Tafuta

Ilikuwa ni tarehe 24 Februari 2022, yaani miaka miwili iliyopita, Urusi ilipoivamia Ukraine na huo ukawa ni mwanzo wa vita ya kipuuzi kabisa. Ilikuwa ni tarehe 24 Februari 2022, yaani miaka miwili iliyopita, Urusi ilipoivamia Ukraine na huo ukawa ni mwanzo wa vita ya kipuuzi kabisa. 

Papa Francisko Kumbukizi ya Miaka Miwili Vita ya Urusi na Ukraine: 2022-2024

Vita kati ya Urusi na Ukraine: 2022-2024: Takwimu kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, raia wa Ukraine waliofariki dunia kutoka na vita walikuwa ni zaidi ya watu 10, 000, waliojeruhiwa ni raia 18, 500. Kuna watu milioni 1.4 hawana uhakika wa maji safi na salama; kuna familia 899.039 wanaopewa mahitaji msingi kama vile chakula, huduma ya afya na umeme na kwamba, kwa mwaka huu wa 2024, UNHCR linasema, linawahudumia zaidi ya watu milioni 2.7.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 24 Februari 2022, yaani miaka miwili iliyopita, Urusi ilipoivamia Ukraine na huo ukawa ni mwanzo wa vita ya kipuuzi kabisa, ambayo imesababisha mateso makubwa kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Ukraine. Baba Mtakatifu Francisko katika muktadha wa kumbukizi hii anasema, jambo la kujiuliza ni ikiwa kama kumekuwepo na juhudi za kutosha ili kukomesha vita hii?  Si rahisi kuweza kujibu kwamba, diplomasia ya Kimataifa ilitia nia ya dhati kabisa ili kuhakikisha kwamba, vita inakoma na amani inatawala. Baba Mtakatifu anasema, hakuna ushindi wa kweli unaojengwa na kusimikwa juu ya vifusi na damu ya watu wasiokuwa na hatia. Takwimu kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, raia wa Ukraine waliofariki dunia kutoka na vita walikuwa ni zaidi ya watu 10, 000, waliojeruhiwa ni raia 18, 500. Kuna watu milioni 1.4 hawana uhakika wa maji safi na salama; kuna familia 899.039 wanaopewa mahitaji msingi kama vile chakula, huduma ya afya na umeme na kwamba, kwa mwaka huu wa 2024, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR linasema, linawahudumia zaidi ya watu milioni 2.7. Ukraine ni nchi ambayo imeharibiwa sana na vita, kiasi cha kusababisha hasara ya Dola bilioni 564 hadi dola bilioni 600 na kwamba, ukarabati wa Ukraine, utachukua muda mrefu kuweza kurejea katika hali yake ya kawaida. Kuna watu milioni 6.4 waliolazimika kuikimbia Ukraine kwa kuhofia usalama wa maisha yao na hadi kufikia mwezi Septemba 2023 watu zaidi ya 900, 000 waliweza kurejea tena kwenye makazi yao na kati yao watu 298, 000 imewabidi kwenda kuishi mahali pengine nje ya makazi yao. Kiwango cha umaskini kimeongezeka kutoka asilimia 5.5% hadi kufikia asilimia 24.2%.

Vita kati ya Ukraine na Urusi vimesababisha madhara makubwa
Vita kati ya Ukraine na Urusi vimesababisha madhara makubwa

Katika vita hii isiyokuwa na macho kuna miji sita imeharibiwa vibaya sana kiasi kwamba, haifai tena kwa maisha ya binadamu. Kuna majimbo manne ambayo yamejitenga na kuwa ni sehemu ya Urusi. Inakadiriwa kwamba, vita hii imezalisha deni kiasi cha dola bilioni 108, hili ni deni la nje, litakalolipwa na Ukraine kwa kipindi cha miaka mingi ijayo. Wachambuzi wa mambo wanasema, tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia 1939-1945, hakuna nchi ya Ulaya iliyoivamia kijeshi nchi nyingine na kwa kiasi kikubwa ilionekana masuala ya kupigana vita yatabaki katika vitabu vya historia pekee. Kumbe, uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine umetia doa diplomasia na mahusiano ya Kimataifa. Urusi ilidai kwamba, uvamizi huu ulikuwa na lengo la kujiimarisha kimkakati upande wa Jeshi na pili ilikuwa ni kuondoa hatari za siasa za kibaguzi nchini Ukraine. Kimsingi vita hii imevunja makubaliano ya kuundwa kwa Jumuiya ya Nchi Huru, Mkataba wa nchi mbili kati ya Urusi na Ukraine, Mkataba wa mpaka unaotambulika kimataifa wa Urusi na Ukraine, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Sheria ya Helsinki ya 1975 pamoja na Mkataba wa Budapest.

Vita hii imetia doa diplomasia na ushirikiano wa Kimataifa
Vita hii imetia doa diplomasia na ushirikiano wa Kimataifa

Vita hii imepelekea kupanda zaidi kwa bei ya nishati ya mafuta na hivyo kuibua mnyororo wa kupanda kwa bei za uzalishaji, usafirishaji na ugavi wa bidhaa. Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba sasa nchi nyingi zimelazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza nishati ya mafuta kuliko kawaida na hili limeathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi husika na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kwenye mambo mengine muhimu. Urusi na Ukraine ni wazalishaji na wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Vita hii imeongeza gharama ya mazao ya nafaka na hivyo kupelekea baadhi ya nchi kukosa uhakika na usalama wa chakula. Nchi zile zilizokuwa zinafanya biashara ya moja kwa moja na Urusi pamoja na Ukraine zinajikuta zikiwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na vita kupamba moto. Baba Mtakatifu Francisko katika kumbukizi ya miaka miwili tangu kuzuka kwa vita kati ya Urusi na Ukraine, anatoa wito wa nguvu kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, vita hii inafikia ukomo, ili hatimaye, kuanza majadiliano ya amani katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kamwe amani haiwezi kujengwa kwenye vifusi na damu ya watu wasiokuwa na hatia!

Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu
Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu

Naye Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki la Kyiv-Halyč, nchini Ukraine, anawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kushikamana na wananchi wa Ukraine kwani mshikamano wa dhati unaokoa maisha, kwa sababu vita inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni kuhusu: Utume wa familia; Utume wa maombolezo sanjari na utume wa matumaini ya ufufuko wa wafu katikati ya maombolezo na maafa makubwa. Kwa upande wake, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, anasema Kanisa bado lina ndoto ya haki, amani na maridhiano kati ya Urusi na Ukraine. Litaendelea kuwa karibu na watu wote wa Mungu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Vatican kwa kutumia diplomasia ya Kimataifa, inaendelea kuwahamasisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, vita inakoma, amani inarejea tena kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ubalozi wa Vatican umeendelea na shughuli zake nchini Ukraine licha ya hatari kubwa iliyoko, kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na uwepo angavu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu wanaoteseka nchini Ukraine. Baba Mtakatifu ameendelea kuwasha moto wa ndoto ya amani kila mara alipobahatika kupata nafasi ya kuzungumza. Anasema, kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, vita kamwe si suluhu ya shida, changamoto na matatizo yanayoikabili Jumuiya ya Kimataifa. Haya ni maneno ya kinabii, lakini daima duniani kutakuwepo na “viongozi wababe” wanaopenda kujimwambafai kwa kutumia mtutu wa bunduki “kuwashikisha wengine adabu.”

Jumuiya ya Kimataifa haijaweka utashi wa kutosha kuzuia vita hii
Jumuiya ya Kimataifa haijaweka utashi wa kutosha kuzuia vita hii

Baba Mtakatifu anasema “dhana ya vita ya haki na halali” kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa siasa na utu na inabaki kuwa ni aibu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Mtakatifu Paulo VI tarehe 4 Oktoba 1965 alipokuwa analihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alikemea sana vita, akaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki na amani. Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa tarehe 11 Aprili 1963 anasema, amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya amani sehemu mbalimbali za dunia, licha ya shida, matatizo na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza kwenye uso wa dunia. Ndoto ya matumaini na amani ni muhimu kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukraine unaosimikwa katika mchakato wa haki, amani na upatanisho.

Vita Ukraine
23 February 2024, 14:13