Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 10 Februari 2024 amekutana na kuzungumza na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 10 Februari 2024 amekutana na kuzungumza na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Vyombo vya Ulinzi na Usalama Mjini Vatican Vyapongezwa Kwa Umahiri, Weledi na Huruma

Hii ni dhamana inayojumuisha: Ulinzi na usalama; umakini wa hali ya juu ili kudhibiti hali na matukio yasiyotarajiwa; utendaji unaohitaji hekima na busara; nguvu, umakini na uelewa. Huduma kwa wale wanaoomba msaada bila kusahau changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa dhamana na wajibu huu nyeti. Utekelezaji wa majukumu haya mazito unajikita katika sifa kuu mbili yaani maadili na sadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amevishukuru na kuvipongeza vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotekeleza dhamana na wajibu wake msingi kwa kuzingatia: Uaminifu, uvumilivu, weledi na dhamana kwa maisha ya watu na mali zao mjini Vatican, bila kuwasahau viongozi wa maisha ya kiroho, wanaowasindikiza kila siku katika shughuli na maisha yao ya Kikristo. Anatambua na kuthamini uwepo wao wakati wa anapokutana na mahujaji pamoja na wageni wanaomtembelea Khalifa wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, wale wanaofanya hija kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro na waandamizi wake waliolala usingizi wa amani kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican; wakati wa Ibada na mikutano mbalimbali bila kusahau hija zake za kichungaji ndani na nje ya Italia.

Papa Francisko akisalimiana na vikosi vya ulinzi na usalama Vatican
Papa Francisko akisalimiana na vikosi vya ulinzi na usalama Vatican

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 10 Februari 2024 amekutana na kuzungumza na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Ametumia muda huu kuwapongeza kwa kujisadaka mchana na usiku kutekeleza dhamana hii nyeti na yenye athari nyingi katika maisha ya watu. Hii ni dhamana inayojumuisha: Ulinzi na usalama; umakini wa hali ya juu ili kudhibiti hali na matukio yasiyotarajiwa; utendaji unaohitaji hekima na busara; nguvu, umakini na uelewa. Huduma kwa wale wanaoomba msaada bila kusahau changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa dhamana na wajibu huu. Mtakatifu Yohane XXIII aliwahi kusema kwamba, utekelezaji wa sheria ni kazi nzito, inayohitaji sifa kuu za kimaadili na zaidi ya yote ni kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ulinzi na usalama unahitaji nidhamu, maadili, sadaka na majitoleo
Ulinzi na usalama unahitaji nidhamu, maadili, sadaka na majitoleo

Mtakatifu Yohane wa XXIII alikuwa akifafanua umuhimu wa kuwa na watumishi wazuri na waaminifu kwa ajili ya Jumuiya ya kibinadamu, vyombo na mashuhuda wa amani katika jamii. Haya ni maneno yenye maana nzito yanayokidhi matarajio yote mawili na wakati mwingine yanadai sana kiasi cha kuumiza sanjari na changamoto za kimaadili. Sifa njema na ujenzi wa amani jamii ni mambo yanayostawishwa hatua kwa hatua na wala hayawezi kuja mara moja tu! Binadamu katika asili yake anayo nuru na vivuli vilivyowekewa mipaka na kujeruhiwa na dhambi. Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na watu ambao wako tayari kusimama kidete, kuingilia kati na kufanya maamuzi magumu ya kuwalinda waathiriwa, kuwatia hatiani wakosaji, lakini daima wakiongozwa kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, wema wa kila mtu.  

Wema wa kila mtu ni kauli mbi ya vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican.
Wema wa kila mtu ni kauli mbi ya vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican.

Kumbe, hii ni dhamana inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kuwa na uhakika wa taarifa, uelewa makini pamoja na huruma. Hii ndiyo maana watu wana waamini sana askari wanapokuwa wamevalia mavazi yao. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwashukuru askari wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican pamoja na familia zao kwa kazi nzuri wanayoifanya na mwishowe, amewaaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu, mlinzi na mwombezi wao!

Ulinzi na Usalama
14 February 2024, 14:38