Tafuta

Kardinali Paul Josef Cordes amefariki dunia tarehe 15 Machi 2024 akiwa na umri wa miaka 89 ya kuzaliwa. Kardinali Paul Josef Cordes amefariki dunia tarehe 15 Machi 2024 akiwa na umri wa miaka 89 ya kuzaliwa.   (ANSA)

Kardinali Paul Josef Cordes 5 Septemba 1934 - 15 Machi 2024: Waamini Walei

Jumatatu tarehe 18 Machi 2024, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kumkumbuka na kumsindikiza Hayati Kardinali Paul Josef Cordes kwenye usingizi wa milele. Ibada hii imehudhuriwa na Makardinali 27 na kati yao ni Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Kardinali Cordes ni kati ya waasisi wa Siku ya Vijana Ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Kardinali Paul Josef Cordes amefariki dunia tarehe 15 Machi 2024 akiwa na umri wa miaka 89 ya kuzaliwa. Kardinali Paul Josef Cordes alikuwa ni Rais Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Cor Unum lililokuwa linajishughulisha na misaada ya Kanisa Katoliki. Jumatatu tarehe 18 Machi 2024, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kumkumbuka na kumsindikiza Hayati Kardinali Paul Josef Cordes kwenye usingizi wa milele. Ibada hii imehudhuriwa na Makardinali 27 na kati yao ni Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Alikuwepo pia Padre Markus Bentz, Paroko wa Parokia ya Kirchhundem, mahali ambapo Kardinali Paul Josef Cordes amezikwa. Mara baada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani “Ultima Commendatio & Valedictio.” Mama Kanisa amemkumbuka na kumwombea Hayati Kardinali Paul Josef Cordes ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na rehema aweze kumsafisha na kumtakasa na mapungufu yake ya kibinadamu ili hatimaye, aweze kupokelewa kwenye furaha na maisha ya uzima wa milele huko mbinguni. Kwa muda mrefu Hayati Kardinali Paul Josef Cordes amekuwa akisumbuliwa na maradhi pamoja na umri wake kuwa mkubwa. Alipokea hali hii kwa moyo wa amani na utulivu wa ndani, akiwa na tumaini la furaha ya maisha na uzima wa milele. “Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa.” Hek 3:1. Kwa sasa roho ya Kardinali Paul Josef Corded iko mikononi mwa Mungu, ili kufurahia upendo wake usiokuwa na mwisho.

Hayati Kardinali Paul Josef Cordes Muasisi wa Siku ya Vijana Ulimwenguni
Hayati Kardinali Paul Josef Cordes Muasisi wa Siku ya Vijana Ulimwenguni

Hayati Kardinali Paul Josef Cordes katika ujana wake, alitamani sana kuwa daktari wa binadamu, lakini mpango huu, ulifutika na hatimaye, akajiunga na Seminari kuu ya Paderborn na kwamba, hizi ni juhudi za Sr. Candida di Olpe, mtawa wa Shirika la Wafranciskani wa ndani, aliyesali sana, ili Kardinali Paul Josef Cordes, siku moja aweze kuwa ni Padre, Sr. Candida di Olpe, alikuja kumwelezea Kardinali Paul Josef Cordes mpango huu, miaka michache baada ya kupewa Daraja Takatifu ya Upadre kunako mwaka 1961. Mwaka 1971 akajipatia Shahada ya Uzamivu katika Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Magonza, Ujerumani, na baadaye akateuliwa kuwa ni Katibu mtendaji Tume ya Shughuli za Kichungaji ya Baraza la Maaskofu Ujerumani. Mwaka 1975 Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Paderborn na kuchagua kauli mbiu yake ya Kiaskofu isemayo “Deus fidelis” yaani “Mungu ni Mwaminifu.”

Kardinali Paul Josef Cordes Mtumishi Mwaminifu wa Kanisa.
Kardinali Paul Josef Cordes Mtumishi Mwaminifu wa Kanisa.

Hii kauli mbiu ndiyo iliyoongoza maisha na utume wake akawa kweli ni mwaminifu kwa Mungu, Kanisa na kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwaka 1980 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Rais Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei akajitoa na kujisadaka kwa ajili ya utume kwa vijana wa kizazi kipya, ustawi na maendeleo ya waamini walei. Huyu ndiye muasisi wa Kituo cha Vijana cha Mtakatifu Lorenzo, kilichoko mjini Vatican, ili kuwasaidia mahujaji vijana waliokuwa wanapitia mjini Roma. Ndiye aliyeratibu mkutano wa vijana Kimataifa ulioadhimishwa kunako mwaka 1984. Kuanzia tarehe 2 Desemba 1995 hadi mwaka 2010 alikuwa ni Rais wa Baraza la Kipapa la Misaada ya Kanisa Katoliki, akaonesha kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha upatanisho kwa watu wa Mungu waliokuwa wamekumbwa na maafa au majganga asilia. Ni kiongozi aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa kweli za Kiinjili; Upendo kwa Mungu na Jirani na kwamba, upendo wa Mungu kwa waja wake daima unawaambata. Katika wosia wake, aliomba msamaha kwa Mungu na kwa wale aliowaokosea. Alipenda kukita maisha yake katika imani na sasa anapumzika mbele ya Mungu milele yote.

Kardinali Cordes

 

19 March 2024, 15:03