Baba Mtakatifu amesema hali ya vita nchini Sudan kwa sasa ni tete na kwamba, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wahanga wa vita hii Baba Mtakatifu amesema hali ya vita nchini Sudan kwa sasa ni tete na kwamba, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wahanga wa vita hii   (AFP or licensors)

Hali ya Vita ya Wenyewe Kwa Wenyewe Sudan Ni Tete Sana!

Baba Mtakatifu Francisko amesema hali ya vita nchini Sudan kwa sasa ni tete na kwamba, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wahanga wa vita hii na anapenda kutoa wito kwa wahusika wakuu wa vita hii ya wenyewe kwa wenyewe, kuwajibika barabara ili kuhakikisha kwamba vita inakoma na misaada ya kiutu inawafakia waathirika. Amani ya kweli ni chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu; kinzani, misigano na utaifa ni kikwazo cha amani ya kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Vita kati ya Majenerali wawili Abdel Fattah al-Burhan, kiongozi wa Kikosi cha Wanajeshi wa Sudan (SAF), na Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti, mkuu wa Kikosi cha Dharura (RSF) nchini Sudan ni kielelezo cha uchu wa mali na madaraka. Majenerali wawili hao walifanya kazi sanjari na kufanya mapinduzi pamoja sasa vita vyao vya kuwania madaraka vinasaimbaratisha Sudan.  Vita hii ya wenyewe kwa wenyewe ni ya waasimu wawili. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 18 Februari 2024 amesema hali ya vita nchini Sudan kwa sasa ni tete na kwamba, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wahanga wa vita hii na anapenda kutoa wito kwa wahusika wakuu wa vita hii ya wenyewe kwa wenyewe, kuwajibika barabara ili kuhakikisha kwamba vita inakoma na misaada ya kiutu inawafakia waathirika.

Hali ya wananchi Sudan ni tete sana kutokana na vita
Hali ya wananchi Sudan ni tete sana kutokana na vita

Na kwa ushirikiano na msaada wa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waweze kupata suluhu ya amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu Sudan. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema: Amani ya kweli ni chachu ya maendeleo ya watu na kwamba, kinzani, misigano na utaifa usiokuwa na mashiko ni mambo yanayotishia amani. Kumbe, vita, migogoro na kinzani mbalimbali zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kujikita katika: sheria, haki, usawa, upendo; ukweli na uhuru, tunu ambazo zinaonesha umuhimu wa pekee hata katika ulimwengu mamboleo. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukazia kutotumia nguvu kuwa ndio unaopaswa kuwa ni mtindo wa maisha ya kisiasa ili kujenga na kudumisha amani duniani na anamwomba Mwenyezi Mungu awasaidie watu kuchota tunu hizi msingi kutoka katika undani wa maisha yao.

Amani ya kweli ni chachu ya maendeleo endelevu
Amani ya kweli ni chachu ya maendeleo endelevu

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na washirika wake wametoa wito wa kuongezewa dola bilioni 4.1 ili kukidhi mahitaji ya dharura ya kibinadamu ya raia wa Sudan ya wapatao milioni 1.5, ambao wamekimbilia Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan ya Kusini. Takribani watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu, ulinzi na usalama. Watu milioni 18 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Uhasama mkubwa unaendelea kuharibu mitandao ya usambazaji maji na miundombinu mingine muhimu ya kiraia nchini Sudan, na karibu robo tatu ya vituo vya afya havina huduma katika majimbo yaliyoathiriwa na migogoro. Magonjwa yakiwemo kipindupindu, surua na malaria yanaenea wakati ambapo theluthi mbili ya watu wanakosa huduma bora za afya. Baadhi ya watoto milioni 19 hawako shuleni na kwamba, kuna ukiukaji mkubwa wa haki msingi za binadamu sanjari na nyanyaso za kijinsia.

Papa Vita Sudan
20 February 2024, 14:35