Chuo Cha Kipapa Cha Lithuania cha Mt. Casmir Kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 75 ya Uwepo Wake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Chuo cha Kipapa cha Lithuania cha Mtakatifu Casmir kilichoko mjini Roma, kilianzishwa kunako mwaka 1944 baada ya uvamizi wa Urusi uliopelekea machafuko ya hali ya hewa kisiasa na kikanisa na hivyo kusababisha vurugu, watu wengi kukamatwa na kufungwa gerezani; wengine wakakimbilia uhamishoni ili kusalimisha maisha yao. Makleri wakanyanyaswa sana na kutezwa utu, heshima na haki zao msingi. Maaskofu ili kuokoa imani ya Kanisa Katoliki waliwatuma baadhi ya majandokasisi kumalizia masomo yao nchini Ujerumani. Na baada ya Mwaka mmoja, Vatican ilisaidia mchakato wa kuanzisha Seminari ya watu wa Mungu kutoa Lithuania kama sehemu ya malezi na majiundo ya Kipadre na huo ukawa ni mwanzo wa kuanzishwa kwa Chuo cha Kipapa cha Lithuania cha Mtakatifu Casmir kilichoko mjini Roma, takribani miaka 75 iliyopita, chini ya usimamizi wa Monsinyo Ladislao Tulaba (1912 – 16 Juni 2002.)
Kimsingi, Chuo Cha Kipapa cha Lithuania cha Mtakatifu Casmir kilichoko mjini Roma, kama kilivyo kwa sasa kilifunguliwa rasmi mwezi Mei 1948. Takwimu zinaonesha kwamba, tangu mwaka 1948 hadi mwaka 2024, kuna zaidi ya Mapadre 170 ambao wamepata malezi na majiundo yao Chuoni hapo na kati yao ni Kardinali Audrys J. Backis. Baada ya masomo na majiundo yao ya Kipadre, Majandokasisi walirejea wote kuendelea na huduma nchini mwao. Chuo hiki kimekuwa ni mahali pa majiundo ya: Kiakili, Kiroho, Kiutu, Kichungaji na Kitamaduni. Chuo pamoja na mambo mengine kinapania kuendelea kuwa ni kitovu cha malezi na majiundo kwa watu wa Mungu kutoka Lithuania.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Kipapa cha Lithuania cha Mtakatifu Casmir kilichoko mjini Roma, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake Jumatano tarehe 6 Machi 2024, ameungana na walezi na wanafunzi waliopitia Chuoni hapo, kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maadhimisho ya Jubilei hii. Baba Mtakatifu amewataka wanafunzi hawa kujenga maisha na wito wao kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni mashuhuda na watangazaji wenye furaha wa Habari Njema ya Wokovu. Mwishoni mwa Katekesi yake amewataka vijana, wazee na wanandoa wapya kuendelea na maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa njia ya sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, linalomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ametoa mwito kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Ukraine na Nchi Takatifu, kwani kuna idadi kubwa ya watu wanaoteseka kutokana na vita. Bila kuwasahau watu wote wanaoteseka na kuathirika kwa vita hii.