Miaka 700 tangu alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu, Miaka 750 tangu alipofariki dunia na kumbukumbu yake imeadhimishwa tarehe 7 Machi 2024 Miaka 700 tangu alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu, Miaka 750 tangu alipofariki dunia na kumbukumbu yake imeadhimishwa tarehe 7 Machi 2024  

Kumbukizi ya Miaka 750 Tangu Alipofariki Mt. Thoma wa Akwino: Utakatifu wa Maisha

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anapenda kuyakumbuka matukio makuu matatu katika maisha na utume wa Mtakatifu Thoma wa Akwino: Miaka 700 tangu alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu, Miaka 750 tangu alipofariki dunia na kumbukumbu yake imeadhimishwa tarehe 7 Machi 2024 sanjari na miaka 800 tangu alipozaliwa, tukio ambalo litaadhimishwa kunako mwaka 2025. Ontolojia ya Kijamii ya Mt. Thoma wa Akwino Mintarafu Neno la Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mtakatifu Thoma wa Akwino, “St. Thomas Aquinas, San Tommaso d’Aquino,” anayejulikana kama “Doctor Angelicus; “Angelic Doctor” alizaliwa kunako mwaka 1225 huko Roccasecca, karibu na mji wa Aquino. Akafariki dunia 7 Machi 1274, huko Fossanova, karibu na mji wa Terracina, nchini Italia. Akatangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane XXII tarehe 18 Julai 1323 huko Avignon, nchini Ufaransa na kunako mwaka 1567 akatangazwa kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Alikuwa ni mtawa Mdominican. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anapenda kuyakumbuka matukio makuu matatu katika maisha na utume wa Mtakatifu Thoma wa Akwino: Miaka 700 tangu alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu, Miaka 750 tangu alipofariki dunia na kumbukumbu yake imeadhimishwa tarehe 7 Machi 2024 sanjari na miaka 800 tangu alipozaliwa, tukio ambalo litaadhimishwa kunako mwaka 2025. Ni katika kumbukizi ya maadhimisho ya Miaka 750 tangu Mtakatifu Thoma wa Akwino alipofariki dunia, Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii iliyoko chini ya uongozi wa Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, kati ya tarehe 7 na 8 Machi 2024 imeendesha warsha iliyonogeshwa na kauli mbiu: "Ontolojia ya Kijamii ya Mtakatifu Thoma wa Aquinas na Mtazamo Katika Sheria ya Asili. Maarifa Kwa Ajili na Kutoka Katika Sayansi Jamii.” Warsha hii, pamoja na mambo mengine imepembua kwa kina na mapana kuhusu “Ontolojia ya Kijamii katika mwelekeo wa Kitaalimungu; Haki asilia na Ulimwengu wa Kijamii; Uchumi, Siasa na Utawala Bora: Sheria ya Kibinadamu, Teknolojia Sanjari na Mabadiliko ya Kijamii. Kardinali Pietro Parolin, tarehe 7 Machi 2024 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kumbukizi ya Miaka 750 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Thoma wa Akwino, yaani tarehe 7 Machi 1274.

Papa Francisko anakazia huduma ya upendo kwa watu wa Mungu
Papa Francisko anakazia huduma ya upendo kwa watu wa Mungu

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Warsha hii amekazia kuhusu mchango wa Mtakatifu Thoma wa Akwino mintarafu Neno la Mungu, Falsafa na Taalimungu, Sheria Asilia, Utu na Heshima ya Binadamu, Chanzo na Asili ya Mafundisho Jamii ya Kanisa na Mkazo wa Baba Mtakatifu ni Injili ya huduma kwa watu wa Mungu. Mchango wa Mtakatifu Thoma wa Akwino unapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu kwamba, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya imani na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kwamba, neema ya Mungu ndiyo inayoweza kuganga na kuponya utu wa mwanadamu ulioharibiwa kutokana na dhambi. Sayansi Jamii katika ulimwengu mamboleo zinajikita zaidi katika kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii katika ngazi ya mtu binafsi na jamii katika ujumla wake. Hii ni amana na utajiri ambao Mtakatifu Thoma wa Akwino alijichotea kutoka katika Falsafa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sheria ya Mungu na ya maumbile inamwonesha mtu njia ya kufuata ili kutenda mema na kujipatia lengo. Sheria ya maumbile yatangaza amri za kwanza na muhimu zinazotawala maisha ya maadili. Amri zake kuu zinafafanuliwa katika Amri kumi za Mungu. Hii ni Sheria ya maumbile kwa sababu akili inayoiamuru ni ya maumbile hasa ya hali ya binadamu. Hii ni Sheria inayokazia Haki ni mwanga wa ufahamu uliowekwa na Mungu ndani ya binadamu na kwa njia yake mwanadamu anafahamu yale anayopaswa kutenda na yale anayopaswa kuyaacha. Mwanga wa sheria hiii ulitolewa na Mungu wakati wa kazi ya uumbaji. Rej. KKK 1955.

Mtakatifu Thoma wa Akwino Miaka 750 ya kifo chake
Mtakatifu Thoma wa Akwino Miaka 750 ya kifo chake

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ni Mtu mpya: “Maana Adamu, mtu wa kwanza, alikuwa mfano wa yule atakayekuja, yaani Kristo Bwana. Naye Kristo aliye Adamu mpya, akilifunua Fumbo la Mungu Baba na la upendo wake, hudhihirisha kikamilifu kwa binadamu, binadamu alivyo, na kumjulisha wito wake mkuu. Kweli zote hupata chanzo na hitimisho lake kwa Kristo Yesu. Gaudium et spes. 22. Msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa ni: Upatanisho, Mshikamano, Haki na Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, mwanadamu anapaswa kujikita zaidi katika huduma kwa haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea kujikita katika huduma ya upendo, kama alivyofanya Kristo Yesu kwa kuwaosha miguu mitume wake, alionesha sadaka kubwa pasi na kujibakiza kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu na kwamba, upendo wake hauna mipaka. Huu ni muhtasari wa Heri za Mlimani, kiini cha Mafundisho ya Kristo Yesu na mfano bora wa kuigwa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, amana na utajiri waliojichotea washiriki wa warsha hii kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 750 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Thoma wa Akwino, utawasaidia kuchangia katika medani mbalimbali za Sayansi Jamii, ili kukuza na kudumisha: Udugu wa kibinadamu, haki na amani kwa watu wote.

Wito: Kuchangamkia utakatifu wa maisha na ufuasi wa Kristo Yesu
Wito: Kuchangamkia utakatifu wa maisha na ufuasi wa Kristo Yesu

Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahubiri yake kwenye Kanisa la Fossanova amekazia mwaliko kwa watu wote wa Mungu kuwa ni wafuasi wa Mtakatifu Thoma wa Akwino katika utakatifu wa maisha, huku wakijitahidi kutoa kipaumbele cha kwanza na uwiano mzuri kati ya imani na uwezo wa mtu kufikiri na kutenda. Waamini wajitahidi kujenga na kudumisha urafiki na Mwenyezi Mungu kwa njia ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Huu ni wito na mwaliko wa kujitahidi kumuiga Bikira Maria aliyekuwa ni mwanafunzi wa kwanza wa Kristo Yesu. Mtakatifu Thoma wa Akwino kwa hakika alikuwa kama “Majani yanayobeba punje za Neno la Mungu.”

Mt. Thoma wa Akwino

 

12 March 2024, 14:34