Mchango na Sadaka ya Ijumaa Kuu 2024: Waathirika wa Vita Nchi Takatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mchango na Sadaka ya Ijumaa Kuu kwa Ajili ya Nchi Takatifu ni fursa ya moja kwa moja kwa watu wa Mungu sehemu mbalimballi za dunia kuwa ni mashuhuda na vyombo haki, amani na maridhiano kati ya watu. Msaada huu ni ishara ya umoja na ushiriki katika utume wa Mama Kanisa, katika mchakato wa kulinda na kuendeleza maeneo Matakatifu. Mchango na sadaka hii inayotolewa na waamini, kila Ijumaa kuu ni kiungo muhimu sana kwa Wakristo wanaoishi katika Nchi Takatifu. Mtakatifu Paulo VI, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, alitembelea Nchi Takatifu mwezi Januari 1964 na kuguswa na mahitaji ya Wakristo. Katika Wosia wake wa Kitume “Nobis in animo” yaani “Umuhimu wa Kanisa katika Nchi Takatifu” uliochapishwa tarehe 25 Machi 1974, alikazia umoja na mshikamano wa waamini. Huo ukawa ni chimbuko la Mchango na Sadaka ya Ijumaa kuu kwa ajili ya Nchi Takatifu: "Pro Terra Sancta." Mtakatifu Paulo VI alihimiza sana umuhimu wa uwepo endelevu wa Kanisa katika Nchi Takatifu, kama amana na urithi wa imani; ushuhuda angavu wa Jumuiya ya Wakristo unaoonesha jiografia ya ukombozi.
Tangu wakati huo, Kanisa linaendelea kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoteseka, kunyanyaswa na hata kuuwawa huko Mashariki ya Kati, lakini hasa kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kutoka kwa Makanisa yote duniani, ni alama ya upendo, udugu na mshikamano wa Kanisa kwa watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu. Huu ni ushuhuda wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika uekumene wa damu, huduma na sala pamoja na kuendeleza majadiliano ya kidini ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu katika misingi ya: haki, amani na maridhiano. Ni kwa njia ya ushuhuda wa umoja, upendo na mshikamano Kanisa linataka kuwajengea waamini na watu wote wenye mapenzi huko Mashariki ya kati Injili ya amani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi ili kuondokana na: vita, vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kiimani, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kwa waamini wa Kanisa Katoliki huko Nchi Takatifu, iliyochapishwa tarehe 27 Machi 2024, hasa anapenda kuwakumbatia waathirika wa vita kati ya Israeli na Palestina; watoto waliopokwa maisha yao ya baadaye; watu wanaohuzunika na kuwa na uchungu kutokana na madhara ya vita. Lakini maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ni moyo na kiini cha imani ya Kikristo inayopata chimbuko lake kutokana na mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Nchi Takatifu ni mahali pa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Nchi Takatifu ni kiini cha historia ya wokovu na jiografia ambayo kwa miaka mingi imeandikwa kwa ushuhuda na uwepo wa Wakristo katika Nchi Takatifu. Hiki ni kielelezo cha imani na ushuhuda wa upendo na matumaini. Kristo Yesu uzima wa waamini wake, kama Msamaria mwema, awamiminie faraja na divai ya matumaini majeraha yao ya kiroho na kimwili; waguswe na kuhisi upendo wake wa kibaba na kutoka kwa waamini wa Kanisa Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia. “Ili wote wawe wamoja” ndiyo kauli mbiu iliyoongoza Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu, tarehe 5 Januari 1964.
Baba Mtakatifu amegusia umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha amani na usalama wa watu wa Mungu katika Nchi Takatifu. Jumuiya ya Wakristo huko katika nchi Takatifu imekuwa ni shuhuda wa Fumbo la Pasaka. Wakristo huko Nchi Takatifu ni taa zinazowaka na kwamba, wao ni mbegu ya wema katika nchi yenye mapambano. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, kutokana na mateso yao ya sasa wataweza kufufuka na Kristo Yesu, kwa ajili ya Pasaka ya Amani. Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika barua waliyowaandikia Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kuhusu sadaka na mchango wa Ijumaa Kuu kwa mwaka 2024, wanasema uwe ni msaada kwa ajili ya watu wanaoteseka kutokana na vita kati ya Israeli na Palestina! Watu ambao wamewapoteza watoto, ndugu na jamaa kutokana na vita hii bila kuwasahau wale ambao wamekuwa ni vilema kwa sababu ya vita. Vita imepelekea hata mahujaji wa matumaini kusitisha safari zao huko Mashariki ya Kati. Kristo Yesu Mfalme wa amani, Mungu pamoja nasi; Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake amezaliwa katika Nchi Takatifu.
Baba Mtakatifu Francisko hachoki kutoa mwaliko kwa watu wa Mungu huko nchini Takatifu kuhakikisha kwamba, wanaheshimu utakatifu wa maisha, utu, na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anaendelea kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wanaoteseka kutokana na vita kati ya Israeli na Palestina. Shirika la Wafranciskani Walinzi wa Nchi Takatifu wanaendelea kusali na kuombea amani duniani. Kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuonesha mshikamano wao wa dhati na waathirika wa vita. Mchango huu ni muhimu sana katika mchakato wa kulinda na kuendeleza maeneo matakatifu, dhidi ya uchoyo na ubinafsi. Makanisa ni sehemu ya amana na urithi wa watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati. Lakini kutokana na vita watu wamelazimika kuzikimbia nchi na Makanisa yao, mahali ambapo wazazi wao walipatumia kwa ajili ya sala. Mchango wa Ijumaa Kuu ni muhimu sana, kwa ajili ya Kanisa mahalia, ili liweze kupata njia mpya ya kuwahudumia waathirika wa vita; kugharimia ujenzi wa mkazi mapya, kutoa fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya, kugharimia elimu pamoja na majiundo makini, huku wakiendelea kubaki katika nchi yao, kielelezo cha ushuhuda wa imani. Kumbe, sadaka na mchango wa Ijumaa kuu kwa mwaka 2024 ni kielelezo cha upendo na mshikamano na watu wa Mungu katika Nchi Takatifu.