Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 5 Februari 2024 ameongoza mkutano wa Makardinali washauri tisa ili kuendelea na mjadala ulioanzishwa mwezi Desemba 2023 : Dhamana na wajibu wa wanawake katika utume wa Kanisa Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 5 Februari 2024 ameongoza mkutano wa Makardinali washauri tisa ili kuendelea na mjadala ulioanzishwa mwezi Desemba 2023 : Dhamana na wajibu wa wanawake katika utume wa Kanisa  (Vatican Media)

Dhamana na Wajibu wa Wanawake Katika Maisha na Utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 5 Februari 2024 ameongoza mkutano wa Makardinali washauri tisa ili kuendelea na mjadala ulioanzishwa mwezi Desemba 2023 kuhusu dhamana na wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Majadiliano hayo yamechangiwa pia na Sr. Linda Pocher, Mama Giuliva Di Berardino, Jalimu wa mafundisho ya maisha ya kiroho, Jimbo kuu la Verona, Mama Jo Bailey, Askofu wa Kanisa la Kianglikana na Katibu mkuu msaidizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna haja ya kutambua kwamba, kuna usawa na utofauti, kama kielelezo makini kinachotafuta uwiano mzuri unaojikita katika mahusiano dhidi ya utamaduni wa mfumo dume unaoendelea kumkandamiza mwanamke. Kuna haja ya kuvuka kishawishi cha kudhani kwamba, wote ni sawa sawa, kwa kushindwa kutambua tofauti, katika utambulisho wa mtu na asili kwani mwanamke na mwanaume wanakamilishana. Pili, Baba Mtakatifu anasema, uwezo wa mwanamke kuzaa ni kanuni na utambulisho maalum kwa wanawake ambao wamejaliwa uwezo wa kuendeleza zawadi ya maisha, kwa kuilinda na kuidumisha. Kanisa linapenda kuwapongeza wanawake kwa mchango wao katika medani mbali mbali za maisha ya mwandamu; kwani wamekuwa mstari wa mbele katika masuala ya elimu na majiundo; shughuli na mikakati mbali mbali ya kichungaji na kwamba, wanawake wanaonesha sura ya huruma ya Mungu kwa binadamu. Ni watu wanaojisadaka kwa njia ya huduma, kwa kuonesha ukarimu, kimsingi, wanawake ni sawa na tumbo la Kanisa linalopokea na kuzaa maisha.

Dhamana na wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa
Dhamana na wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa

Tatu, Baba Mtakatifu anajaribu kuangalia mwili wa mwanamke kati ya tamaduni na bayolojia, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanamke mwili unaopendeza, lakini pia umesheheni madonda ambayo wakati mwingine yamesababishwa na dhuluma pamoja na nyanyaso. Mwili wa mwanamke ni kielelezo cha maisha, lakini kwa bahati mbaya, unaharibiwa hata na wale ambao walipaswa kuwalinda na kuwasindikiza katika maisha! Kuna mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, biashara ya ngono na vitendo vya ukeketaji; mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuyavalia njuga, ili kusitisha vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya wanawake duniani, kiasi cha kuwageuza kuwa kama bidhaa inayouzwa sokoni, bila kusahau umaskini unaosababisha wanawake wengi kuishi katika mazingira magumu na hatarishi; kiasi hata cha kunyanyaswa, kielelezo cha utamaduni usiojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine.

Wanawake wanao mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Kanisa
Wanawake wanao mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Kanisa

Nne, Baba Mtakatifu anapopembua kuhusu wanawake na dini: mwelekeo wa kutafuta ushiriki katika maisha na utume wa Kanisa anakiri kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wanawake wanashiriki kwa ukamilifu zaidi katika utekelezaji wa dira na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani na nje ya Kanisa. Wanawake ni wadau wakuu katika kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ni watu wenye utajiri mkubwa, wanaoweza kusaidia upatikanaji wa amani na utulivu; wito na utume maalum kwa wanawake. Ziwepo juhudi za makusudi ili kuwahamasisha wanawake kushiriki katika maisha ya hadhara, katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa: mahali panapotolewa maamuzi na utekelezaji wa mikakati na sera mbali mbali; kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha ya kifamilia. Wanawake wasaidiwe kufanya maamuzi machungu katika maisha, kwa kuwajibika barabara katika jamii na katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 5 Februari 2024 ameongoza mkutano wa Makardinali washauri tisa ili kuendelea na mjadala ulioanzishwa mwezi Desemba 2023 kuhusu dhamana na wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Majadiliano hayo yamechangiwa pia na Sr. Linda Pocher, Jalimu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha “Auxilium cha Roma” Mama Giuliva Di Berardino, Jalimu wa mafundisho ya maisha ya kiroho, Jimbo kuu la Verona, Mama Jo Bailey, Askofu wa Kanisa la Kianglikana na Katibu mkuu msaidizi wa Ushirika wa Waanglikani.

Wanawake na Kanisa

 

06 February 2024, 14:58