2024.02.15 Papa na Uwakilishi wa Harakati  ya "La Diaconie de la Beaute" 2024.02.15 Papa na Uwakilishi wa Harakati ya "La Diaconie de la Beaute"  (Vatican Media)

Papa,wasanii:Kukutana na uzuri wa Mungu huturuhusu kuelekea jamii za kibinadamu na kidugu

Papa amekutana na ujumbe kutoka Ufaransa,Harakati ya "Diaconie de la beauté" ambapo amezungumzia juu ya uzuri kama mwaliko kwa namna tofauti ya kuwa duniani,ambao uzalisha maisha,matumaini na kiu ya furaha.Katika ukweli unaotikiswa na vita na vurugu,sanaa ni muhimu ili kuonesha thamani ya maelewano kati ya watu na asili.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 15 Februari 2024 amekutana na Ujumbe wa Harakati ya Ufaransa iitwayo:Diaconie de la beauté yaani Ushemasi wa Uzuri, ambapo Papa amekutana nao tena katika fursa ya Kongamano lao jijini Roma na furaha yake kuwa pamoja nao katika kuadhimisha miaka kumi ya tangu kuanza mpango huo wanaouandaa kila mwaka. Papa amemshukuru Monsinyo Le Gall kwa kujitolea kwake kwa harakati hiyo. Hata hivyo amependa kutafakari kwa ufupi juu ya mielekeo mitatu inayowatambulisha: kiroho, matukio na makazi.

Papa akutana na ujumbe wa Harakati ya Ushemasi wa Uzuri
Papa akutana na ujumbe wa Harakati ya Ushemasi wa Uzuri

Kipimo cha kwanza ni cha kiroho. Papa amesema “Wito wao ni kuwasaidia wasanii kuunda daraja kati ya mbingu na dunia. Wanataka kuamsha ndani yao utafutaji wa ukweli, iwe ni wanamuziki, washairi au waimbaji, wachoraji, wasanifu majengo au waelekezi, wachongaji, waigizaji au wachezaji au kitu kingine chochote. Kwa sababu uzuri hutualika kwa njia tofauti ya kuwa ulimwenguni. Ni kuhusu kutafakari. Kwa hakika, Baba Mtakatifu amesisitiza kuwa “uzuri hutufanya tuhisi kwamba maisha yanaelekezwa kuelekea utimilifu. Kwa uzuri wa kweli ndivyo tunaanza kuhisi hamu kwa ajili ya Mungu"(Hotuba kwa wasanii, 23 Juni 2023). Kumwamini Mungu kunaweza tu kuhimiza kiumbe kujishinda, kujielekeza katika maisha ya kimungu kupitia maongozi ya kisanii.

Mwelekeo wa pili -  Baba Mtakatifu amesema kuwa katika  Kifaransa  neno linaitwa ‘evenemenziale’ yaani matukio, na kwamba   chama chao cha  Ushemasi wa Uzuri huwasaidia wasanii kufanya upya mazungumzo yenye matunda na Kanisa, kupitia mikutano, maonesho, matamasha na maonesho. Ni njia ya wao kufanya ukaribu wa Kanisa kuonekana kwa wasanii kwa kuingia katika mazungumzo na utamaduni wao na maisha yao, iwe ni waamini au la.

Harakati ya Ushemasi wa Uzuri kutoka Ufaransa
Harakati ya Ushemasi wa Uzuri kutoka Ufaransa

Na mwelekeo wa tatu ni wa makazi. Baba Mtakatifu ameeleza kuwa shukrani kwa utume wao wenye kuzaa matunda, kazi yao inaongezeka kwa uundaji wa nyumba za wasanii  ulimwenguni kote. Maisha ya msanii mara nyingi huoneshwa na upweke, wakati mwingine na unyogovu na mateso makubwa ya ndani. Changamoto yao ni kuutoa uzuri uliojificha ndani yake, ili naye awe mtume wa uzuri huu unaozalisha matumaini na kiu ya furaha.

Dhamira inayochangia katika kuhamasisha hadhi ya msanii ambaye hajisikii kukataliwa, kutoeleweka, kutengwa na kubaguliwa. Kwa hiyo amewahimiza waendelee nayo. Papa Francisko kwa njia hiyo amewasihi wawe waimbaji wa maelewano kati ya watu, waimbaji wa maelewano kati ya tamaduni na dini. Ubinadamu wetu unatikiswa na jeuri ya kila aina, na vita, na migogoro ya kijamii. Katika muktadha huu, tunahitaji wanaume na wanawake wenye uwezo wa kutufanya tuwe na ndoto ya ulimwengu tofauti, ulimwengu mzuri. Wafanye watu wawe na ndoto, ili watamani maisha kwa ukamilifu!

Papa akitoa hotuba yake kwa Ujumbe wa Harakati ya 'Ushemasi wa uzurì'
Papa akitoa hotuba yake kwa Ujumbe wa Harakati ya 'Ushemasi wa uzurì'

Zaidi ya hayo, leo hii  ni uharaka kwetu kuunda upya upatano kati ya mwanadamu na mazingira. Majanga makubwa ya tabianchi yanatuhitaji kukagua tabia na tabia zetu. Na sanaa ni njia yenye nguvu sana ya kufikisha ujumbe wa uzuri wa maumbile. Kwa hakika, “kutunza ulimwengu unaotuzunguka na kututegemeza kunamaanisha kujitunza wenyewe. Lakini tunahitaji kujiunda kama “sisi” tunaoishi katika nyumba ya pamoja” (Fratelli tutti, 17).

Papa Francisko amesema kuwa “Hebu tujiulize: ni nini mchango wetu katika kujenga ulimwengu wenye maelewano? Ni swali ambalo lazima tujiulize kila mmoja wetu. Utamaduni wa uzuri daima hutufanya kusonga tena. Kukutana na uzuri wa Mungu huturuhusu kuanza tena, kwenye njia kuelekea jamii zaidi za kibinadamu na za kidugu. Papa Franciso amewashukuru tena na kutakia heri  ya Ushemasi wao. Amewabariki kutoka ndani ya moyo wake na kuwaomba wamuombee.

Hotuba ya Papa kwa Harakati ya Ushemasi wa Uzuri kutoka Ufaransa
15 February 2024, 14:55