Sinodi ya Maaskofu. Sinodi ya Maaskofu.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko anaonesha mada kumi za Vikundi vya Mafunzo ya Sinodi

Papa Francisko ametuma barua kwa Kardinali Mario Grech,Katibu Mkuu wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi na kueleza mambo kumi ya majadiliano ambayo Vikundi vya Utafiti vitachunguza kabla ya kikao cha pili cha Sinodi kinachotarajiwa mwezi Oktoba 2024.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kwa kuzingatia Ripoti ya Muhtasari, iliyoidhinishwa katika hitimisho la Kikao cha Kwanza cha Mkutano Mkuu wa XVI wa Kawaida wa Sinodi, mnamo tarehe 28 Oktoba 2023, Baba Mtakatifu Francisko  ameonesha mada kumi ambazo Makundi ya Utafiti wa Sinodi yatazingatia kabla ya mijadala ya Sinodi mwezi Oktoba 2024. Baba Mtakatifu kwa njia hiyo ameorodhesha mada hizo za majadiliano katika barua aliyomwandikia Kardinali Mario Grech, Katibu Mkuu wa Sekretarieti kuu ya Sinodi iliyochapishwa  Alhamisi tarehe 14 Machi 2024.

Wakati huo huo, Katika Ofisi ya Vyombo vya Habari mjini Vatican kulifanyika mkutano na waandishi wa habari ili kuelezea nyaraka mbili mpya kutoka Sekretarieti Kuu ya Sinodi. Waraka wa kwanza unaitwa: “Jinsi gani ya kuwa Kanisa la Sinodi katika utume? Mitazamo mitano ya kina ya kitaalimungu katika mtazamo wa Kikao cha Pili,” wakati huo huo wa  pili ni “Makundi ya mafunzo juu ya maswali yaliyotokea katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano Mkuu wa XVI wa Kawaida wa Baraza la Wawakilishi wa Sinodi ya Maaskofu ili kuimarisha kwa ushirikiano na Mabaraza ya Kipapa ya Curia Romana.

Barua ya Papa kwa Kardinali Grech

Katika barua kwa Kardinali Grech, Papa amesema kuwa "Ripoti ya Muhtasari inaorodhesha masuala mengi muhimu ya kitaalimungu, ambayo yote ni kwa viwango tofauti vinavyohusiana na upyashaji wa sinodi ya Kanisa na sio bila athari za kisheria na kichungaji. Masuala haya, kwa asili yake, yanahitaji uchunguzi wa kina.” Kwa vile haitawezekana kufanya utafiti huu katika wakati wa Kikao cha Pili, kitakachofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 27 Oktoba 2024," Papa amebainisha kuwa “Ninapanga wagawiwe kwa Vikundi maalum vya Mafunzo ili vichunguzwe ipasavyo. Hii, itakuwa mojawapo ya matunda ya mchakato wa Sinodi uliozinduliwa tarehe 9 Oktoba 2021.” Baba Mtakatifu pia katika barua hiyo alikumbuka kwamba mashauriano haya yatafanywa kwa roho ya  Barua ya Mkono wake iliyochapishwa mnamo tarehe 16 Februari 2024 ambapo alithibitisha  kwamba: “Mabaraza ya Kipapa ya Curia Romana yatashirikiana, kulingana na uwezo wao maalum, katika kazi ya Sekretarieti Kuu ya Sinodi' kwa kuanzisha Vikundi vya Mafunzo ambavyo vitaanzisha, kwa njia ya sinodi, utafiti wa kina wa baadhi ya mada zilizojitokeza katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano Mkuu wa XVI wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu.”

Vikundi vilivyokabidhiwa mafunzo

Sekretarieti Kuu ya Sinodi, kwa makubaliano na Mabaraza ya Kipapa  yanayofaa ya Curia Romana, Papa  alibainisha kuwa imekabidhiwa kuunda Vikundi hivyo vya Mafunzo. “Pia wanapaswa kufanya hivyo kwa njia, ambayo inawaalika Wachungaji na Wataalam kutoka Mabara yote kuwa sehemu yao na kuzingatia sio tu mafundisho ambayo tayari yapo, lakini pia uzoefu muhimu zaidi unaofanyika katika Watu wa Mungu walikusanyika katika Makanisa ya mahalia. Ni muhimu kwamba Vikundi vya Mafunzo vilivyotajwa, vifanye kazi kulingana na njia halisi ya sinodi,Papa alibainisha huku akiomba kwamba Kadinali Grech awe msimamizi. Haya yote yatawezesha Kikao cha Pili, kuzingatia kwa urahisi zaidi mada kuu aliyoikabidhi kwa wakati huo, na ambayo sasa inaweza kufupishwa katika swali  hili:

'Jinsi gani ya kuwa Kanisa la sinodi katika utume?'

Papa amebainisha kuwa Vikundi vya Utafiti vitatoa ripoti ya awali ya shughuli zao katika Kikao cha Pili na watalenga, ikiwezekana, kuhitimisha mamlaka yao ifikapo Juni 2025. Baada ya kuzingatia mambo yote ipasavyo, Papa Francisko ameandika kuwa: “Ninaelekeza kwamba Vikundi vinavyohusika kushughulikia mada zilizoorodheshwa hapa chini katika muundo wa muhtasari, kwa kuzingatia yaliyomo katika Ripoti ya Muhtasari.”

Mada kumi, ambazo Papa amezifafanua ni hizi:

1. Baadhi ya vipengele vya uhusiano kati ya Makanisa Katoliki ya Mashariki na Kanisa la Kilatini (kifungu 6)

2. Kusikiliza Kilio cha Maskini (kifungu 4 na 16)

3. Dhamira katika mazingira ya kidijitali (kifungu 17)

4. Marekebisho ya Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis katika mtazamo wa sinodi ya kimisionari (kifungu 11)

5. Baadhi ya masuala ya kitaalimungu na kisheria kuhusu aina maalum za huduma (kifungu 8 na 9)

6. Marekebisho, katika mtazamo wa kimisionari wa sinodi, ya hati zinazogusa uhusiano kati ya Maaskofu, maisha ya kuwekwa wakfu, na vyama vya kikanisa (kifungu 10)

7. Baadhi ya vipengele vya mtu na huduma ya Askofu (vigezo vya kuchagua wagombea wa Uaskofu, kazi ya mahakama ya Maaskofu, asili na ziara za Kitume ( ad limina Apostolorum) kutoka katika mtazamo wa sinodi ya kimisionari (kifungu 12 na 13)

8. Wajibu wa Wawakilishi wa Papa katika mtazamo wa sinodi ya kimisionari (Kifungu 13)

9. Vigezo vya kitaalimungu na mbinu za sinodi za utambuzi wa pamoja wa masuala yenye utata ya mafundisho, kichungaji na maadili (kifungu 15)

10. Mapokezi ya matunda ya safari ya kiekumene katika mazoea ya kikanisa (kifungu 7)

Papa Francisko alisisitiza tena, "Sekretarieti kuu ya Sinodi, ina kazi ya kupanga, muhtasari wa kazi ya kubainisha mamlaka ya jina, kwa nuru ya maelekezo yangu.” Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha kwa kumshukuru Kardinali Grech kwa kazi iliyokamilika hadi sasa na kuwahakikishia wale wote wanaoshirikiana kwa ukarimu katika safari hii inayoendelea kwa baraka na usindikizaji wake.

Maandalizi ya Sinodi Oktoba 2024: mambo 10 ya kuzingatia
14 March 2024, 16:13