Wakulima lazima wazingatiwe Wakulima lazima wazingatiwe 

Papa:tabianchi,rasilimali zinaporwa,migogoro ya kiuchumi inatishia maisha ya mamilioni ya watu

Papa aliwaandikia ujumbe washiriki katika kikao cha 47 cha Baraza la Wakuu wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo:njaa na umaskini lazima vishughulikiwe bila kusuluhisha mikakati ya kufikirika au ahadi zisizoweza kufikiwa lakini kwa kukuza matumaini yanayotokana na hatua za pamoja.Tushirikiane kujenga mfumo shirikishi zaidi wa kilimo na chakula.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekuma ujumbe wake kwa Rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo na wajumbe na wawakilishi wa kudumu wa Nchi Wanachama wote  kuwa na furaha ya kuwaelekea wao katika wakati wa mkutano huo wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo na kuchukua fursa hiyo kuwatumia salamu zake za dhati.  Papa amependa kuwashukuru kwa kujitolea, wakati na nguvu wanaazojitolea kupigania ili ulimwengu uwe bora, ambapo hakuna mtu anayeona kukiukwa utu wao na ambapo udugu unakuwa ukweli, chanzo cha furaha na matumaini kwa wote.

Dunia inakabiliwa na migawanyiko

Baba Mtakatifu anaandika kuwa leo, ulimwengu wetu unakabiliwa na mgawanyiko wa kuhuzunisha. Kwa upande mmoja, mamilioni ya watu wanasumbuliwa na njaa huku, kwa upande mwingine, kutojali sana kunadhihirika katika upotevu wa chakula. Chakula ambacho hutupwa kila mwaka hutoa gesi chafuzi, wakati usambazaji sahihi utatosha kuwalisha wale wote wanaoangaika kwa  njaa. Hizi ni nyakati za hatari. Tunasukuma ulimwengu kwa mipaka ya hatari: hali ya tabianchi inabadilika, rasilimali zinaporwa; shida na migogoro ya kiuchumi inatishia maisha ya mamilioni ya watu. Wakikabiliwa na mgogoro huo, jumuiya za vijijini ndizo za kwanza kuathirika, kwani hazina rasilimali za kukabiliana na hali inayotokana na mabadiliko ya tabianch na uhasama, na zimetengwa katika kupata fedha.

Watu Asilia ni waathirika na mateso

Watu wa kiasili pia ni waathirika wa mateso, kunyimwa na kunyanyaswa. Ingawa ujuzi wao wa usimamizi wa maliasili na uhusiano wao na mazingira unaweza kusaidia kuhifadhi bioanuwai. Kundi jingine lililotelekezwa ni wanawake, nguzo ya zaidi ya nusu ya familia zinazokumbwa na uhaba wa chakula katika maeneo ya vijijini, ambako vijana wengi pia wanakosa mafunzo, rasilimali na fursa. Vijana ndio mustakabali wa jamii zetu za vijijini na hapo ndipo kuna uwezekano mkubwa wa uvumbuzi na mabadiliko chanya. Baba Mtakatifu anasisitiza katika ujumbe huo alioulekeza kwa rais wa mfuko huo kwamba “, ukweli huu unatusukuma kukabiliana na matatizo yaliyopo, hasa njaa na umaskini, kutoridhika na mikakati ya kufikirika au ahadi zisizoweza kufikiwa, bali kukuza matumaini yanayotokana na hatua za pamoja. Tushirikiane kujenga mfumo shirikishi zaidi wa kilimo na chakula. Mipango ya utafiti na teknolojia inayolenga kukuza kilimo endelevu na rafiki wa mazingira pia itachangia hili.

Kusaidia mgawanyo sawa wa rasilimali

Baba Mtakatifu anakazia kusema kuwa pia ni muhimu kuondoa upotevu wa chakula na kusaidia mgawanyo sawa wa rasilimali. Kuwekeza tu katika usafiri na kuhifadhi kunaweza kupunguza hasara ya wakulima wadogo, ambao huzalisha theluthi moja ya chakula kinachotumiwa kila siku.” Papa kwa njia hiyo anaomba msaada wa kimungu kwa ajili yao wote, ili hekima, huruma na roho ya ushirikiano mwaminifu na huduma iongoze mijadala yao na kwamba sababu za kutengwa, umaskini na usimamizi mbaya wa rasilimali ziweze kuondolewa, pamoja na athari za migogoro ya tabianchi. Mapendekezo na vitendo vyao vioneshe maadili ya ulimwengu ya haki, mshikamano na huruma, na yaelekezwe kwa wema wa wote na kufanya kazi kwa amani na urafiki wa kijamii, na kuleta mabadiliko kwa niaba ya maendeleo fungamani ya binadamu.

Ujumbe wa Papa kwa wakuu wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo
15 February 2024, 15:18