Papa Francisko Ujumbe Makini kwa Mapadre wa Jimbo kuu la Roma: Huduma kwa watu watakatifu wa Mungu, Uaminifu na Maongozi ya Roho Mtakatifu. Papa Francisko Ujumbe Makini kwa Mapadre wa Jimbo kuu la Roma: Huduma kwa watu watakatifu wa Mungu, Uaminifu na Maongozi ya Roho Mtakatifu.  (Vatican Media)

Ujumbe Makini Kwa Mapadre: Huduma, Uaminifu na Maongozi ya Roho Mtakatifu!

Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu matatu: Huduma ya Kipadre, kama washiriki waaminifu kwa Maaskofu katika huduma ya kwa watu wa Mungu, chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawakumbusha Mapadre kwamba, wao ni washiriki waaminifu, wanaosaidiana na Maaskofu mahalia katika huduma kwa watu wa Mungu na wala si kwa kujichukulia maamuzi, matamanio yao ya muda mrefu na wala si kwa kujikita katika historia yao wenyewe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Kristo Yesu katika maisha na utume wake wa hadhara alijitambulisha kuwa ni Mchungaji mwema, hali ambayo ilijidhihirisha katika ushuhuda wa maisha yake ya kila siku kiasi cha kusema kwamba, Yeye ndiye mchungaji mwema anayeutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Kristo Yesu ni mlango salama wa kondoo na kondoo huisikia sauti yake kwa sababu huwaita kwa majina na kuwapeleka nje kwa kuwatangulia nao humfuata nyuma. Anawajua walio wake na walio wake wanamjua fika. Rej. Yn. 10: 1-18. Wito na maisha ya Kipadre ni zawadi na sadaka kubwa inayotolewa kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni utimilifu wa wito unaowawezesha Mapadre kuwa ni Kristo mwingine kwa kutenda kama Kristo Yesu “In persona Christi.” Maisha na utume wa kipadre yanatekelezwa kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa pamoja na kuwahudumia watu kwa upendo wa Kimungu. Kwa ufupi kabisa, Mapadre wanashiriki katika huduma ya: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni mwendelezo wa kazi ya ukombozi ambayo Kristo Yesu amekuja kuitekeleza hapa duniani, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Mapadre wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili baada ya kukutana na Kristo Mfufuka.

Ushemasi ni Daraja ya Huduma kwa Watu wa Mungu
Ushemasi ni Daraja ya Huduma kwa Watu wa Mungu

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha; ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 24 Februari 2024 amekabidhi hotuba kwa Mashemasi wa Jimbo kuu la Roma, wanaotarajiwa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa mwaka 2024. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia mambo makuu matatu: Huduma ya Kipadre, kama washiriki waaminifu kwa Maaskofu katika huduma ya kwa watu wa Mungu, chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawakumbusha Mapadre kwamba, wao ni washiriki waaminifu, wanaosaidiana na Maaskofu mahalia katika huduma kwa watu wa Mungu na wala si kwa kujichukulia maamuzi, matamanio yao ya muda mrefu na wala si kwa kujikita katika historia yao wenyewe.

Ushirika unasimikwa katika udugu, uaminifu na unyenyekevu kwa Kristo Yesu
Ushirika unasimikwa katika udugu, uaminifu na unyenyekevu kwa Kristo Yesu

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakazia kwamba, Mapadre ni washiriki wenye busara wa Daraja ya Uaskofu, msaada na chombo chake, waitwao kuwatumikia watu wa Mungu wakiwa wamoja. Hili ni Fumbo la Ushirika wa watu wa Mungu na Mapadre ni mashuhuda wa kwanza wa ushirika huu unaosimikwa katika udugu, uaminifu na unyenyekevu na wala si kufanya mambo pekepeke. Hii ni changamoto ya kujikita katika majiundo endelevu, kwa kushirikiana kwa ukaribu katika urika wa Mapadre, waliowatangulia katika huduma, kwa kuwa wazi bila ya kutumbukia katika kishawishi cha kufanya mambo pekepeke, hali ambayo inaweza kumtumbukiza Padre katika vishawishi vingi zaidi. Baba Mtakatifu anasema, amependa kukutana na kuzungumza nao wangali katika Daraja ya Ushemasi kwa sababu huu ni Ushemasi wa mpito na msingi wa huduma ya Kipadre mintarafu mawazo ya Kristo Yesu anayesema, “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.” Mk 10:45. Hapa mkazo ni umuhimu wa huduma kwa watu wa Mungu na kwamba, Mapadre wawe na ujasiri na unyenyekevu wa kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kuwahudumia vyema watu wa Mungu, daima wakijiachilia mikononi mwa Mungu kadiri ya hali na mazingira pengine hata kwenda kinyume cha yale waliyojifunza wakiwa Seminarini.

Maisha na utume wa Kipadre ni Sadaka ya Ekaristi Takatifu
Maisha na utume wa Kipadre ni Sadaka ya Ekaristi Takatifu

Maisha na utume wa shughuli za kichungaji ni sadaka na majitoleo yanayopata chimbuko lake katika Fumbo la Ekaristi Takatifu linalomwilishwa katika uhalisia, vipaumbele na sadaka ya maisha ya kila siku “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu.” Huu ni mwelekeo unaosimikwa katika ukarimu, huruma na upendo, kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake, ili kuwahudumia watu wa Mungu kwa furaha na unyenyekevu. Ni furaha inayowasaidia kupiga hatua kwa uvumilivu na katika kufanya mang’amuzi. Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kutekeleza dhamana na wajibu wao chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao. Huyu ni Roho ambaye anawaimarisha katika utume wao, unaomwilishwa kila siku ya maisha wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, na wakati wa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili kukaa na kuendelea kuishi pamoja na Kristo Yesu, watu watakatifu wa Mungu pamoja na watu wote wanaokutana nao katika hija ya maisha na utume wao kama Mapadre. Na kwa jinsi hii, nyoyo zao zitaendelea kuchota furaha kutoka kwa Kristo Yesu, huku wakiwa wanajikita katika sala, mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu, ili kuhakikisha kwamba, maisha na utume wa Kipadre unaendelea kuchanua na kupaishwa kila siku.

Ujumbe kwa Mapadre
24 February 2024, 14:37