2024.02.25 Wakati wa sala ya Malaika wa Bwana Papa ametoa wito wa kusitisha vita,ghasia na vurugu sehemu mbali mbali za dunia. 2024.02.25 Wakati wa sala ya Malaika wa Bwana Papa ametoa wito wa kusitisha vita,ghasia na vurugu sehemu mbali mbali za dunia.  (ANSA)

Papa: Vita na vurugu Ukraine,Palestina,Israeli,DRC na Nigeria!

Papa Francisko amekumbuka miaka 2 tangu kuzuka kwa vita nchini Ukraine;amekumbusha vita Palestina na Israel na vita katika sehemu nyingine za dunia;amewakumbuka watu wa Mongolia wanaoteseka kwa baridi kali na vurugu nchini DRC pamoja na utekaji nyara nchini Nigeria.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mara baada ya Tafakari na sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 25 Februari 2024, Baba Mtakatifu Francisko akiwageukia waamini waliounganika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican alisema: “Jana, Februari 24, tulikumbuka kwa uchungu ukumbusho wa  mwaka wa pili tangu kuanza kwa vita kamili nchini Ukraine. Ni wahanga wangapi, majeruhi, uharibifu, uchungu, machozi katika kipindi ambacho kinazidi kuwa kirefu sana na ambacho mwisho wake bado haujaonekana! Ni vita ambayo sio tu vinaharibu eneo hilo la Ulaya, lakini vinaibua wimbi la hofu na chuki duniani kote. Wakati nikifufua mapenzi yangu ya kina kwa watu wa Ukraine wanaoteswa na kuombea kila mtu, hasa kwa waathiriwa wengi wasio na hatia, ninasihi kwamba ubinadamu huo upatikane ambao unaturuhusu kuunda mazingira ya suluhisho la kidiplomasia katika kutafuta haki na amani ya kudumu."

Ukaribu wa Papa kwa Palestina na  Israel

Baba Mtakatifu Francisko akitazama vita vingine katika Nchi Takatifu amesema “ kaka na dada, tusisahau kuiombea Palestina, kwa ajili ya Israeli na kwa ajili ya watu wengi waliosambaratishwa na vita, na kuwasaidia kwa hakika wale wanaoteseka! Hebu tufikirie juu ya mateso mengi, tufikirie juu ya watoto waliojeruhiwa, wasio na hatia.”

Wasiwasi wa Papa kuhusu vurugu nchini Congo(DRC)

Baba Mtakatifu Francisko akiendelea na mtazamo huo wa vita vilivyosambaratika ulimwenguni, pia amegeukia Afrika na kusema kuwa “Ninafuatilia kwa wasiwasi ongezeko la ghasia katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Naungana na mwaliko wa Maaskofu kuombea amani, tukitarajia kukomeshwa kwa mapigano na kutafuta mazungumzo ya dhati na yenye kujenga.

Papa ameelezea utekaji Nyara nchini Nigeria

Bado Baba Mtakatifu ametazama nchini Nyingine ya Afrika na kusema kuwa “Utekaji nyara unaozidi kutokea nchini Nigeria unasababisha wasiwasi. Ninaelezea ukaribu wangu kwa watu wa Nigeria katika maombi, nikitumaini kwamba watafanya kazi ili kuhakikisha kuwa kuenea kwa matukio hayo kunadhibitiwa iwezekanavyo.”

Ukaribu wa Papa kwa watu wa Mongolia na baridi kali

Mawazo ya Baba takatifu Francisko aidha yamempelekea katika Bara la Asia na kwamba “ Pia niko karibu na wakazi wa Mongolia, waliokumbwa na wimbi la baridi kali, ambalo linasababisha madhara makubwa ya kibinadamu. Jambo hili lililokithiri pia ni ishara ya mabadiliko ya hali tabianchi na athari zake.” Kwa kuongezea amesema “ Mgogoro wa hali ya tabianchi  ni tatizo la kijamii la kimataifa, ambalo lina athari kubwa kwa maisha ya kaka na dada wengi, hasa wale walio katika hatari zaidi: tuombe ili tuweze kufanya maamuzi ya busara na ya ujasiri ili kuchangia katika utunzaji wa  kazi ya uumbaji.”

Salamu kwa mahujaji kutoka pande za dunia

Baba Mtakatifu hata hivyo hakukosa kutoa salamu kwa mahujaji na waamini kutoka pande za dunia waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na kuseama: “Nawasalimu ninyi waamini wa Roma na sehemu mbali mbali za dunia, kwa namna ya pekee mahujaji kutoka Jaén(Hispania), vijana wa Kiromania Wakatoliki wa Kigiriki wa Paris, Jumuiya za Neokatekumenali kutoka Poland, Romania na Italia. Nawasalimia Waseminari ya Kipapa ya Kimaeneo ya Posillipo, Sekretarieti ya Jukwaa la Kimataifa la Matendo ya Kikatoliki, Skauti wa Paliano na wanakipaimara wa Lastra Signa, Torre Maina na Gorzano. Pia ninasalimia Shirikisho la Italia la Magonjwa Adimu, Klabu ya Utamaduni ya "Reggio Ricama", wanachama wa Harakati ya  Kusitisha Vurugu na watu waliojitolea wa Chama cha N.O.E.T.A.A. Na ninawasalimu watoto wa Parokia ya Bikira Mkingwa wa Dhambi Asili Amewatakia Dominika Njema  Tafadhali wasisahau kumuombea. Mlo mwema cha mchana mwema na kwaheri ya kuonana.

Wito wa Papa kwa Ukraine,Palestina na Israeli,Congo DRC na Nigeria,na ukaribu wa Mongolia

 

25 February 2024, 12:46