Mapadre Waungamishaji Wazamisheni Waamini Wenu kwenye Bahari ya Huruma ya Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ibada ya Upatanisho ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kuambata na kukumbatia huruma, upendo na amani ya ndani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, waamini wanakirimiwa tena maisha mapya baada ya kuanguka dhambini na kupoteza ile neema ya utakaso waliyopewa wakati wa Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, Kanisa linazidi kukua na kupanuka, kwa kumfuasa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu asiyekuwa na mawaa. Huu ni mwaliko wa kujitakasa kwa kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu kuzungumza kutoka katika undani wa maisha ya watu, ili kweli Wakleri waendelee kuwa ni vyombo vya huruma na upatanisho kati ya Mungu na watu wake. Katika maisha na utume wa kipadre, Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza! Kwaresima ni kipindi cha neema na mwaliko wa kuanza tena upya safari ya maisha ya kiroho, kwa kutambua kwamba, kama binadamu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanayo mambo mengi yanayowatofautisha, lakini hata katika tofauti zao msingi, bado wanaunganishwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na wanakuwa wamoja katika maisha na utume wa kikuhani. Ibada ya Upatanisho iendelee kuimarisha umoja na mshikamano kati ya wakleri pamoja na waamini katika ujumla wao, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa pamoja na familia ya binadamu! Kwaresima ni kipindi cha kumwilisha Injili ya upendo kwa watu wote bila ubaguzi anasema Baba Mtakatifu.
Kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 8 Machi 2024 Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume linaendesha majiundo endelevu kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, ili wahudumu wa huruma ya Mungu waweze kuwazamisha waamini katika bahari ya huruma ya Mungu. Kati ya mada zinazochambuliwa ni pamoja na: Udhibiti, makosa na vikwazo kwa usikivu wa muungamishaji na mwenye kutubu: haki na wajibu katika Sakramenti ya Kitubio, Uzoefu wa mwenye kukiri dhambi zake: Makundi ya wale wanaotubu: Kesi za kupagawa na pepo wachafu na jinsi ya kuwasaidia waamini; Utambuzi na usindikizaji wa maisha ya kiroho; Akili mnemba ni ushindi au hatari? Mawazo ya kiutendaji juu ya utekelezaji wa huduma ya Maungamo; Kuungama na mwelekeo wa kiroho, “The Ordo Paenitentiae”: tafakari na amana; pamoja na rasilimali kwa ajili ya huduma ya kichungaji ya toba na maungamano: Rehema kamili juu ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa 2025.
Akili mnemba ni teknolojia ya siku zijazo: Kumekuwepo na maboresho makubwa katika maisha ya watu kutokana na kuboreka kwa njia za mawasiliano, huduma kwa umma, elimu pamoja na ongezeko la ulaji; mwingiliano na mafunagamano ya kijamii, mambo yanayojionesha katika uhalisia wa kila siku ya maisha ya watu. Kuna haja ya kufahamu kwa kina maana ya sayansi na teknolojia pamoja na athari zake kwa binadamu. Kumbe, teknolojia ya akili mnemba lazima izingatie mambo yafuatayo: Iwe ni shirikishi, inayotekelezeka kwa misingi ya ukweli na uwazi; usalama, usawa, pamoja na kulinda siri za watu na kwamba, teknolojia ya akili mnemba iwe inategemewa. Kuwepo na chombo kitakachodhibiti masuala ya maadili, haki msingi za watumiaji na waathirika. Teknolojia ya akili mnemba itumie pia tafiti za kitekolojia na kisayansi, ili kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili haki iweze kuchangia katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani duniani. Teknolojia ya akili mnemba ni teknolojia ya siku zijazo na kwamba, itakuwa na athari kubwa katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu, kwa kuweka msingi wa ufahamu hadi kufikia ukweli ambao ni Kristo Yesu mwenyewe.
Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa ya Toba ya Kitume katika hotuba yake ya ufunguzi amekumbusha kwamba, majiundo haya ni mwelekeo wa hija ya matumaini katika kiti cha Mtakatifu Petro sanjari na Sakramenti ya Upatanisho, ndiyo maana kauli mbiu ya majiundo haya kwa mwaka 2024 ambayo yameingia katika awamu yake ya 34 yanaongozwa na kauli mbiu “Kuanzia tena kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho ili kuwa ni mahujaji wa matumaini” kumwelekea Kristo Yesu, kiini cha matumaini ya Wakristo. Sakramenti ya Upatanisho ni chombo muhimu sana kwa maisha ya mwamini binafsi na ni chachu ya toba na wongofu wa ndani, ili kuwa ni kiumbe kipya na hivyo kuwajenga kama mahujaji wa matumaini. Sakramenti ya Upatanisho ni kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake kwani hii ni chachu ya mageuzi ya kweli yanayosimikwa katika utakatifu wa maisha, mafundisho tanzu ya Kanisa, taalimungu, historia na fadhila ya upendo. Yote haya yanaliwezesha Kanisa kutambua asili zake mbili: ile ya kibinadamu na asili ya Kimungu. Mageuzi ya kweli ndani ya Kanisa yaliwezeshe Kanisa kuwa ni shuhuda na chombo cha matumaini. Kanisa kama Jumuiya ya waamini linahitaji: Ushirika, toba na wongofu wa ndani, ili kuwawezesha waamini kumwilisha msamaha katika maisha yao. Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya matumaini na maisha ya uzima wa milele. Wanaoijongea Sakramenti ya Kitubio hupokea humo kutoka huruma ya Mungu ondoleo la kosa lililotendwa dhidi yake, na papo hapo hupatanishwa na Kanisa ambalo dhambi yao imelijeruhi, na ambalo kwa mapendo, mfano na sala huhangaikia wongofu wao. Rej. KKK 1422.