Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika, tarehe 18 Februari 2024 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, ameyaelekeza macho na mawazo yake katika Jimbo la Cabo Delgado mji mkuu wa Pemba, nchini Msumbiji ambako kumerejea tena vurugu dhidi ya watu wasiokuwa na ulinzi. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika, tarehe 18 Februari 2024 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, ameyaelekeza macho na mawazo yake katika Jimbo la Cabo Delgado mji mkuu wa Pemba, nchini Msumbiji ambako kumerejea tena vurugu dhidi ya watu wasiokuwa na ulinzi.  (AFP or licensors)

Papa Francisko Asikitishwa na Mashambulizi ya Kigaidi Nchini Msumbiji

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika, tarehe 18 Februari 2024 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, ameyaelekeza macho na mawazo yake katika Jimbo la Cabo Delgado mji mkuu wa Pemba, nchini Msumbiji ambako kumerejea tena vurugu dhidi ya watu wasiokuwa na ulinzi. Kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa miundombinu, utekaji nyara, sanjari na ukosefu wa ulinzi na usalama. Kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu, utekaji nyara wa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji ni kati ya maeneo ambayo yana utajiri mkubwa wa gesiasilia yenye thamani ya takribani dola bilioni 60. Lakini hili ni eneo ambalo limekuwa ni tishio kubwa kwa usalama na maisha ya wananchi wengi nchini Msumbiji kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na vikosi vya kigaidi. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita zaidi ya watu 2, 400 wameuwawa kikatili na makazi yao kuchomwa moto! Baba Mtakatifu Francisko, Dominika, tarehe 18 Februari 2024 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, ameyaelekeza macho na mawazo yake katika Jimbo la Cabo Delgado mji mkuu wa Pemba, nchini Msumbiji ambako kumerejea tena vurugu dhidi ya watu wasiokuwa na ulinzi. Kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa miundombinu, utekaji nyara, sanjari na ukosefu wa ulinzi na usalama. Hii ni vita inayoendeshwa na magaidi wa dola ya kiislam wanaojulikana kama “Ahl al-Sunnah wa al-jama’ah, IS. Tayari wamekwisha choma moto Makanisa kadhaa pamoja na makazi ya watu na hivyo kupelekea idadi ya watu kukosa makazi maalum. Inasikitisha kuona kwamba, hata Parokia ya Mama Yetu wa Afrika ilichomwa moto, huko Mazeze. Baba Mtakatifu anakaza kusema, vita daima ni kushindwa kwa binadamu, watu wamechoka na vita na kwamba, siku zote vita havina maana kwani vilaleta vifo, uharibifu na kamwe havitakuwa ni suluhu ya matatizo na changamoto anazokumbana nazo mwanadamu. Badala yake, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuendelea kujizatiti katika sala bila kuchoka, ili kumwomba Mwenyezi Mungu zawadi ya akili na nyoyo zinazoweza kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa amani. Ulinzi na usalama sanjari na mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi ni kati ya vipaumbele vya Serikali ya Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji.

Madhara ya vita na mashambulizi ya kigaidi nchini Msumbiji
Madhara ya vita na mashambulizi ya kigaidi nchini Msumbiji

Itakumbukwa kwamba, kauli mbiu iliyongoza hija kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji kuanzia tarehe 4-6 Septemba 2019 ilikuwa ni: matumaini, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu katika hotuba yake alipenda kuonesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano na familia ya Mungu nchini Msumbiji kutokana na majanga asilia. Alikazia umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Baba Mtakatifu aliwashukuru watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa mapokezi na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake nchini Msumbiji. Aliwapongeza kwa utajiri wa tamaduni, uoto wa asili, furaha na matumaini ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Aliwashakuru wadau wote waliojisadaka ili kupyaisha tena mchakato wa amani na upatanisho nchini Msumbiji. Baba Mtakatifu aliipongeza na kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imesimama kidete ili kuhakikisha kwamba, mchakato wa amani na upatanisho wa kitaifa, licha ya matatizo na changamoto zake, unarejea tena na matokeo yake ni kutiwa saini kwa Mkataba wa Amani huko Serra da Gorongosa kati ya Chama cha FRELIMO na RENAMO. Mkataba huu ukafutilia mbali uhasama kati ya ndugu wamoja nchini Msumbiji na kwamba, Mkataba huu utaimarisha zaidi Mkataba wa Amani uliotiwa saini mjini Roma kunako mwaka 1992. Matunda ya mchakato huu yameanza kuonekana kwa kutambuana kama ndugu, wenye dhamana na wajibu wa kuendeleza ustawi wa nchi ya Msumbiji. Ujasiri unaleta amani ya kweli, unatafuta na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi. Wananchi wa Msumbiji wameteseka sana na madhara ya vita na kinzani za kijamii, lakini hawakutaka kukubali kutawalia na chuki, uhasama na mtindo wa kutaka kulipizana kisasi na kwamba, vita haikuwa na usemi wa mwisho katika mustakabali wa wananchi wa Msumbiji.

Papa Francisko anasema, watu nchini Msumbiji wana kiu ya haki na amani
Papa Francisko anasema, watu nchini Msumbiji wana kiu ya haki na amani

Vita imeharibu sana makazi ya watu, imewatumbukiza wananchi katika baa la njaa, ujinga na maradhi. Vita imewakosesha watu nyumba za sala na ibada; imepelekea watu kukosa fursa za ajira na kwamba, kuna umati mkubwa wa wananchi wa Msumbiji walilazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta: usalama na hifadhi ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 Septemba, 2019 aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zimpeto uliosheheni watu kutoka sehemu mbali mbali za Msumbiji. Katika mahubiri yake alikazia umuhimu wa familia ya Mungu nchini Msumbiji kujikita katika mchakato wa upatanisho ili kuondokana na vita, chuki na uhasama. Ni wakati wa kusamehe na kusahau, ili kumwilisha Amri ya upendo inayovunjilia mbali kuta za utengano. Ni muda muafaka wa kujizatiti katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Amani ya kweli inabubujika kutoka katika undani wa mwamini mwenyewe! Baba Mtakatifu alisema, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kuwasikiliza na kuwapenda adui zao. Haya ni maneno ambayo yanapaswa kupewa uzito wa pekee hata na watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa kutambua na kuguswa na uhalisia wa maisha yao. Adui ni watu wanao wachukia na kuwatenga wengine; ni watu wanaowachafulia wengine utu na heshima yao pamoja na kuwakashfu jirani zao. Wananchi wengi wa Msumbiji bado wana madonda ya vita, chuki na uhasama. Ni madonda yanayowagusa hata watu wengine ambao tayari wamekwisha tangulia mbele za haki, lakini kuna wengine bado wako hai. Kuna hatari kwamba, madonda ya zamani yataibuliwa tena na hivyo kukwamisha maendeleo yaliyokwisha kupatikana hadi wakati huu kama ilivyojitokeza huko Cabo Delgado.

Vita Msumbiji
20 February 2024, 15:12