Tafuta

Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, Alhamisi tarehe 8 Februari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, Alhamisi tarehe 8 Februari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kumbukizi ya Miaka 60 Hati ya Liturujia ya Kanisa: Majiundo Makini ya Watu wa Mungu

Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, Alhamisi tarehe 8 Februari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika hotuba yake amekazia kuhusu: Kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wachapishe Hati Kuhusu Liturujia ya Kanisa; Uaminifu wa Kanisa; Upyaisho wa Liturujia ya Kanisa, Majiundo ya Wahudumu wa Liturujia pamoja na Watu wa Mungu katika ujumla wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kuanzia tarehe 6 Februari hadi tarehe 10 Februari 2024 linaadhimisha Mkutano wake wa Mwaka kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Nendeni, mkatuandalie Pasaka tupate kuila” na kwa Lugha ya Kilatini “Euntes parate nobis Pascha” Lk 22:8 Huu ni muda muafaka kwa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kujadiliana kuhusu: fursa, matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika majiundo ya Liturujia katika Kanisa kwa sasa. Hii ni nafasi ya kutafakari kuhusu Katiba ya Liturujia ya Kanisa, kama inavyobainishwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati yake ya “Sacrosanctum Concilium” yaani kuhusu Liturujia ya Kanisa. Hii ni hati inayojadili pamoja na mambo mengine kuhusu: Kanuni za jumla za marekebisho na ukuzaji wa Liturujia Takatifu; Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sakramenti nyingine na Visakramenti; Liturujia ya Vipindi vya Kanisa, Mwaka wa Liturujia ya Kanisa, Muziki Mtakatifu; Sanaa Takatifu na Vifaa Vitakatifu pamoja na nyongeza. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanahimiza malezi ya Kiliturujia na ushiriki hai wa waamini katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa kuzingatia marekebisho ya Liturujia Takatifu. Rej. SC, 16. Sanjari na kuendeleza malezi na majiundo endelevu kwa Wakleri pamoja na waamini walei. Rej. SC 16. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.” Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo Yesu na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli.

Majiundo makini ya Kiliturujia ya watu wa Mungu ni muhimu
Majiundo makini ya Kiliturujia ya watu wa Mungu ni muhimu

Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, Alhamisi tarehe 8 Februari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika hotuba yake amekazia kuhusu: Kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wachapishe Hati Kuhusu Liturujia ya Kanisa; Uaminifu wa Kanisa; Upyaisho wa Liturujia ya Kanisa, Majiundo ya Wahudumu wa Liturujia pamoja na Watu wa Mungu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican waliazimu kukuza kila siku maisha ya Kikristo kati ya waamini; kuzilinganisha taratibu zile zinazobadilika na mahitaji mamboleo; kuyahimiza mambo yale yote yanayosaidia kuleta umoja kati ya waamini; kuyaimarisha yale yote yanayofaa kwa kuwaita wote kundini mwa Kanisa. Mababa wanajali kwa namna ya pekee kurekebisha na kukuza Liturujia: kiroho, kichungaji, kiekumene na kimisionari na kwamba, marekebisho ya Liturujia ya Kanisa ndicho kiini cha marekebisho ya Kanisa, ili kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa Kanisa. Marekebisho ya Kanisa hayana budi kujikita katika uaminifu kwa Kristo Mchumba wake, hadi ukamilifu wake, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Mama na kwamba, Kristo aliye hai ndicho kiini cha marekebisho ya Kanisa ili kuwawezesha watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika Liturujia ya Kanisa “Actuoasa participatio” hali inayopyaisha zawadi ya Sakramenti ya Ubatizo. Hii ni changamoto pia kwa Kanisa kuendeleza majiundo kwa waamini walei kwa kutambua kwamba, Liturujia ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Kipaumbele cha kwanza ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa, ili kwa njia yao waweze kuwasindikiza na kuwasaidia waamini walei kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Kristo aliye hai anayeleta mabadiliko katika maisha.

Muhimu: Malezi, makuzi na majiundo ya Kiliturujia
Muhimu: Malezi, makuzi na majiundo ya Kiliturujia

Katiba ya Kitume inayojulikana kama “Praedicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inakazia kuhusu malezi na majiundo ya Kiliturujia kwa Mabaraza ya Kipapa kushirikiana kikamilifu. Haya ni: Baraza la Kipapa la Elimu, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri pamoja na Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, ili kila Baraza liweze kutoa mchango wake kwa kutambua kwamba, Liturujia ya Kanisa ni kilele ambapo kazi ya Kanisa inaelekea, na papo hapo ni chemchemi zinamotoka nguvu zake zote. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, katika ratiba ya masomo, Majandokasisi wanapata majiundo ya Liturujia ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, hata waamini walei wanapaswa kupatiwa malezi, makuzi na majiundo ya Kiliturujia, wanapokusanyika kuadhimisha Siku ya Bwana au katika Sikukuu na Sherehe za Mwaka wa Liturujia wa Kanisa. Hizi ni fursa za kwanza kabisa kwa majiundo ya walei na kwamba, wahakikishe kuwa wanashiriki kikamilifu katika maandalizi ya Sikukuu za watakatifu walinzi na waombezi wa Parokia na Majimbo yao, ili kutambua maana ya maadhimisho ya Fumbo la Wokovu.

Kumbukumbu ya Miaka 60 ya Hati Kuhusu Liturujia ya Kanisa
Kumbukumbu ya Miaka 60 ya Hati Kuhusu Liturujia ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Nendeni, mkatuandalie Pasaka tupate kuila” na kwa Lugha ya Kilatini “Euntes parate nobis Pascha” Lk 22:8 ni maneno ya Kristo Yesu yanayokazia umuhimu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kujikita katika majiundo, malezi na makuzi ya Liturujia ya Kanisa, ili hatimaye, kila mwamini aweze kuliishi vyema Fumbo la Pasaka kama mtu binafsi na kama jumuiya ya waamini. Hii ni dhamana na wajibu mkubwa na ulio bora, kwani hii ni kazi inayofanyika ili kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanaadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa utambuzi na kwa ukamilifu, ili hatimaye, waweze kuwa na maisha katika Kristo Yesu.

Liturujia ya Kanisa
08 February 2024, 16:55