Kwaresima Ni Muda Muafaka wa Maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Jubilei ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024. Huu ni mwaliko kwa waamini katika kipindi hiki cha Kwaresima anasema Baba Mtakatifu Francisko kujikita zaidi katika maisha ya sala, ili kuweza kutambua uwepo endelevu na angavu wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao.
Mafungo ya maisha ya kiroho yawasaidie waamini kukuza na kudumisha: Moyo wa Sala, Ibada na Majitoleo kwa Mwenyezi Mungu pamoja na Kanisa lake. Ni wakati wa kufanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu, tayari kulimwilisha katika uhalisia wa maisha, wito na vipaumbele katika maisha. Ni wajibu wa waamini kutambua uwepo wa Mungu katika kazi ya uumbaji, bila ya kumwogopa. Itakumbukwa kwamba, wakati fulani katika maisha yao, Mitume walishikwa na woga, kwa sababu hawakuwa na imani thabiti kiasi cha kumwomba Kristo Yesu awaongezee imani. Rej. Lk 17:5. Hali hii inaweza kumkuta mwamini ikiwa kama hawezi kuzamisha mahusiano na mafungamano yake ya dhati na Yesu Kristo na kusahau kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na msamaha kwa wale wote wanaomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2024 unanogeshwa na kauli mbiu “Kupitia Jangwani Mungu Anatuongoza Kwenye Uhuru: Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.” Kut 20:2. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anakazia zaidi wito wa ukombozi kutoka utumwani, ili kukutana na Mungu, huku wakiacha nyuma yao kongwa la utumwa, mwaliko kwa Kipindi hiki cha Kwaresima kufungua macho yao ili kujionea hali halisi. Katika safari ya kutoka utumwani, ni Mwenyezi Mungu anayeona, ongoza na kuwakirimia waja wake uhuru kamili. Kwaresima ni mwaliko wa kutambua ukuu wa Mungu, toba, wongofu wa ndani sanjari na kuambata uhuru na kwamba, haya ni mapambano ya jangwa la maisha ya kiroho.
Kwaresima ni kipindi cha kujizatiti katika sala na matendo ya huruma kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema, tayari kumwilisha wema, huruma na upendo wa Mungu kwa watu waliojeruhiwa: kiroho na kimwili. Ni kipindi cha kujikita katika utekelezaji wa maamuzi ya kijumuiya. Ni katika muktadha wa mafungo ya maisha ya kiroho, kuanzia Dominika jioni tarehe 18 hadi tarehe 23 Februari 2024, Baba Mtakatifu pamoja na viongozi wa Sekretarieti kuu ya Vatican wanafanya mafungo binafsi, kama sehemu ya maandalizi ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana na Maadhimisho ya Mwaka wa Sala. Kumbe, Jumatano tarehe 21 Februari 2024 hakutakuwepo na Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya wageni na mahujaji. Kwaresima ni Kipindi cha Kupyaisha Imani, Matumaini na Mapendo.” Baba Mtakatifu anakazia: Imani inayowaalika waamini kukubali ukweli na kuushuhudia mbele ya Mungu na jirani zao. Matumaini ni sawa kama na chemchemi ya maji hai yanayowawezesha waamini kusonga mbele na safari yao. Upendo, kwa kufuata nyayo za Kristo Yesu mintarafu huruma kwa watu wote, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na matumaini. Huu ni muda muafaka wa kusali na kutafakari, tayari kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Ni muda wa kwenda jangwani ili kujichotea nguvu za maisha ya kiroho, tayari kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuliandama Kanisa na jamii katika ujumla wake. “Jangwa” au "Upweke mtakatifu" ni muhimu sana katika maisha na utume wa waamini ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wao. Ni baada ya Yesu kubatizwa na Roho kutua kama njiwa juu yake. Roho huyo huyo aliyetua juu ya Yesu, katika Injili ya ya Dominika ya kwanza ya Kwaresima Mwaka B, anamtoa Yesu na kumpeleka jangwani. Huko anakaa siku 40 akijaribiwa na Shetani, Ibilisi. Hizi ni alama zenye maana kubwa sana katika utume wa Yesu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua kuwa “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwa kuzingatia historia ya Waisraeli waliosafiri jangwani kwa miaka 40 kuelekea nchi ya ahadi, jangwa lilikuwa ni mahala pa kujaribiwa uamifu, mahala pa kutakaswa na mahala pia pa kuonja wema, upendo na huruma ya Mungu. Wakiwa jangwani Mungu aliwaonesha upendo wake mkuu kwa kuwalinda, kuwaongoza na kuwapatia chakula. Wakristo wanahamasishwa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, huku wakiendelea kukita maisha yao katika sala, silaha madhubuti ya maisha ya kiroho. Mwenyezi Mungu anawataka waamini kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano thabiti pamoja naye kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kielelezo cha moyo wa shukrani kwa wito na zawadi maisha ambayo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake! Kwa wale wote ambao Mwenyezi Mungu amewapaka mafuta na kuwaweka wakfu kuwa ni makuhani wake wanapaswa kutambua kwamba, huduma ya kwanza wanayopaswa kuipatia kipaumbele katika maisha, wito na utume wao ni sala kwa ajili ya kuwaombea walimwengu ambao wanakumbana na magonjwa na wengi wao wamejeruhiwa sana. Wakleri wajenge utamaduni wa kusali daima, kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha tafakari hii katika maisha na utume wao kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wawe ni watu wakarimu kwa kutambua kwamba, wameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mashuhuda na vyombo vya neema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.