Sadaka na Majitoleo ya Sr. Paesie Kwa Watoto Wanaoishi Katika Mazingira Magumu na Hatarishi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Kuna maswali mengi ambayo mwanadamu anajiuliza katika safari ya maisha yake hapa duniani, lakini, anashindwa kupata majibu muafaka kwani, majibu makini yanafumbatwa katika Fumbo la Mwenyezi Mungu! Mwanadamu katika unyonge wake, anaweza kuyaangalia yote haya kwa jicho la huruma, mapendo na udadisi mkubwa! Anaweza kusikiliza kilio na mahangaiko ya watu, akabaki akiwa amepigwa butwaa na kujiuliza kwanini haya yanatendeka? Mwanadamu anapoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zake, anaweza kuangua kilio na kuteseka pamoja nao, kama kielelezo cha ushuhuda wa upendo na mshikamano. Kuna sababu mbalimbali zinazopelekea watoto kujikuta wakiwa katika hali na mazingira magumu na hatarishi. Sababu kubwa ni umaskini wa hali na kipato; udhaifu wa binadamu; ukosefu wa haki msingi na hali ngumu ya maisha inayowapelekea baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara! Haya pia ni matunda ya utandawazi usiojali wala kuguswa na utu na heshima ya binadamu. Lakini, wakati mwingine, wazazi wanawapenda sana watoto wao, lakini wanashindwa kumwilisha upendo huu katika uhalisia wa maisha ya watoto wao na matokeo yake, watoto wanajenga chuki dhidi ya wazazi wao na hapo familia inakuwa ni mahali pa chungu kwa watoto wengi, kiasi cha kutafuta faraja nje ya familia zao!
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 3 Februari 2024 amepiga simu na kuzungumza mubashara na Sr. Paesie aliyekwenda nchini Haiti kama Mtawa wa Shirika la Masista wa Upendo na hivyo kufunga nadhiri zake za daima kunako mwaka 1999. Katika maisha na wito wake, alihisi kuitwa kuwahudumia watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi, jambo alilolitekeleza kunako mwaka 2017. Aliwaacha Wamisionari wa upendo na kuanzisha Familia ya Kizito, Jumuiya mpya iliyopewa jina la kumbukumbu ya shuhuda wa imani aliyesadaka maisha yake katika kipindi cha miaka kumi na nne, nchini Uganda. Tarehe 3 Juni 2018, Familia ya Kizito ilipewa kibali kutoka kwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Port au Prince nchini Haiti, Kama Shirika la Kitawa na kwamba, Jumuiya hii ilikuwa chini ya Mamlaka ya Kijimbo. Jumuiya ya Kizito inawahudumia watoto elfu mbili na mia tano kituoni kwao.
Sr. Paesie katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Vatican News anakiri kushangazwa sana alipopokea simu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko huku akimtumia ujumbe wa kumtia shime, kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi nchini Haiti. Baba Mtakatifu amemhakikishia sala na sadaka yake katika maisha na utume wake miongoni mwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Sr. Paesie anasema, amewashirikisha wanajumuiya na timu anayofanya nayo kazi, ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, jambo ambalo limeibua furaha na matumaini makubwa kwa watoto wa Haiti wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Sr. Paesie anatekeleza utume wake kati ya makundi ya wahalifu wa kitaifa na Kimataifa yanayotishia usalama wa maisha ya watu, hali inayoongeza umaskini, ujinga na maradhi. Hivi karibuni, watawa sita walitekwa nyara na baadaye kuachiliwa huru. Magenge ya wahalifu yanatafuta fedha, ndiyo maana yanateka watu matajiri, ili waweze kulipwa fidia. Takwimu zinaonesha kwamba, Haiti kuna zaidi ya watu laki tatu wasiokuwa na makazi maalum, watu wengi wanahofia usalama wa maisha na mali zao. Leo hii kuna watu wanaolala barabarani, hali ya maisha ambayo hapo awali haikuwepo, watu wanaona na kutembea na kifo machoni pao!