Tafuta

Maadhimisho ya Juma Kuu ni muda wa neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu, ili kuwawezesha waamini katika Parokia na Jumuiya zao mbalimbali kumfungulia Kristo Yesu, malango ya nyoyo zao. Maadhimisho ya Juma Kuu ni muda wa neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu, ili kuwawezesha waamini katika Parokia na Jumuiya zao mbalimbali kumfungulia Kristo Yesu, malango ya nyoyo zao.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Juma Kuu Ni Kipindi Cha Neema na Baraka

Maadhimisho ya Juma Kuu ni muda wa neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu, ili kuwawezesha waamini katika Parokia na Jumuiya zao mbalimbali kumfungulia Kristo Yesu, malango ya nyoyo zao, anapowajia katika Maadhimisho ya Juma kuu, tayari kumwendea Kristo Yesu sanjari na kuwaendelea jirani, ili kuwapelekea mwanga na furaha ya imani ya Kikristo. Maadhimisho ya Juma kuu ni muda muafaka wa kutafakari mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Dominika ya Matawi, tarehe 24 Machi 2024 ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Jumamosi kuu, Kanisa katika majonzi makubwa, linasubiria ushindi wa Kristo Yesu Mfufuka! Maadhimisho ya Juma Kuu ni kiini cha Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kusali kwa ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Maadhimisho ya Juma Kuu ni muda wa neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu, ili kuwawezesha waamini katika Parokia na Jumuiya zao mbalimbali kumfungulia Kristo Yesu, malango ya nyoyo zao, anapowajia katika Maadhimisho ya Juma kuu, tayari kumwendea Kristo Yesu sanjari na kuwaendelea jirani, ili kuwapelekea mwanga na furaha ya imani ya Kikristo. Huu ni mwaliko wa kutoka daima, kama mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu; kwa kuheshimiana na katika hali ya uvumilivu, wakitambua kwamba, wao wanachangia mikono, miguu na nyoyo zao, lakini ni Mwenyezi Mungu ndiye anayewaongoza na kuwaonesha njia ya kupitia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, alikwisha elezwa mpango mkakati wa maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Eulalia na Askofu mkuu Celso Morga wa Jimbo kuu la Mèrida-Badajoz aliyekuwa ameambatana na viongozi kadhaa kutoka Jimboni humo.

Maadhimisho ya Juma Kuu ni Kipindi cha Neema na Baraka
Maadhimisho ya Juma Kuu ni Kipindi cha Neema na Baraka

Baba Mtakatifu anasali na kuziombea familia, wagonjwa, watu wanaoishi katika hali ya upweke, maskini na wahitaji zaidi, bila kuwasahau vijana wa kizazi kipya ambao ndiyo “jeuri na amana” ya Udugu wa Mèrida. Kazi zote zinazofanyika katika kipindi cha Mwaka mzima, zihakikishe kwamba, zinabakiza alama ya kudumu katika Maadhimisho ya Juma kuu kwa waamini wote wanaofanya tafakari katika vituo vya toba na wongofu wa ndani, kwani hii ni fursa ya kutangaza na kushuhudia wokovu, unaopaswa kuacha alama ya kudumu. Katika maadhimisho ya Juma kuu, kuna haja ya kutoa kipaumbele cha pekee kwa sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema aliyemwonea huruma na kumtendea kwa rehema. Rej. Lk 10: 25-37. Huu ni mwaliko wa kumwilisha upendo kwa Mungu na jirani kwani watu wote mbele ya Mungu ni ndugu wamoja na wala si maadui.

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma
Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwaka huu 2024 wakati atakaposhiriki Ibada ya Njia ya Msalaba, kuzunguka Magofu ya Colosseo mjini Roma tarehe 29 Machi 2024 Ijumaa kuu, atawakumbuka waamini watakaokuwa wamekusanyika kwenye Magofu ya Merida yaliyoko Jimbo kuu la Merida-Badajoz lililoko nchini Hispania; eneo linalowakusanya waamini wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Haya ndiyo yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu katika ujumbe wake  aliowatumia Jumuiya ya Mèrida “Confraternite di Mérida” kwa maadhimisho ya Juma Kuu kwa mwaka 2024 ambalo lina amana na utajiri mkubwa. Huu ni mji uliobuniwa ili kuwakaribisha na kuwaenzi wanajeshi wastaafu; una makaburi mengi ya Kirumi kama vile Kaburi “la Amphitheatre” hii ni sehemu ambamo kunafanyika Maadhimishyo Mwaka wa Jubilei ya Eulalia kwa heshima ya Shuhuda mdogo wa imani, Mtakatifu Eulalia. Ibada kwa Mtakatifu Eulalia imefanya Mèrida kuwa ni chimbuko la Ukristo nchini Hispania na mahali pa mahujaji katika historia ya Kanisa. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawatakia heri na baraka tele katika maadhimisho ya Juma kuu, ili maadhimisho haya yaweze kuzaa matunda mengi chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Eulalia.

Juma Kuu

 

18 March 2024, 14:33