Kuna Haja Kwa Ukraine Kuonesha Ujasiri Katika Majadiliano Ili Kukomesha Vita
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Vita kati ya Urusi na Ukraine, Israeli na Palestina pamoja na athari zake kwenye Ukanda wa Gaza ni kati ya tema zilizojadiliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye mahojiano maalum kati yake na Lorenzo Buccella wa Kituo cha Radio Na Televisheni cha Uswis, “Radiotelevisione Svizzera, RSI.” Mahojiano haya yatachapishwa rasmi tarehe 20 Machi 2024. Katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Kanisa limetumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu; Tafakari ya Neno la Mungu; Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tarehe 13 Machi 2013 Baba Mtakatifu Francisko alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kielelezo cha huduma na mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu amegusia pia madhara ya vita na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika kutafuta na kudumisha amani duniani, ili kuondoa giza la maisha linalomsonga mwanadamu sanjari na kuondokana na unafiki katika maisha, ili kutangaza na kushuhudia ukweli. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Vita kati ya Urusi na Ukraine, Israeli na Palestina pamoja na athari zake kwenye Ukanda wa Gaza ni mambo yanayofifisha matumaini ya watu wa Mungu na kwamba, hili ni jambo baya sana na kwamba, vita mara nyingi inahitimishwa kwa pande husika kuwekeana mkataba.
Baba Mtakatifu anatumia sura ya bendera nyeupe iliyopendekezwa wakati wa mahojiano ili kuonesha umuhimu wa kusitisha chuki na uhasama, ili hatimaye, kufikia maridhiano yanayopaswa kufikiwa kwa ujasiri katika mazungumzo na kwamba, matumaini yake ni suluhisho la kidiplomasia kwa haki na amani ya kudumu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Ukraine haina budi kuonesha ujasiri na kuanza kujikita katika majadiliano ili kusitisha vita hii ambayo inaendelea kusababisha athari kubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Vita ya Ukraine, kuna baadhi ya nchi ambazo zimejitolea kuongoza majadiliano kati ya Urusi na Ukraine na kati ya nchi hizi na Uturuki, kabla ya mambo hayajawa mabaya zaidi. Lengo la majadiliano ni kuokoa maisha ya watu. Ukraine ni taifa ambalo limeteseka tangu utawala wa Joseph Stalin kiongozi wa Sovieti ya Urusi. Kumbe, hapa kipaumbele cha kwanza ni ujasiri. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa kwa miaka ya hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliadhimisha Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, iliyoambatana na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kutoa baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa tarehe 27 Machi 2020. Kimya kikuu kilitawala, huku mvua ikinyeesha, Baba Mtakatifu akaongoza sala kwa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofuatilia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii, ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika kipindi hiki maalum katika historia ya mwanadamu kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.
Mama Kanisa anatumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali; Tafakari ya Neno la Mungu; Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ulikuwa tupu, watu wachache sana waliokuwa wanahusika na ulinzi na usalama pamoja na mawasiliano ndio walionekana katika maeneo haya. Katika mahojiano maalum Baba Mtakatifu anakiri umuhimu wa siku hii maalum iliyosimikwa katika kimya kikuu, upweke na sala kwa ajili ya Bikira Maria Afya ya Warumi: “Salus Populi Romani.” Huu ni ujumbe ambao ulipenya na kuingia katika nyumba za watu mbalimbali. Alitambua kile ambacho alipaswa kutenda, yaani kuwaombea wale waliokuwa wanateseka, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaokomboa waja wake, apende kuwaonesha huruma na upendo wake usiokuwa na kikomo. Rangi nyeupe inaonesha utakatifu wa maisha. Utamaduni wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kuvaa kanzu nyeupe ni urithi na amana ya Baba Mtakatifu Pio V aliyezikwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu. Rangi nyeupe ni alama ya furaha, amani na mambo mazuri. Hii ni rangi inayotumiwa na Mama Kanisa wakati wa Pasaka na Noeli.
Itakumbukwa kwamba, ilikua ni tarehe 13 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na tangu wakati huo, akaanza kuvaaa kanzu nyeupe kama Wadominikani. Lakini kanzu nyeupe ni vazi linalovutia alama zinazoonekana kwa urahisi sana, changamoto na mwaliko wa kutokuwa na madoa kwenye kanzu ya maisha na utume wako. Ni kweli kwamba binadamu wote ni wadhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. Kanzu nyeupe inamrejesha Baba Mtakatifu Francisko siku ile ya Ubatizo na Komunio ya kwanza. Wajibu wake mkuu ni kutoa ushuhuda kwa Kanisa, katika kuamua na kutenda, huku akiwa amezunguka na wasaidizi wanaomsaidia kutekeleza utume wake. Upweke ni jambo la kawaida katika kufanya maamuzi katika maisha ya kimungu. Upweke hasi ni hatari sana katika maisha ya mwamini. Baba Mtakatifu anasema, kuna dhambi jamii na kwamba, leo hii, Jumuiya ya Kimataifa inapania kuwekeza katika biashara ya silaha duniani na kwamba, inasikitisha kuona madhara ya vita sehemu mbalimbali za dunia. Tarehe 2 Novemba, Kumbukumbu ya waamini marehemu wote, Baba Mtakatifu huadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Makaburini. Vita nchini Slovakia imewafuta wazee wengi na kwamba, hakuna picha kubwa zaidi ya madhara ya vita kama hii kwani watu wengi wanafariki dunia na kwamba, Njiwa ni alama ya amani.
Baba Mtakatifu anasema, watoto wengi anaokutana nao kutoka kwenye maeneno ya vita hawana furaha, amani na utulivu wa ndani; ni watu ambao kesho yao imepokwa. Vita daima ni kielelezo cha kushindwa ubinadamu. Hakuna vita ya haki bali vita ni matokeo ya biashara haramu ya silaha duniani, kielelzo cha watu wachache kujichumia utajiri wa haraka haraka kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Hiki ni kielelezo cha giza katika maisha ya mwanadamu, ubinafsi unaoteketeza maisha ya watu kimaadili. Kwa bahati mbaya mwanadamu katika maisha yake, anayo pia sehemu ya giza, kielelezo cha dhambi inayomwandama mwanadamu. Giza katika maisha ya mwanadamu linaweza kudumu kwa kitambo kirefu. Baba Mtakatifu anasema, anajitahidi kuhakikisha kwamba, maisha yake yanasimikwa katika ukweli na uwazi; na pale inaposhindikana na kujikuta ameanguka dhambini, anakimbilia mara moja kwenye “Kiti cha huruma ya Mungu” yaani Sakramenti ya Upatanisho. Papa kama binadamu yeyote yule, anaweza kuanguka dhambini, kumbe, hakuna mtu anayeweza kujiamini kupita kiasi. Hii ni changamoto ya kuondokana na unafiki katika maisha na hata wakati mwingine, misaada ya kiutu inatolewa ili kuficha ile dhana ya kosa. Maisha ya mwanadamu yanapaswa kuandikwa kwenye karatasi nyeupe. Maisha ni karatasi nyeupe, yatakakuwa maisha mazuri na mema ikiwa kama yataandikwa na matendo mema, adili na matakatifu, kinyume chake, karatasi itageuka na kuwa nyeusi kutokana na mambo mabaya katika maisha!