Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266. Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266.  (Vatican Media)

Kumbukizi ya Miaka 11 ya Maisha na Utume wa Papa Francisko Kama Khalifa wa Mt. Petro

Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo ni: Maskini, Amani, Mazingira na Udugu unaofumbatwa katika diplomasia ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo ni: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika diplomasia ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni maskini wa hali na mali; wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka kumi na moja tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe na kuanza kuliongoza rasmi Kanisa Katoliki, yaani tarehe 19 Machi 2024, Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa niaba yake mwenyewe na watu wa Mungu nchini Italia, amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa matashi mema, sanjari na kumshukuru kwa kutumia vyema Mamlaka matakatifu ya ufundishaji katika Kanisa “Magisterium” kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, ili kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika kipindi cha mwaka 2023-2024, Baba Mtakatifu ametoa wito wa kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, wakimbizi na wahamiaji, waathirika wa vita na majanga asilia, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani pamoja na kupunguza pengo la uchumi lililopo kati ya watu wa Mataifa.

Kumbukumbu ya Miaka 95 ya Mktaba wa Lateran- 2024
Kumbukumbu ya Miaka 95 ya Mktaba wa Lateran- 2024

Mafundisho yake yamekuwa ni changamoto kubwa kwa wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutafuta suluhu za kiuchumi, kijamii, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Akili Mnemba, “Artificial Intelligence”, sanjari na ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi vikipewa kipaumbele cha kwanza. Rais Sergio Mattarella wa Italia amegusia pia kumbukizi ya Maadhimisho ya Miaka 95 ya “Patti Lateranensi” yaani “Mkataba wa Lateran.” Itakumbukwa kwamba, Vatican ni kati ya nchi ndogo kabisa duniani, tarehe 11 Februari, 2024 imeadhimisha miaka 95 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana saini Mkataba na Serikali ya Italia “Inter Sanctam Sedem e Italiae Regnum Conventiones” kwa kifupi “Patti Lateranensi” yaani “Mkataba wa Lateran” unaoratibiwa na kusimamiwa na Sheria za Kimataifa na hivyo kuhitimisha kile kilichojulikana “Masuala ya Roma, Questione Roman.” Hii ni Italia iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha shughuli za Kanisa na Serikali ya Italia.

Ujumbe wa Rais Sergio Mattarella kwa Papa 2024
Ujumbe wa Rais Sergio Mattarella kwa Papa 2024

Kardinali Pietro Gasparri, Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati huo kwa niaba ya Kanisa pamoja na Bwana Benito Mussolini, Waziri Mkuu wa Italia kwa niaba ya Serikali ya Italia, walitiliana saini Mkataba wa Lateran maarufu kama “Patti Lateranensi.” Mkataba huu ulikuwa na sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuhitimisha kinzani na mpasuko uliokuwa umejitokeza baada ya Serikali ya Italia kuvamia mji wa Roma kunako mwaka 1870. Mkataba huu ulitoa uhuru kwa Kanisa Katoliki nchini Italia kuweza kujiamria mambo yake bila kuingiliwa na Serikali. Huu ni msingi wa uhuru wa kuabudu. Vatican ikapewa mamlaka kamili ya kujisimamia yenyewe katika shughuli zake na Serikali ya Italia, tangu wakati huo ikatambua uhuru na mamlaka ya mji wa Vatican hata katika udogo wake. Mkataba huu, uliiwezesha Vatican “Kiti Kitakatifu-Holy See” kuwa na uhuru kamili kuhusiana na masuala ya dini na imani.

Kumbukizi ya Miaka 95 ya Mkataba wa Lateran, 2024
Kumbukizi ya Miaka 95 ya Mkataba wa Lateran, 2024

Itakumbukwa kwamba, Mkataba wa Lateran, ulifanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984 wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuendana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizokuwa zimeibuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican. Ushirikiano kati ya Serikali ya Italia na Vatican unalenga kulinda, kudumisha na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni mkataba unaojipambanua kwa kukazia uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Nchi ya Vatican inapaswa kuendelea kuwepo, ikiwa huru katika kujiamria mambo yake yenyewe, ili kutekeleza utume wake katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili ulimwenguni kote. Mifumo ya kisiasa na sera mbalimbali zinazogusa utu, heshima na maisha ya mwanadamu na hata wakati mwingine kuzama katika undani wake. Vatican imekuwa mstari wa mbele kukemea uhuru usiokuwa na mipaka wala uwajibikaji; imekazia majadiliano katika ukweli na uwazi na mshikamano wa kidugu. Vatican ni kati ya nchi ambazo ziko mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu, kama mtu mmoja mmoja au taifa. Zote hizi ni kati ya sababu ambazo zinahalalisha uwepo wa Nchi ya Vatican ili iweze kutekeleza majukumu yake katika misingi ya ukweli, haki na uwazi. Kumbe, mwaka 2024 ni kumbukizi ya miaka 40 tangu Mkataba wa Lateran, ulipofanyiwa marekebisho ya msingi kunako mwaka 1984. Rais Sergio Mattarella wa Italia anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa hija za kitume ambazo amezifanya na anatarajia kuzifanya katika kipindi cha mwaka 2024 yaani kutembea: Venezia, Verona na Trieste.

Papa Miaka 11 ya Utume
19 March 2024, 15:22