Tafuta

Baraka ya Papa ya Urbi et Orbi 2024 Baraka ya Papa ya Urbi et Orbi 2024  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa wa Siku ya 98 ya Kimisionari Duniani 2024:Enendeni njia panda

Katika ujumbe wa Siku ya 98 ijayo ya Kimisionari duniani 2024,Papa anasisitiza Yesu anaendelea kubisha mlango,lakini kutoka ndani ili tumtoe nje.Tangazo la Injili ni la dharura kwa wote,lakini lifanyike kwa fadhili bila kulazimisha au kugeuza imani.Kanisa kwa uaminifu wa utume litaendelea kwenda hadi miisho ya dunia.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika siku ambayo Mama Kanisa anafanya Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, sambamba na  Siku ya Watawa Ulimwenguni tarehe 2 Februari 2024, Baba Mtakatifu Francisko ametoa ujumbe wake wa Siku ya  98 ya Kimisionari Ulimwenguni itakayoadhimishwa tarehe 20 Oktoba 2024 ambayo inaongozwa na Kauli mbiu: “enendeni hata njia panda za barabara na wote mwaonao waiteni harusini”(rej Mt 22:9). Kwa njia hiyo ufuatano ni ujumbe wa siku ya Kimisionari ambapo Baba Mtakatifu:

Kaka na dada!

Kauli mbiu niliyochagua kwa ajili ya Siku ya Kimisionari ulimwengini  kwa  mwaka huu imechukuliwa kutoka katika mfano wa Injili wa karamu ya harusi (rej. Mt 22:1-14). Baada ya wageni kukataa mwaliko wake, mfalme, mhusika mkuu katika historia hiyo, anawaambia watumishi wake: “Basi, enendeni kwenye njia kuu, mkawaalike kwenye karamu ya harusi wote mtakaowapata” (Mt 22,9). Tukitafakari kifungu hiki muhimu katika muktadha wa mfano na maisha ya Yesu mwenyewe, tunaweza kutambua vipengele kadhaa muhimu vya uinjilishaji. Haya yanaonekana kwa wakati ufaao kwetu sote, kama wanafunzi wamisionari wa Kristo, katika hatua hii ya mwisho ya safari ya kisinodi ambayo, kwa maneno ya kauli mbiu yake, “Ushirika, Ushiriki, utume”, inalenga kulielekeza tena Kanisa katika kazi yake ya msingi ambayo ni mahubiri ya Injili katika ulimwengu wa leo.

1. “Nenda ukaalike!” Utume hauchoki kwenda kuwaalika wengine kwenye karamu ya Bwana

Katika amri ya Mfalme kwa watumishi wake tunapata maneno mawili yanayoelezea moyo wa utume: vitenzi ni “kutoka nje” na “kualika.” Kuhusu cha kwanza, tunahitaji kukumbuka kwamba watumishi walikuwa wametumwa hapo awali kupeleka mwaliko wa mfalme kwa wageni (rej Mt 22 3-4). Tunaona Utume,  ni kwenda bila kuchoka kwa wanaume na wanawake wote, ili kuwaalika kukutana na Mungu na kuingia katika ushirika naye. Bila kuchoka! Mungu, mkuu wa upendo na mwingi wa huruma mara kwa mara hupanga kukutana na wanaume na wanawake wote, na kuwaita kwenye furaha ya ufalme wake, hata katika hali ya kutojali au kukataa kwao. Yesu Kristo, Mchungaji Mwema na mjumbe wa Baba, alitoka nje kwenda kuwatafuta kondoo waliopotea wa watu wa Israeli na kutamani kwenda mbali zaidi, ili kuwafikia hata kondoo walio mbali zaidi (rej. Yh 10:16). Kabla na baada ya kufufuka kwake, aliwaambia wanafunzi wake, “Nendeni!”, hivyo kuwahusisha katika utume wake mwenyewe (rej. Lk 10:3; Mk 16:15). Kanisa, kwa upande wake, kwa uaminifu kwa utume waliopokea kutoka kwa Bwana, litaendelea kwenda hadi miisho ya dunia, na kuanza safari tena na tena, bila kuchoka wala kukata tamaa mbele ya magumu na vikwazo.

Ninachukua fursa hii kuwashukuru wale wamisionari wote ambao, kwa kuitikia wito wa Kristo, wameacha kila kitu nyuma kwenda mbali na nchi yao na kupeleka  Habari Njema mahali ambapo watu bado hawajaipokea, au kuipokea hivi karibuni tu. Wapendwa, kujitolea kwenu kwa ukarimu ni onesho dhahiri la kujitolea kwenu kwa ad gentes - watu wote  ambao Yesu aliwakabidhi wanafunzi wake: “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mt 28:19). Tunaendelea kuomba na tunamshukuru Mungu kwa miito mipya na mingi ya kimisionari kwa ajili ya kazi ya uinjilishaji hadi miisho ya dunia.

Tusisahau kwamba kila Mkristo ameitwa kushiriki katika utume huu wa ulimwengu mzima kwa kutoa ushuhuda wake mwenyewe kwa Injili katika kila muktadha, ili Kanisa zima liweze kuendelea na Bwana na Mwalimu wake kwenye “njia” za dunia ya leo hii. Tamasha la leo katika Kanisa ni kwamba Yesu anaendelea kubisha mlango, lakini kutoka ndani, ili tumtoe nje! Mara nyingi tunaishia kuwa Kanisa 'lililofungwa' ambalo halimwachii Bwana atoke nje, ambalo humweka kama 'wake', ambapo Bwana alikuja kwa ajili ya utume na anataka sisi tuwe wamisionari” ( Hotuba kwa Washiriki katika Kongamano lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la  Walei, Familia na Maisha, 18 Februari 2023). Sisi sote tuliobatizwa tuwe tayari kuanza upya kila mmoja kadiri ya hali yake ya maisha ili kuanzisha harakati jipya la kimisionari kama vile mapambazuko ya Ukristo!

Ili kurudi kwa amri ya mfalme katika mfano huo, watumishi wanaambiwa sio tu “kwenda,” lakini pia “kualika:” “Njooni arusini!” (Mt 22:4). Hapa tunaweza kuona kipengele kingine, ambacho si cha muhimu sana, cha utume uliokabidhiwa na Mungu. Kama tunavyoweza kuwazia, watumishi walipeleka mwaliko wa mfalme kwa uharaka lakini pia kwa heshima na fadhili nyingi. Vivyo hivyo, utume wa kupeleka Injili kwa kila kiumbe lazima,  uige “mtindo” uleule wa Yule anayehubiriwa. Katika kuutangazia ulimwengu “uzuri wa upendo wa wokovu wa Mungu uliodhihirishwa katika Yesu Kristo ambaye alikufa na kufufuka kutoka kwa  wafu” (Evangelii Gaudium, 36), wanafunzi wamisionari wanapaswa kufanya hivyo kwa furaha, ukuu na ukarimu ambao ni matunda ya Roho Mtakatifu ndani yao (taz. Gal 5:22). Sio kwa kushinikiza, kulazimisha au kugeuza imani, lakini kwa ukaribu, huruma na upole na kwa njia hiyo kuakisi njia ya Mungu mwenyewe ya kuwa na kutenda.

2.“Kwenye karamu ya harusi”. Mwelekeo wa eskatolojia na Ekaristi utume wa Kristo na Kanisa.

Katika mfano huo, mfalme anawaomba watumishi wapeleke mwaliko wa karamu ya harusi ya mwanawe. Karamu hiyo ni onesho la karamu ya eskatolojia. Ni taswira ya wokovu wa mwisho katika Ufalme wa Mungu, unaotimizwa hata sasa kwa kuja kwa Yesu, Masiha na Mwana wa Mungu, ambaye ametupatia uzima tele (rej. Yh 10:10), unaofananishwa na meza iliyowekwa pamoja na vyakula vitamu na divai nzuri, wakati Mungu atakapoharibu kifo milele (taz. Isa 25:6-8). Utume wa Kristo unahusiana na utimilifu wa wakati, kama alivyotangaza mwanzoni mwa mahubiri yake: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia” (Mk 1:15). Wanafunzi wa Kristo wameitwa kuendeleza utume huu wa Bwana na Mwalimu wao. Hapa tunafikiria fundisho la Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican juu ya tabia ya kieskatologia ya uenezaji wa kimisionari wa Kanisa: “Wakati wa utendaji wa kimisionari unaendelea kati ya ujio wa kwanza wa Bwana na ule wa pili…, kwa maana Injili lazima ihubiriwe kwa mataifa yote kabla ya  Bwana kurudi (taz. Mk 13:10)” (Ad Gentes, 9).

Tunajua kwamba miongoni mwa Wakristo wa kwanza ari ya kimisionari ilikuwa na mwelekeo wenye nguvu wa kieskatologia. Waliona uharaka wa kuhubiriwa kwa Injili. Leo hii  pia ni muhimu kudumisha mtazamo huo, kwa kuwa hutusaidia kueneza Injili kwa shangwe ya wale wanaojua kwamba “Bwana yu karibu” na kwa tumaini la wale wanaokaza mwendo kuelekea lengo, wakati ambapo sisi sote tutakuwa pamoja na Kristo kwenye karamu yake ya harusi katika ufalme wa Mungu. Wakati ulimwengu unaweka mbele yetu “karamu” mbalimbali za ulaji, faraja ya ubinafsi, mkusanyiko wa mali na ubinafsi, Injili inamwita kila mtu kwenye karamu ya kimungu, yenye ishara ya furaha, ushirikiano, haki na udugu katika ushirika na Mungu na wengine. Utimilifu huu wa maisha, ambao ni zawadi ya Kristo, unatarajiwa hata sasa katika karamu ya Ekaristi, ambayo Kanisa huadhimisha kwa amri ya Bwana kwa kumbukumbu yake. Mwaliko wa karamu ya eskatolojia tunayoleta kwa kila mtu katika utume wetu wa uinjilishaji unahusishwa kwa kiasi kikubwa na mwaliko wa meza ya Ekaristi, ambapo Bwana hutulisha kwa Neno lake na kwa Mwili na Damu yake.

Kama Benedikto wa kumi na sita alivyofundisha: “Kila adhimisho la Ekaristi hutimiza kisakramenti mkusanyiko wa eskatolojia kwa Watu wa Mungu. Kwetu sisi, karamu ya Ekaristi ni kionjo halisi cha karamu ya mwisho iliyotabiriwa na manabii (rej. Isa 25:6-9) na kuelezewa na Agano Jipya kama 'karamu ya harusi ya Mwana-Kondoo' (Uf 19:9)., kuadhimishwa kwa furaha ya ushirika wa watakatifu” (Sacramentum Caritatis, 31). Kwa hiyo, sisi sote tunaitwa kushuhudia kwa uzito  zaidi kila Ekaristi, katika vipimo vyake vyote, na hasa vipimo vyake vya eskatolojia na kimisionari. Katika suala hili, ningesisitiza tena kwamba “hatuwezi kukaribia meza ya Ekaristi bila kuvutwa katika utume ambao, kuanzia katika moyo wa Mungu,unakusudiwa kuwafikia watu wote” (Sacramentum Caritatis,  84).

Upyaisho wa Ekaristi Takatifu ambao Makanisa mengi mahalia  yanautangaza kwa kusifiwa katika enzi ya baada ya Uviko -19 pia itakuwa muhimu kwa kufufua roho ya kimisionari katika kila mshiriki wa waamini. Kwa imani na shauku kubwa kiasi gani tunapaswa kuriri katika kila Misa: “Tunatangaza kifo chako, ee Bwana, na kutukuza kufufuka wako, mpaka utakapokuja tena”! Katika mwaka huu wa maombi kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya 2025, ninapenda kuwahimiza wote wazidishe kujitolea kwao zaidi ya yote kushiriki katika adhimisho la Misa na kuombea utume wa Kanisa wa Uinjilishaji. Kwa kutii amri ya Mwokozi, kutoacha kusali, katika kila adhimisho la Ekaristi na liturujia, “Baba Yetu” pamoja na ombi lake, “Ufalme wako ufike”. Kwa njia hiyo, sala ya kila siku na Ekaristi hasa inatufanya kuwa mahujaji na wamisionari wa matumaini, tukisafiri kuelekea uzima wa milele ndani ya Mungu, kuelekea karamu ya harusi ambayo Mungu amewaandalia watoto wake wote.

3. “Kwa wote”. Utume wa kiulimwengu wa wanafunzi wa Kristo katika Sinodi kamili na Kanisa la kimisionari

Tafakari ya tatu na ya mwisho inahusu wapokeaji wa mwaliko wa Mfalme: “kila mtu.” Kama nilivyosisitiza, “Huu ndio moyo wa utume: hiyo  ya ‘wote’, bila kutenganisha yeyote. Basi, kila utume wetu unazaliwa kutoka katika moyo wa Kristo ili aweze kuwavuta wote kwake” (Hotuba kwa Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, 3 Juni 2023). Leo, katika ulimwengu uliosambaratishwa na migawanyiko na migogoro, Injili ya Kristo inabakia kuwa sauti ya upole lakini thabiti inayowaita watu binafsi kukutana, kutambua kwamba wao ni kaka na dada, na kushangilia katika upatanisho katikati ya tofauti. “Mungu Mwokozi wetu hutaka kila mtu aokolewe na kupata kujua yaliyo kweli” (1 Tim 2:4). Basi, tusisahau kamwe kwamba katika utendaji wetu wa umisionari tunaombwa kuhubiri Injili kwa wote: “Badala ya kuonekana kuwa tunaweka wajibu mpya, [sisi] tunapaswa kuonekana kama watu wanaotaka kushiriki furaha yao, wanaoelekeza kwenye upeo wa matazamo wa uzuri na wanaowaalika wengine kwenye karamu ya kupendeza”(Evangelii Gaudium, 14).

Wanafunzi Wamisionari wa Kristo sikuzote wamekuwa na hangaiko la kutoka moyoni kwa watu wote, haidhuru hali yao ya kijamii au hata kiadili. Mfano wa karamu unatuambia kwamba, kwa amri ya mfalme, watumishi walikusanya “wote waliowaona, wema na wabaya” (Mt 22: 10). Zaidi ya hayo, “maskini, vilema, vipofu na viwete ( Lk 14:21 ), kwa neno moja, kaka na dada zetu walio wadogo kabisa, waliotengwa na jamii, ni wageni wa pekee wa mfalme. Karamu ya harusi ya Mwanae ambayo Mungu ametayarisha inabaki wazi sikuzote kwa wote, kwa kuwa upendo wake kwa kila mmoja wetu ni mkubwa na hauna masharti. “Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yh 3:16). Kila mtu, kila mwanamume na kila mwanamke, anaalikwa na Mungu kushiriki neema yake, ambayo inabadilisha na kuokoa. Mtu anahitaji tu kusema “ndiyo” kwa zawadi hii ya kimungu isiyo na malipo, akiikubali na kujiruhusu kubadilishwa nayo, na kuivaa kama “joho la harusi” (taz. Mt 22:12).

Dhamira kwa wote inahitaji kujitolea kwa wote. Tunahitaji kuendelea na safari yetu kuelekea Kanisa la kisinodi na kimisionari kikamilifu katika huduma ya Injili. Sinodi kimsingi ni ya kimisionari na, kinyume chake, utume daima ni sinodi. Kwa hiyo, ushirikiano wa karibu wa kimisionari leo hii ni wa haraka na wa lazima zaidi, katika Kanisa la ulimwengu wote na katika Makanisa mahalia. Katika nyayo za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Watangulizi wangu, ninapendekeza kwa majimbo yote duniani huduma ya Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari.Yanawakilisha njia za msingi “ambazo Wakatoliki wanajazwa kutoka utotoni na mtazamo wa kweli wa ulimwengu mzima na wa kimisionari na pia njia ya kuanzisha ukusanyaji mzuri wa fedha kwa ajili ya utume wote, kila mmoja kulingana na mahitaji yake” (Ad Gentes, 38). Kwa sababu hiyo, makusanyo ya sadaka ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni katika Makanisa yote mahalia yamekusudiwa kwa ukamilifu kwa mfuko wa mshikamano wa ulimwengu wote ambao Shirika la Kipapa la Uenezaji wa Imani kisha husambaza kwa niaba ya Papa kwa ajili ya mahitaji ya utume wote katika Makanisa yote. Tuombe kwamba Bwana atuongoze na atusaidie kuwa Kanisa la Kisinodi na la kimisionari zaidi (taz. Mahubiri kwa ajili ya Misa ya Kuhitimisha Mkutano Mkuu wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu, tarehe 29 Oktoba 2023).

Hatimaye, na tuinue mtazamo wote  kwa Maria, ambaye alimwomba Yesu afanye muujiza wake wa kwanza kwa usahihi kwenye karamu ya harusi, huko Kana ya Galilaya (taz. Yn 2:1-12). Bwana aliwapatia wale bwana na bibi harusi na wageni wote divai mpya, kama kielelezo cha karamu ya harusi ambayo Mungu anatayarisha kwa ajili ya wote katika mwisho wa wakati. Na tuombe maombezi yake ya kimama kwa ajili ya utume wa kueneza Injili ya wanafunzi wa Kristo katika wakati wetu. Kwa furaha na mahangaiko ya upendo ya Mama yetu, kwa nguvu iliyozaliwa na huruma na mapenzi (rej. Evangelii Gaudium, 288), twende mbele kuwapelekea kila mtu mwaliko wa Mfalme, Mwokozi wetu. Maria Mtakatifu, Nyota ya Uinjilishaji, utuombee!

Ujumbe ulitiwa saini na Papa Francisko katika Kanisa la Mtakatifu Yohane wa Laterano tarehe 25 Januari 2024, katika Siku kuu ya Uongofu wa Mtakatifu Paulo.

Ujumbe wa Papa wa Siku ya 98 ya Kimisionari ulimwenguni 2024
02 February 2024, 11:55