Nia za sala mwezi Machi 2024:Kwa ajili ya mashahidi wa nyakati zetu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika nia ya mwezi Machi 2024, ambapo tarehe 24 Machi ni Siku ya maombi na kufunga kwa ajili ya kuwaombea wafiadini wamisionari, Baba Mtakatifu Francisko anaweka wakfu kwa nia yake katika njia ya video iliyotolewa na Mtandao wa Maombi ya Papa Kimataifa kwa ajili ya wale wanaoishi imani yao licha ya mateso na ukosefu wa uhuru na ushuhuda wao ni ishara kwamba tuko kwenye njia iliyo sawa. Tunachapisha ujumbe kamili wa Baba Mtakatifu ambao anazungumza kwa lugha ya kihipania. “Mwezi huu, ninataka kukuelezea historia ambayo inaakisi Kanisa la leo hii. Ni historia ya shahidi asiyejulikana sana wa imani. Nilipotembelea kambi ya wakimbizi huko Lesbos, mwanamume mmoja aliniambia, “Baba, mimi ni Mwislamu. Mke wangu alikuwa Mkristo. Magaidi walipokuja kwetu, wakatutazama na kutuuliza ni tulikuwa na dini gani. Walimsogelea mke wangu wakiwa na msalaba na kumwambia autupe chini. Hakufanya hivyo, na walimkata koo mbele yangu.” Ndicho kilichotokea.”
Baba Mtakatifu akiendelea anabainisha kuwa “Ninajua hakuwa na kinyongo. Alikazia fikira juu ya mfano wa upendo wa mke wake upendo kwa Kristo ambao ulimfanya akubali, na kuwa mwaminifu hadi kufa. Kaka, dada, daima kutakuwa na wafiadini miongoni mwetu. Hii ni ishara kwamba tuko kwenye njia sahihi. Mtu anayejua aliniambia kuna wafiadini wengi leo hii kuliko mwanzoni mwa Ukristo. Ujasiri wa mashahidi, ushuhuda wa mashahidi, ni baraka kwa kila mtu.” Kwa kuhitimisha Papa Francisko anasema: “Tuombe kwamba wale wanaohatarisha maisha yao kwa ajili ya Injili katika sehemu mbalimbali za dunia waweze kulijaza Kanisa kwa ujasiri na msukumo wao wa kimisionari. Na kuwa wazi kwa neema ya kifo cha kishahidi.”
Maombi ya Papa kupitia majukwa mbali mbali
Mwaliko ambao Papa Francisko anautoa kwa njia ya video kwa mwezi Machi unatolewa katika Mtandao wa Maombi ya ya Kimataifa wa nia za Papa kupitia majukwaa mbali mbali kama vile: YouTube, Facebook, na tovuti mbali mbali. Ujumbe wa video wa Papa wa mwezi wa Machi, uliotafsiriwa katika lugha 23 na kutangazwa kwa vyombo vya habari katika nchi 114, uliundwa kwa msaada wa Baraza la Kpapa la Kanisa Hitaji (ACN) ambalo ni Shirika la kimataifa la kutoa misaada la Kikatoliki na Mfuko wa kipapa ambao utume wake ni kuwasaidia waamini popote walipo wanapoteswa, kuonewa au katika matatizo kwa njia ya taarifa, sala na matendo.
Wafiadini ni wengi sana katika nyakati hizi
Katika ujumbe huo ambao Papa anatualika kutafakari juu ya wale wanaotoa maisha yao kama mashahidi wa Kristo, juu ya historia zao, na ndiyo maana yanajumuisha pia picha za jumuiya za Kikristo katika hatari na mifano ya ujasiri, kama ile ya mtumishi wa kwanza wa Mungu wa Pakistan, Akash Bashir, ambaye alikufa akiwa na umri wa miaka 20 mnamo 2015 akizuia shambulio la kigaidi kwenye Kanisa lililojaa wamini huko Lahore. Papa anaposema kuwa “Kuna mashahidi wengi leo kuliko mwanzo wa Ukristo,” ni msisiitzao wa kukumba hata takwimu zilizotolewa na wataalamu na kuakisi jinsi ambavyo mada ya Wakristo wanaoteswa ambao hutoa maisha yao kwa ajili ya imani yao ni muhimu sana.
Hii inatosha kufikiria mnamo mwaka 2023 tu, Shirika la Kipapa la Makanisa Hitaji lilipokea ripoti za watu waliouawa au kutekwa nyara kwa ajili ya imani yao katika nchi 40, ikiwa ni pamoja na Nigeria, ambapo idadi kubwa ya mauaji yalirekodiwa, Pakistan, ambako maeneo ya ibada na nyumba za Wakristo katika Jimbo la Faisalabad, huko Jaranwala, na Burkina Faso, ambako Wakatoliki wa Débé walifukuzwa kutoka kijiji chao kwa sababu ya imani yao tu.
Ni muhimu kuombea waathiriwa
Katika muktadha huo, Regina Lynch, rais mtendaji wa Mfuko wa kipapa, alisema kwamba “uhuru wa kidini, unaotambuliwa katika Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu, ni haki isiyoweza kubatilishwana kwamba hakuna Mkristo anayepaswa kupoteza maisha yake kwa kuitekeleza. Ni jambo la msingi kuhakikisha haki ya kutenda imani kama sehemu ya hadhi ya wanadamu wote.” Kwa njia hiyo, “nia ya Papa Francisko kwa mwezi huu ni muhimu sana kuhimiza maombi kwa ajili ya waathirika wa mateso pamoja na kuunga mkono wale wanaokabiliwa na ubaguzi kwa sababu ya imani yao. Zaidi ya hayo, lazima tushirikishe wanasiasa kutetea haki za walio hatarini zaidi,” alisema Lynch.
Tumeitwa kushuhudia Kristo kwa maisha yote
Kwa upande wa Padre Frédéric Fornos, mkurugenzi wa kimataifa wa Mtandao wa Maombi ya Papa, alikumbuka kutiwa moyo na Mtakatifu Francis wa Assisi ambaye alisema “kuhubiri Injili, na ikibidi kutumia “hata maneno.” Padre alisema “Tumeitwa kushuhudia Kristo kwa maisha yetu yote. Mfiadini ni shahidi wa Kristo ambaye kuwepo kwake ni ushuhuda hai yaani, anajumuisha Injili kwa kuhatarisha maisha yake mwenyewe, bila kutumia vurugu.” Na kwa hivyo nia ya maombi ya Papa Francis inatuhimiza kutafakari "jinsi tunavyomshuhudia Kristo mahali tunapojikuta", alibainisha Padre Fornos, akiongeza kwamba: "sio wote tumeitwa kuhatarisha maisha yetu ili kuwa waaminifu kwa Yesu Kristo." Lakini hata hivyo, inawezekana kujiuliza sana kama "unapokabiliwa na hali zinazoenda kinyume na maadili ya Kikristo, kinyume na Injili", katika kazi ya mtu, katika shughuli zake, katika mzunguko wa mtu wa kijamii au katika familia ya mtu, mtu unachukua au la nafasi ya kufuata njia ya Kristo licha ya magumu na changamoto zinazoweza kutokea."?