa kutengua ndoa za Kikristo. Hii ni dhamana inayotekelezwa kwa njia ya majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi sanjari na utafutaji wa ukweli; kwa kujikita katika maongozi ya Roho Mtakatifu na kwa kuhakikisha kwamba, nyenzo zote muhimu zinatumika ili kufikia ukweli badala ya kufanya maamuzi kwa haraka. Ili kufikia lengo hili, kuna haja kwa Mahakimu na wafanyakazi wa Mahakama kujinoa mara kwa mara katika kozi zinazohusu usimamizi wa kesi Mahakamani pamoja na mafundisho makini kuhusu Mahakama! Kwa hakika huu ni wajibu katika kuhukumu. Kumbe, ili kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, wafanyakazi wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana” wanapaswa kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, ili hatimaye waweze kuwajibika kila sehemu wakiwa ni wafanyakazi wa haki.
Kwa upande wake, Askofu mkuu Alejandro Arellano Cedillo, Dekano wa Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa “Rota Romana” katika hotuba yake kwa Baba Mtakatifu amemhakikishia ushiriki wao katika utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika shughuli zake za kichungaji kwa kujikita katika kuheshimu utawala wa sheria, utakatifu katika haki pamoja na kuendeleza utambuzi wa sheria katika kukuza mahusiano na mafungamano kati ya watu na kwamba, Sheria ni chombo cha kutekelezea haki na hasa miongoni mwa maskini. Ukweli na dhamiri nyofu ya mwanadamu ni mambo msingi kwa wafanyakazi wa Mahakama kama utekelezaji wa haki miongoni mwa watu wa Mungu. Lengo la utume wa Mama Kanisa ni kuwa mhudumu wa haki kwa ajili ya utukufu wa Mungu unaoadhimishwa katika huduma kwa ajili ya wokovu wa watu wote, kumbe sheria ni kwa ajili ya wokovu wa roho za watu “Salus animarum.” Kumbe, wao wanafanya kazi kwa kuzingatia haki, sheria kwa watu wa Mungu, upendo na ukweli ni mambo msingi yanayoweza kuwafanya watu wa Mungu kuwa huru na wenye furaha. Kumbe, kwao huu ni tume wa kuganga na kuponya madonda ya waamini yanayoathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya watu wa Mungu. Ili kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu, wafanyakazi hawa wanapaswa kuwa ni watu wa sala, wasikivu wa Neno la Mungu na washiriki waaminifu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu!