Sakramenti za Kanisa, Utu na Imani: Wongofu wa Kichungaji, Kimisionari na Kerygma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inabainisha dhamana na wajibu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuwa ni kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Maaskofu kutangaza na kushuhudia Injili sehemu mbalimbali za dunia, kwa kulinda na kudumisha mafundisho tanzu ya Kanisa, tayari kujibu kwa ukamilifu changamoto mamboleo. Baraza hili limegawanyika katika sehemu kuu mbili: Sehemu ya kwanza ni kuhusiana na Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Sehemu ya Pili ni Nidhamu. Baraza hili linapaswa kuwa na wataalam wa sheria na hasa zaidi kuhusu ulinzi wa watoto wadogo dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia; kutoa malezi endelevu kwa makleri, ili kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto wadogo. Idara ya Ndoa, kwa mwaka huu wa 2024 inafanya kumbukizi ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake sanjari na ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, tukio lililotekelezwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Kumbe, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linatekeleza dhamana na utume wake kwa kuzingatia akili inayomwilishwa katika imani. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarahe 26 Januari 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Katika hotuba yake amekazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu: Uhalali wa Sakramenti za Kanisa; Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Imani kama kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili; mwaliko wa kujikita katika wongofu wa kichungaji, kimisionari pamoja na kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma.” Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa katika mkutano wake wa mwaka 2024 wamejadili kwa kina na mapana kuhusu uhalali wa Sakramenti kwa sababu Kanisa linakuwa na kukomaa kutokana na Sakramenti.
Kumbe, viongozi wa Kanisa wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha vyema Sakramenti za Kanisa, ili kuwasaidia waamini kutekeleza dhamana yao ya kikuhani, kinabii na kifalme; mambo yanayomwilishwa katika ushuhuda wa upendo, mwaliko ni kuhakikisha kwamba, waamini wanahamasika kupenda uzuri wa Sakramenti pamoja na nguvu yake ya kuokoa! Baba Mtakatifu anaendelea kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa sasa Baraza la Kipapa linaandaa Waraka kuhusu utu, heshima na haki msingi za binadamu, kielelezo cha ukaribu wa Mama Kanisa kwa watu wote. Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; sanjari na kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii unaomwilishwa katika matendo. Baba Mtakatifu kuhusu imani amewakumbusha wajumbe wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu matukio muhimu ikiwa ni pamoja na kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili. Pili ni Jubilei ya Mwaka 2025 inayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Hiki ni kipindi cha kupyaisha utangazaji na ushuhuda wa imani, hususan miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; Uinjilishaji mpya unaopaswa kutekelezwa mijini kwa kuzingatia matatizo, changamoto na fursa zake. Huu ni mwaliko wa kujikita katika wongofu wa kichungaji, kimisionari pamoja na kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma” mambo msingi katika kukoleza maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu; kumbe, matukio yote haya yanapania pamoja na mambo mengine kukuza na kuimarisha imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa lina dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.
Baba Mtakatifu amegusia pia kuhusu Waraka wa Tamko la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “Fiducia supplicans” Yaani “Kuomba Baraka kwa Imani” Maana ya Baraka Kichungaji” lililotolewa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 18 Desemba 2023 baada ya kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko limepokelewa kwa hisia tofauti kinyume cha lengo la Tamko lenyewe. Baba Mtakatifu Francisko akijibu mashaka ya Makardinali “Dubia” waliomwandikia kuelezea wasiwasi wao kuhusu masuala makuu matano huku wakiomba tafsiri kuhusiana na: Ufunuo wa Kimungu, juu ya baraka kwa ndoa za watu wa jinsia moja; Kuhusu Sinodi kama mwelekeo wa Kisheria wa Kanisa; Juu ya Upadrisho wa wanawake ndani ya Kanisa Katoliki na juu ya Toba kama sharti la lazima kwa ajili ya msamaha unaotolewa kwenye Sakramenti ya Upatanisho. Mashaka Kuhusu baraka za ndoa ya watu wa jinsia moja Baba Mtakatifu anasema, Ndoa ya Kikristo kama sura inayoakisi muungano kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake, inatekelezwa kwa utimilifu katika muungano kati ya mwanaume na mwanamke wanaojitoa mmoja kwa mwenziye kwa upendo ulio huru, wenye uaminifu na wa kipekee, ambamo kila mmoja anakuwa ni mali ya mwenzake hadi kufa, na wanakuwa radhi kuendeleza uzao, tena wamewekwa wakfu kwa Sakramenti inayowaletea neema ya kuwa Kanisa la nyumbani na kuwa chachu ya maisha mapya kwa jamii. Hii ndio maana ya Ndoa ya Kikristo na wala si vinginevyo! Rej. Amoris laetitia 292. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kuhusu baraka za kichungaji, kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa watu wenye shida na mahangaiko makubwa, ili waweze kuanza tena hija ya imani. Hii ni baraka ambayo inapaswa kutolewa nje ya Liturujia ya Ndoa na pili baraka kwa watu wanaojitokeza kuiomba kwa kuzingatia mazingira wanamoishi.