Mawasiliano ya Jamii Ni Sehemu Muhimu Sana ya Huduma Kwa Jamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Rai-Radiotelevisione italiana S.p.A., inayojulikana kama RAI ndiye mtoaji wa pekee wa huduma ya radio na televisheni ya umma nchini Italia. Ni kituo cha televisheni cha kwanza nchini Italia na mojawapo ya makampuni makubwa ya mawasiliano Barani Ulaya, kundi la tano kwa ukubwa la televisheni Barani Ulaya. Kituo cha Televisheni Italia kinachomilikiwa na kuendeshwa na Serikali ya Italia kilianzishwa rasmi tarehe 3 Januari 1954 na kwamba, kwa mwaka 2024 kinaadhimisha kumbukizi ya miaka 70 ya huduma kwa watu wa Mungu nchini Italia. Ilikuwa ni tarehe 27 Agosti 1924 Kituo cha Radio cha Italia kilipoanzishwa na kuanza kurusha matangazo yake rasmi tarehe 26 Oktoba 1924, kumbe kwa mwaka 2024 RAI inaadhimisha pia kumbukumbu ya Miaka Mia Moja tangu kuanzishwa kwake. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Miaka 100 tangu kuanzishwa Kituo cha Radio cha Italia na Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Televisheni Italia, viongozi na wafanyakazi wa Kituo cha Televisheni cha Taifa, Italia, RAI Jumamosi tarehe 23 Machi 2024, wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia kwa namna ya pekee kabisa kuhusu umuhimu wa njia za mawasiliano kama sehemu muhimu sana ya huduma kwa umma katika mchakato wa kutafuta na kudumisha ukweli kwa kusikiliza sauti za wadau mbalimbali, ili kujenga na kudumisha majadiliano. Hii ni huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vyombo vya mawasiliano ya jamii vinapaswa kuota ndoto kubwa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kumbukizi hizi zinasimikwa katika historia ya mawasiliano nchini Italia, changamoto ni kuangalia ya mbeleni kwa matumaini na kwamba, daima kuna mwingiliano na vyombo vingine vya mawasiliano. Tangu kuanzishwa kwake, RAI imekuwa ikifanya kazi bega kwa bega na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, RAI imekuwa ni shuhuda mkubwa katika mabadiliko mbalimbali yaliyojitokeza katika historia na maisha ya watu wa Mungu nchini Italia. Ni katika mantiki hii, RAI kimekuwa ni chombo cha huduma ya mawasiliano ya jamii kwa watu wa Mungu nchini Italia na kwamba, hii ni zawadi kwa jumuiya ya Italia. Hii ni huduma inayopaswa kukidhi mahitaji na matamanio ya watu wa Mungu nchini Italia, huku wakiheshimu na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni huduma muhimu sana inayochangia katika kukuza ukweli, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, katika muktadha wa kuhabarisha, kuburudisha katika tamaduni na teknolojia. Katika mawasiliano huduma hii pamoja na mambo mengine inapaswa kujielekeza katika kukuza na kudumisha ukweli dhidi ya habari za kughushi “fake news” ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Ukweli unapatikana kwa kuwasikiliza wadau mbalimbali na kwamba, huduma hii ni haki ya raia wa Italia kupata habari za kweli bila ya kuwa na maamuzi mbele, kwa kujipatia muda wa kuweza kupima na kutathmini madhara yake kwa umma, ili kukwepa uchafuzi wa uelewa wa watu wa Mungu kwani hata mawasiliano ya jamii yanapaswa kusimikwa katika ikilojia.
Ukweli ni jambo linalowasilishwa kwa watu na kamwe ukweli hauwezi kulazimishwa, kwani ni lazima uheshimu dhamiri za watu wengine kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, ukweli unapokelewa kwa kuwajibika. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha majadiliano ili kuweza kufikia ukweli mkamilifu. Baba Mtakatifu anawakumbusha wafanyakazi wa RAI kwamba, kazi yao inajishughulisha si tu habari, bali pia lugha inayotumika katika: Sinema, vipindi vya Televisheni, burudani, matangazo ya biashara bila kusahau vipindi kwa watoto wadogo. Ili kuepuka umaskini wa utu na heshima ya binadamu kuna haja ya kutafuta na kukuza uzuri, mshikamano, kutunza uhuru na hivyo kufanya kazi kwa umoja na mshikamano ili kuwainua watu waweze: kufikiri na kufurahia; waweze kucheka na hata wakati mwingine kutoa machozi, ili kutoa maana ya kweli katika maisha ya binadamu. Kuhusu teknolojia, Baba Mtakatifu anawaalika wafanyakazi wa RAI kujikita katika kanuni maadili na utu wema; kwa kuepuka ubaguzi, ukosefu wa haki, matumizi mabaya ya teknolojia ya akili mnemba au kwa kutaka kuenzi maoni ya umma. Baba Mtakatifu anakaza kusema, RAI ni chombo cha huduma kwa umma, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kipaumbele cha kwanza ni kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti ndani ya jamii, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hiki ni chombo kinachopaswa kuwasaidia watu wa Mungu kukua na kukomaa na hivyo kuwa na mwelekeo mpya katika maisha kwa kuondokana na hali ya watu kujitafuta wenyewe pamoja na kujiamini kupita kiasi.
RAI ina wajibu wa kuwafunda vijana wa kizazi kipya kuwa na ndoto kubwa katika maisha, kwa kuwa na akili na macho wazi. RAI kama chombo cha mawasiliano jamii kinapaswa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujijengea uwezo wa hali ya juu katika mawasiliano, kwa kukuza ubora wa huduma yake; majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi pamoja na kukuza uraia na ushiriki wa watu wa Mungu. Kila siku RAI inarusha matangazo yake katika nyumba nyingi za Waitaliani, kumbe, inapaswa kujenga mahusiano na mafungamano ya urafiki wa kijamii, ili kuwashangaza wasikilizaji na watazamaji wake. Huu ni mwaliko wa kuweza kushiriki furaha na majonzi ya watu wa Mungu nchini Italia; kwa kuendeleza mchakato wa ujenzi wa umoja na maridhiano ndani ya familia na jamii katika ujumla wake; kwa kusikiliza kwa makini na kujadiliana ili kuhabarisha, pamoja na kusikiliza kwa unyenyekevu. Hii ndiyo njia ambayo RAI inapaswa kuitumia katika huduma yake kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Italia.