Tafuta

Dominika tarehe 4 Februari 2024, Baba Mtakatifu Francisko amejiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuadhimisha Siku ya 46 ya Uhai Kitaifa nchini Italia. Dominika tarehe 4 Februari 2024, Baba Mtakatifu Francisko amejiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuadhimisha Siku ya 46 ya Uhai Kitaifa nchini Italia.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Maadhimisho ya Siku ya 46 ya Uhai Kitaita Nchini Italia 2024

Dominika tarehe 4 Februari 2024, Papa amejiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuadhimisha Siku ya 46 ya Uhai Kitaifa. Kauli mbiu "Nguvu ya maisha inatushangaza. Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuvuka migawanyiko ya kiitikadi, ili hatimaye, kutambua kwamba, maisha ya mwanadamu yana thamani kubwa na uwezo wa kushirikisha wengine. Injili ya Uhai dhidi ya...!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 4 Februari 2024, amejiunga na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuadhimisha Siku ya 46 ya Uhai Kitaifa nchini Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu "Nguvu ya maisha inatushangaza. Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuvuka migawanyiko ya kiitikadi, ili hatimaye, kutambua kwamba, maisha ya mwanadamu yana thamani kubwa na uwezo wa kushirikisha wengine. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai” kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo.

Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI., Dominika tarehe 4 Februari 2024 linaadhimisha Siku ya 46 ya Uhai Kitaifa nchini Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu "Nguvu ya maisha inatushangaza. Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasikitika kuona maisha ya watu wengi yanapotea, nguvu ya maisha inashangaza; umuhimu wa maisha, kukaribisha na kupokea maisha kwa pamoja. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasikitika kuona kwamba, maisha ya watu wengi yanapotea kama ndoto ya mchana: Haya ni maisha ya askari, raia, wanawake, watoto na wazee; maisha ya wakimbizi na wahamiaji yanaonekana kana kwamba, hayana thamani, kusikia wamepoteza maisha huko kwenye Bahari ya Mediterrania hii si habari tena yakusikitisha. Maisha ya wafanyakazi wengi yamekuwa kama ni bidhaa kwa kufanyishwa kazi za suluba na katika mazingira magumu hatarishi. Maisha ya wanawake wengi yako hatarini kutokana na vipigo, ukatili wa majumbani sanjari na mfumo dume. Katika hali na mazingira kama haya, watu kukumbatia sera za utoaji mimba linakuwa ni jambo la kawaida; utu, heshima, haki msingi za binadamu na usawa ni mambo yanayowekwa rehani. Maaskofu wanakazia sana kuhusu nguvu ya maisha inayoshangaza dhidi ya ubaguzi na chuki. Mara ngapi, wagonjwa wanaonyanyaswa wamekuwa ni chemchemi ya faraja kwa wale walio wazima? Maisha ya walemavu kimekuwa ni chanzo cha furaha ya kweli? Jambo la msingi ni kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu; msamaha na upatanisho wa kweli. Kwa hakika maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, licha ya matatizo na changamoto zake.

Tangazeni na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Tangazeni na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo

Maaskofu wanakazia umuhimu wa maisha, utu na heshima ya binadamu na kwamba, maisha ya binadamu yanapaswa kulindwa na kudumishwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi dhidi ya Injili ya uhai, kwa kukumbatia sera za utoaji mimba na kifo laini. Kumbe, maendeleo makubwa ya sayansi ya tiba ya mwanadamu kisiwe ni kikwazo cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maadhimisho ya Siku ya 46 ya Uhai Kitaifa nchini Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu "Nguvu ya maisha inatushangaza. Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36 ni fursa ya kukaribisha na kupokea maisha kwa pamoja. Kigezo muhimu cha maendeleo yoyote ya jamii ni kuona jinsi ambavyo jamii hii inavyojitahidi kulinda maisha hasa ya: maskini, wanyonge na dhaifu. Waamini wanalitazama fumbo la maisha ya binadamu na kutambua kutoka ndani mwake, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Muumbaji, ulinzi na ukuaji wake, katika hali zote ni dhamana nyeti inayofumbatwa katika imani na upendo. Maadhimisho haya yanabeba ndani mwake, majadiliano ya kidini na kiekumene, mwaliko wa kumheshimu Mwenyezi Mungu na kumtumikia kwa njia ya ulinzi na thamani ya maisha ya mwanadamu, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na kwamba, Injili ya uhai ni zawadi inayostahili kukaribishwa, chemchemi ya amana na utajiri mkubwa wa wingi wa ubinadamu na maisha ya kiroho kwa ulimwengu unaohitaji zaidi.

Injili ya Uhai
05 February 2024, 15:24