Kongamano la IV la Kimataifa la Pluriel: Mizizi ya Maovu Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu walitia mkwaju kwenye “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu.” Hii ni changamoto kwa waamini wa dini mbalimbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: Binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha utamaduni wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili hatimaye, familia ya binadamu iweze kukua na kukomaa katika mchakato wa upatanisho, kwa kuwakirimia watu matumaini yanayobubujika kutoka katika huduma ya upendo. Dini mbalimbali duniani zina uwezo wa kujenga utamaduni wa kuwakutanisha watu ili kuimarisha umoja na udugu wa kibinadamu. Hati hii ni kikolezo cha ujenzi wa misingi ya usawa, haki, amani na maridhiano duniani. Waamini wa dini mbalimbali wanapaswa kushikamana ili kulinda na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote; kudumisha haki msingi za binadamu; kwa kutoa majibu muafaka dhidi ya vita, kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za dunia. Waamini na watu wenye mapenzi mema wakishirikiana kwa dhati wanaweza kukomesha pia vita, rushwa na ufisadi; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; kwa kubainisha na kutekeleza sera na mikakati ya uchumi fungamani pamoja na kuwakirimia watu wa Mungu matumaini katika hija ya maisha yao.
Kauli mbiu ya Kongamano la 4 la Kimataifa la "PLURIEL” yaani “Jukwaa la Chuo Kikuu cha Utafiti juu ya Uislamu”: “The University Platform for Research on Islam” kuanzia tarehe 2 hadi 6 Februari 2024 huko Abu Dhabi, Falme za Kiarabu linanogeshwa na kauli mbiu “Uislamu na udugu wa kibinadamu: Athari na mitazamo ya “Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu” katika nyakati hizi ambamo kunaendelea kushuhudiwa ukosefu wa haki msingi za binadamu, vita na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la Nne la Kimataifa la “Pluriel” anasema kwamba, mizizi ya maovu yote haya ni ukosefu wa ujuzi wa mwingine, ukosefu wa sanaa na utamaduni wa kusikiliza sanjari na ukosefu wa kubadilika kiakili. Mapungufu haya matatu katika roho ya mwanadamu yanaharibu udugu wa kibinadamu na yanapaswa kutambuliwa vyema ili kugundua tena hekima na amani. Baba Mtakatifu anasema, matatizo na changamoto katika ulimwengu mamboleo hayataweza kupatiwa ufumbuzi, ikiwa kama hakuna jitihada za makusudi za kutaka kufahamiana ili hatimaye, kujengeana imani na kukubaliana kimsingi kwamba wote ni ndugu wa moja, dhana inayopaswa kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha. Amani ya kweli inasimikwa katika heshima na ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kwamba, majadiliano ya kidini ni safari, ushirikiano katika maisha ya kawaida; unafuatia mchakato wa majadiliano pamoja na watu kukutana na kwamba, amani kwa hakika, ni tunda la mahusiano ambayo yanawatambua na kuwakaribisha wengine katika hadhi yao isiyoweza kuondolewa.
Akili ya mwanadamu, kwa upande wake, kimsingi ni ya busara: inaweza kukua ikiwa tu, inabaki kuwa na hamu na wazi kwa nyanja zote za ukweli, na ikiwa inafahamu kuwasiliana katika uhuru na kwamba, haya ni matunda ya uvumbuzi wake. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana kwa makini; kusikiliza kabla ya kuzungumza na kutenda “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika; kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu.” Yak 1:19-20. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kusikiliza, ukimya na kuzungumza maneno ya kweli ili kupata mwelekeo wa ujumla utakaosaidia ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Ukosefu wa kubadilika kiakili ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga, ili kuwajenga waamini na watu wenye mapenzi mema uwezo wa kubadilika kwa kutumia elimu, ili watu wasiwe wagumu, lakini wanyumbulike, huku wakiwa wazi kwa wengine na katika udugu. Watambue na kuthamini yaliyopita na kuyaweka katika majadiliano. Ndoto ya udugu katika amani isishie kwenye majadiliano ya kidini tu, bali imwilishwe katika ujirani mwema, kwa kusikilizana, kuangaliana na kufahamiana; kimsingi huu ndio muhtasari wa neno majadiliano. Waamini wathubutu kutoka katika miundombinu yao, wajenge na kukuza utamaduni wa kusikilizana ili kujifunza kupendana na kwa njia hii, kumpenda hata Mwenyezi Mungu.