Elimu ya dini shuleni ni muhimu sana katika mchakato wa kusaidia kuwalea na kuwafunda wanafunzi tunu msingi za maisha ya imani, maadili na utu wema. Elimu ya dini shuleni ni muhimu sana katika mchakato wa kusaidia kuwalea na kuwafunda wanafunzi tunu msingi za maisha ya imani, maadili na utu wema.  (ANSA)

Mchango wa Kanisa Katika Maendeleo ya Sekta ya Elimu

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la Elimu Kitaifa nchini Hispania amekazia umuhimu wa malezi na majiundo kwa watoto na vijana wa kizazi kipya na kwamba, watoto wote wana haki ya kupata elimu bora, lakini kwa bahari mbaya, si watoto wote wenye fursa ya kupata elimu kutokana na sababu mbalimbali, hasa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Kauli mbiu "Kanisa katika sekta ya elimu: Uwepo na Wajibu wake." Elimu makini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Elimu kwa maana pana ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi. Katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa makusudi na jamii kurithisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine. Elimu ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko pamoja na mabadiliko ya kihistoria na kitamaduni yanayoendelea kujitokeza kwa kasi katika ulimwengu wa utandawazi. Kumbe, kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano katika sekta ya elimu kama sehemu ya mchakato unaopania kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na kutambua kwamba, kila mtu ana haki ya kupata elimu bora, kwa kuzingatia uhuru wake, lakini Kanisa linatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu kama chimbuko la maisha, historia na ulimwengu katika ujumla wake. Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linawaandaa wataalam na mabingwa watakaojisadaka kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kubwa kwa kutambua kwamba, utoaji wa elimu ni kitendo cha upendo na urithishaji wa tunu msingi za maisha. Walimu wawe na uwezo wa kuwamegea vijana wa kizazi kipya: ujuzi na maarifa. Walimu waendelezwe katika taaluma ili waweze kuchangia kwa hali ya juu: Kuhusu weledi, imani na fadhila za maisha ya kiroho zilizoko ndani mwao! Sekta ya elimu ni sawa na bahari kwani haina mwisho, Kanisa limekuwa daima mdau mkuu katika sekta ya elimu, lakini changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, elimu inashiriki kikamilifu katika dhamana ya uinjilishaji mpya kwa kuzingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Papa Francisko analipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kwa elimu
Papa Francisko analipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kwa elimu

Elimu ya dini shuleni ni muhimu sana katika mchakato wa kusaidia kuwalea na kuwafunda wanafunzi tunu msingi za maisha ya imani, maadili na utu wema dhidi ya mmomong’onyoko wa kiutu na kimaadili unaoendelea kuikumba jamii kwa kasi ya ajabu hasa kutokana na athari kubwa za utandawazi, ukanimungu, unafsia na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Elimu ya dini ni chemchemi ya tunu msingi za kimaadili, utu wema na fadhila za kijamii kama vile: juhudi na maarifa; kazi, heshima, nidhamu na utii bila shuruti, mambo msingi katika malezi na makuzi ya wanafunzi katika ujumla wao. Kuna haja ya kukazia, kanuni maadili, utu wema na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, mambo ambayo kwa sasa yanalega lega kutokana na watu wengi kujikita katika uhuru usiokuwa na mipaka. Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, “Conferencia Episcopal Española, CEE” liliendesha Kongamano la Elimu Kitaifa lililonogeshwa na kauli mbiu “Kanisa katika sekta ya elimu: Uwepo na Wajibu Wake. "La Iglesia en la Educación” Hii ilikuwa ni fursa ya kutembea kwa pamoja na kusikilizana kama Kanisa mintarafu: Malezi na makuzi ya watoto na vijana wa kizazi kipya, kwa kutambua kwamba, elimu ni haki msingi kwa wote. Imekuwa ni furrsa ya kubainisha pia changamoto katika sekta ya elimu kama vile: Udhalilishaji wa kimtandao “Bullism”, nyanyaso za kijinsia, mitandao ya vijana waovu, mambo yanayokwenda kinyume cha zawadi ya maisha.

Kanisa limechangia sana maboresho ya sekta ya elimu duniani.
Kanisa limechangia sana maboresho ya sekta ya elimu duniani.

Kanisa katika hali na mazingira kama haya linapania kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la Elimu Kitaifa nchini Hispania amekazia umuhimu wa malezi na majiundo kwa watoto na vijana wa kizazi kipya na kwamba, watoto wote wana haki ya kupata elimu bora, lakini kwa bahari mbaya, si watoto wote wenye fursa ya kupata elimu kutokana na sababu mbalimbali, hasa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu amelipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa elimu kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, Kanisa halina budi kujitahidi kuhakikisha kwamba, hakuna mtu anayeachwa nyuma, kwani kama kuna watu wanaoachwa nyuma, huo ni mwanzo wa kuibuka kwa utamaduni wa kutupwa, utandawazi usiojali wala kuguswa na matatizo ya wengine. Mkazo katika elimu usaidie kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu; haki na amani; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anakaza kusema, sifa bainifu ya Elimu ya Kikatoliki katika nyanja zote za maisha ni ubinadamu wa kweli; ubinadamu unaopata msingi wake katika imani na hivyo kuzalisha utamaduni. Kristo Yesu, daima anaishi katika nyumba za waja wake, anazungumza lugha yao na hufuatana na familia pamoja na waja wake.

Elimu ya dini ni muhimu sana katika malezi na makuzi ya watoto na vijana
Elimu ya dini ni muhimu sana katika malezi na makuzi ya watoto na vijana

Kwa hakika, Kanisa limekuwa na mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Hispania na kwamba, kuna umati mkubwa wa watu ambao wamechangia katika maboresho ya sekta ya elimu nchini Hispania, kiasi hata cha kujenga utamaduni wa elimu na hivyo kuwa ni sehemu ya urithi na utajiri wa Kanisa zima. Baba Mtakatifu anawatia shime Maaskofu wa Hispania kujenga na kudumisha mshikamano wa kidugu sanjari na kuthamini utambulisho wao wa kiimani. Daima wajenge mtandao katika shughuli na utume wao na kamwe wasipende kufanya kazi kipeke peke! Ikumbukwe kwamba, elimu inasimikwa katika msingi wa uhuru, urafiki wa kijamii pamoja na utamaduni wa watu kukutana. Baba Mtakatifu anawapongeza Maaskofu wa Hispania kuipembua sekta ya elimu nchini mwao katika mapana ya elimu, kwa kusoma alama za nyakati na kwamba, anapenda kuwatia shime wadau wote wa elimu, watambue kwamba, huu ni utume maalum mbele ya Mwenyezi Mungu na jamii katika ujumla wake.

Elimu iwajengee wanafunzi matumaini
Elimu iwajengee wanafunzi matumaini

Kwa upande wake Kardinali Juan José Omella Omella, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcellona na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania katika hotuba yake amegusia kuhusu: Maana ya Elimu ambao kimsingi ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano na hofu ya Mungu; Uinjilishaji mpya sanjari na kujikita katika kutafuta na kuambata kile kilicho kweli, chema na kizuri “Verum, bonum, pulchrum” pamoja na kudumisha Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” kwa njia ya ushuhuda na kazi zao. Wasaidie kuhamasisha tunu msingi za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani; uzuri, wema, ukarimu na udugu wa kibinadamu. Kila mtu ajitahidi kuwajibika, ili kuendeleza mchakato wa mageuzi; ili kuganga na kuponya ulimwengu huu ambao umejeruhiwa vibaya; kila mmoja, akijitahidi kuwa ni Msamaria mwema, anayeguswa na mahangaiko ya wengine, badala ya kuchochea chuki na uhasama kati ya jamii. Huu ni mfumo wa elimu wenye mwono mpana na wenye uwezo wa kuwashirikisha wote ili kutoa majibu yatakayosaidia kujenga mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ulimwengu mamboleo unawahitaji watu watakaojenga na kudumisha amani na utulivu.

Kanisa na Elimu
03 March 2024, 16:01