Wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, CEF., tarehe 12 Januari 2023 wamekutana na Papa Francisko. Wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, CEF., tarehe 12 Januari 2023 wamekutana na Papa Francisko.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Wadau wa Tasnia ya Mawasiliano Fanyeni Kazi kwa Ujasiri, Ushuhuda na Mwelekeo Mpana

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: changamoto za mawasiliano ya jamii katika ulimwengu mamboleo; mawasiliano kama ushuhuda unaosimikwa katika maneno, maandishi na picha; waandishi wa habari wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ujasiri pasi na woga, huku wakiwa na mwono mpana zaidi kwa kukazia mambo yale yanayowaunganisha watu na haya yatangazwe kwa ubunifu mkubwa unaobubujika katika upendo, wawe ni mashuhuda wa ukweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, CEF.,  The Universités des communicants en Église (UCE), mara kwa mara hunolewa, ili waweze kuboresha ari na utendaji wa shughuli zao katika maisha na utume wa Kanisa kadiri ya maeneo yao ya kazi. Kwa mwaka 2024, Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa limeandaa kongamano la wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii, kama sehemu mahususi ya maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 inayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu.

Mawasiliano ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa binadamu
Mawasiliano ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa binadamu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mawasiliano ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa mwanadamu, kwani tangu mwanzo, Adamu alipomwona Eva akasema sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, nyama katika nyama yangu, Basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. Rej. Mwa 2:23. Katika hotuba yake, aliyoitoa Ijumaa, tarehe 12 Januari 2024, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: changamoto za mawasiliano ya jamii katika ulimwengu mamboleo; mawasiliano kama ushuhuda unaosimikwa katika maneno, maandishi na picha; waandishi wa habari wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa ujasiri pasi na woga, huku wakiwa na mwono mpana zaidi kwa kukazia mambo yale yanayowaunganisha watu! Baba Mtakatifu amewaambia wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwamba, mawasiliano ni wajibu na utume wao mahususi na kwamba, safari yao mjini Roma ni fursa kwa ajili ya kusali, kusikiliza na kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye anachukua nafasi kubwa katika ulimwengu wa mawasiliano!

Wadau wa tasnia ya mawasiliano: Ushuhuda, ujasiri na mwono mpana
Wadau wa tasnia ya mawasiliano: Ushuhuda, ujasiri na mwono mpana

Wadau wa tasnia ya mawasiliano watambue ukweli huu kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia; kujenga na kudumisha ushirika unaowaunganisha na Kristo Yesu, ili kamwe katika utume huu, wasijikute wanatumbukia katika ubinafsi na uchoyo wao; sera na mikakati ya binafsi; au wakazama katika upweke hasi, wasiwasi na hofu na hatimaye kudhani kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ndiyo funga kazi na hakuna cha zaidi tena! Kuna changamoto kubwa katika maendeleo ya sayansi ya mawasiliano na kati ya changamoto hizi; umiliki na udhibiti wa mawasiliano, uchu wa madaraka; na kudhani kwamba, mambo yote ni matokeo ya sera na mikakati ya kiuchumi na uratibu wake, lakini kuna chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Kumbe, kuna haja ya kuhabarisha watu kwa njia ya moyo, kwa kuangalia na kutazama kwa jicho la moyo; na hatimaye, kusikiliza kwa sikio la moyo, ili kuwashirikisha wengine kile ambacho hawakioni wao. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, dhidi ya ulimwengu mamboleo ambao umechafuka sana kwa maneno, picha pamoja na uchu wa mali na madaraka. Mawasiliano si kwa ajili ya kufanya “propaganda”, au matangazo ya biashara, lakini kwa Wakristo mawasiliano ya jamii ni kuwashirikisha wengine ujenzi wa mtandao wa wema na uzuri; mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwa kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya. Kimsingi mawasiliano ya jamii kwa Wakristo yanafumbatwa katika: ushuhuda, ujasiri na mwono mpana zaidi.

Mawasiliano ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa binadamu
Mawasiliano ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa binadamu

Baba Mtakatifu anasema, haya ni mawasiliano yanayofumbatwa katika maneno, picha na maandishi na kwamba, huu ndio ushuhuda unaojenga mtandao wa mawasiliano ya jamii. Kanisa Katoliki nchini Ufaransa kwa sasa limezama katika mchakato wa utakaso, ili kuona mwanga zaidi katika maisha na utume wa Kanisa,  mwaliko wa kutangaza na kushuhudia pia matukio mazuri katika maisha na utume wa Kanisa, ili kujenga na kudumisha ushirika, udugu wa kibinadamu pamoja na kujitahidi kuwa wabunifu na kwamba, watu wa Mungu wanayo kiu ya kumsikiliza Mama Kanisa anayewapenda watu wote. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii watekeleze dhamana na wajibu wao kwa ujasiri pasi na woga; kwa kujikita katika unyenyekevu; kwa kuwa makini katika taaluma na weledi. Waandishi wa habari wakati mwingine wanapaswa kufanya maamuzi magumu, lakini kamwe wasikate temaa, bali wawe na furaha ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, upendo unaowafanya kumtambua Mwenyezi Mungu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka. Watambue kwamba, walimwengu wanao kiu ya Mungu, wanatamani kukutana na Muumba wao na wakati mwingine, hata kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu anawataka waandishi wa habari kuwa na mwono mpana zaidi unaowawezesha kuuangalia ulimwengu katika ujumla wake, uzuri na yote yaliyomo, tayari kuangalia mambo msingi; kwa kukazia yale mambo yanayowaunganisha watu; haya yatangazwe kwa ubunifu mkubwa unaobubujika kutoka katika upendo. Watangaze na kushuhudia ukweli unaofumbatwa katika upendo na kwamba, mawasiliano yao yapate chimbuko lake kutoka katika moyo unaoangalia kwa upendo.

Mawasiliano Ufaransa

 

13 January 2024, 15:15