Mapadre Wanapaswa Kuwa ni Vyombo na Mashuhuda wa Furaha ya Injili na Huduma!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, majiundo ya awali na endelevu kwa ajili ya Makleri ni muhimu sana ili kuwawezesha kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kati ya watu wanaowahudumia. Anakazia umuhimu wa maisha ya sala tangu mwanzo ili hatimaye, Mapadre waweze kuchota nguvu ya kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara, katika maisha na utume wa Kanisa. Wawe ni viongozi wanaojitaabisha kusoma Neno la Mungu, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wao. Maandiko Matakatifu yasomwe na kueleweka kwa msaada wa Roho Mtakatifu na chini ya uongozi wa Ualimu wa Kanisa, kwa kuzingatia yaliyomo katika Maandiko yote katika umoja wake; kwa kuheshimu Mapokeo hai ya Kanisa na mwishoni kwa kujali ulinganifu wa imani, yaani mshikamano wa kweli zote za imani! Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu pamoja na Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 6 hadi 10 Februari 2024 linaendesha Kongamano la Kimataifa juu ya Majiundo Endelevu ya Wakleri katika maisha na utume wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.” 2 Tim 1:6.
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri tarehe 8 Desemba 2016 lilichapisha Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” Utangulizi wa mwongozo huu unabainisha changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kulinda, kukuza na kudumisha wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre. Huu ni wito wenye thamani kubwa katika maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuhudumiwa kwa umakini mkubwa kwa kuheshimu dhamiri nyofu, wajibu unaotekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, ili kweli Wakleri waweze kung’ara kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia! Mwongozo unatoa kwa muhtasari: Sheria, kanuni na mambo msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unabainisha wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; Waratibu wa Seminari kitaifa na Kimataifa pamoja na mwongozo wa malezi ya Seminari moja moja. Kumbe, kongamano hili linachota amana na utajiri wake kutoka katika Mwongozo wa Malezi ya Kipadre, lengo ni kuimarisha majiundo endelevu miongoni mwa mapadre. Mada ambazo zimewasilishwa ni pamoja na: Mapadre katika mabadiliko makubwa katika Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; Majiundo endelevu: kiutu, kiakili na kichungaji, kwa kutambua kwamba, kimsingi Mapadre ni watu wa Mungu na wahudumu wa Injili; Maisha ya kijumuiya, ili kuwawezesha Mapadre kujisikia kwamba, wako nyumbani; Maisha ya Kipadre na Udugu wa Kipadre; Majiundo ya Kimisionari na Mbinu Mkakati Mpya wa Shughuli za kichungaji; Maisha na Utume wa Mtakatifu Petro na Paulo. Hii imekuwa ni nafasi ya kushirikishana: manga’muzi, changamoto, fursa na matarajio kwa siku za usoni, tayari kushusha nyavu zao tena mintarafu Neno la Mungu, hata kama wamefanya kazi ya kuchosha usiku kucha. Rej. Lk 5: 4-5; Yn 21:6.
Hii ina maana kujitaabisha kutafuta lugha na nyenzo zinazosaidia kukoleza majiundo endelevu na kwamba, kimsingi, Mapadre hawana majibu yote ya changamoto za maisha na utume wao. Kumbe, Kongamano hili linalenga pamoja na mambo mengine kupyaisha zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre; Kugundua tena kwamba, wao ni Wapakwa wa Bwana, tayari kuwasha moto wa ari na huduma ya kitume kwa watu wa Mungu. Washiriki wa Kongamano hili la Majiundo endelevu, Alhamisi tarehe 8 Februari 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika hotuba yake: Amewashukuru Mapadre kwa huduma kwa watu wa Mungu; amewataka wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha; wawe ni sehemu ya watu wa Mungu na wazalishaji wa huduma. Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungano na Kristo Yesu, anayewaokoa kutoka katika ubinafsi na uchoyo wao tayari kuwakirimia maana ya maisha, upendo na matumaini, kwa kutambua kwamba, kwa hakika wanapendwa na Mungu mwingi wa huruma na mapendo, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wanapaswa kuwa ni mashuhuda kabla ya kuwa ni waalimu.
Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” unakazia pamoja na mambo mengine kwamba, Mapadre ni watumishi na wamisionari wa Ufalme wa Mungu; mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili, vinginevyo Mapadre wanaweza kujisikia kuwa ni wamiliki wa Daraja Takatifu. Kumbe, Mapadre wanapaswa kuwa ni Mitume wa Yesu kwa njia mfumo wa maisha na utume wao, vinginevyo wanaweza kujikuta wakimezwa na malimwengu na hivyo kutopea katika uharibifu. Majiundo endelevu ya Makleri yapewe kipaumbele cha kwanza, tayari kutoa huduma kwa watu wa Mungu katika marika yote tayari kupambana na changamoto za maisha na utume wa Kipadre, ili hatimaye faraja ya Injili iweze kuwafikia watu wote wa Mungu kwa njia ya utu uliofundwa na Roho Mtakatifu. Mapadre watambue kwamba, wao ni sehemu ya hija ya safari ya watu wa Mungu katika maisha yao wakati wa raha, furaha na machungu ya maisha. Daima Mapadre na Maaskofu washikamane na kufungamana na watu wa Mungu, ili kujenga na kudumisha udugu wa Kipadre na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Mapadre wawe ni wazalishaji wa huduma kwa mfano wa Kristo Yesu mchungaji mwema alivyofanya siku ile iliyotangulia kuteswa wake. Katika huduma, majiundo endelevu yanang’arisha: weza na uzuri ambao Padre anaubeba ndani mwake; mwanga unaomulika mapungufu pamoja na madonda yake, tayari kumfunda, ili kuwahudumia wote; kuwasaidia watu wa Mungu kufanya mang’amuzi maisha yao ya kiroho sanjari na kuwasindikiza katika shida, mahangaiko na fursa katika maisha yao tayari kukabiliana na changamoto za maisha, tayari kubeba vyema Misalaba ya maisha na utume wao, kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Mapadre wawe na huruma; watu wenye uwezo wa kusamehe na kusahau, lakini daima wakumbuke kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, kiini cha maisha na utume wao wa Kipadre; wao ni sehemu ya watu wapendwa wa Mungu na kwamba, wao ni wazalishaji wa huduma, tayari kujikita katika huruma, ili kweli wawe ni Mababa na wachungaji wa maisha ya kiroho. Bikira Maria, Mfariji awalinde na kuwaongoza katika maisha na utume wao, ili waweze kuwa ni faraja kwa watu wa Mungu.