Mpango Mkakati wa "Saa 24 Kwa Ajili ya Bwana" Kwa Mwaka 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujizatiti kikamilifu katika hija ya Kipindi cha Kwaresima, yaani Siku 40 katika Jangwa la maisha ya kiroho kwa njia ya: toba na wongofu wa ndani; kufunga, kusali, kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kulinafsisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya: imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima na kwa mwaka huu ni tarehe 8-9 Machi 2024 na mkazo unawekwa katika maisha ya sala na msamaha wa dhambi. Kila Jimbo linapaswa kufanya maadhimisho haya ili kuwapatia waamini nafasi ya kuweza kuchunguza dhamiri zao, kujuta, kuungama na hatimaye, kutimiza malipizi, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huu ni muda pia wa kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa kuongozwa na Neno la Mungu kutoka katika Sura ya sita ya Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Warumi. Kufa na kuishi pamoja na Kristo ili “kuenenda katika upya wa uzima.” Baba Mtakatifu katika Maadhimisho ya Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” Ijumaa tarehe 8 Machi 2024 ataongoza Ibada hii kwenye Parokia ya “San Pio V” iliyoko Jimbo kuu la Roma. Katika Maadhimisho haya waamini wote wanaweza kupata kitubio na maondoleo ya dhambi. Baba Mtakatifu pia atakuwepo kwenye Kiti cha huruma ya Mungu ili kuwaungamisha baadhi ya waamini. Makanisa yaliyo wazi ni kielelezo cha upendo wenye huruma wa Mungu kwa waja wake.
Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kushiriki Ibada hii kwa uchaji, kama njia ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Waamini watambue kwamba, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wa Mungu kwa binadamu. Kwa njia hii, waamini nao wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Hii ni huruma inayopaswa pia kushuhudiwa katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho inayogusa undani wa mtu, kwani hili ni chimbuko la amani na utulivu wa ndani. Ni huruma inayosamehe na kuokoa. Mapadre waungamishi wanao wajibu wa kuwa ni watumishi waaminifu wa huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu, kwa kuwapokea waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma katika mfano wa Mwana mpotevu! Maadhimisho ya Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana”, ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma ya Baba wa milele. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani. Ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu ambao ni kiini cha Injili; huruma ambayo kimsingi inapaswa kupenya na kugota katika moyo na akili ya binadamu. Kanisa linapaswa kuwaendea watu wote pasi na ubaguzi kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.
Huu ni ushuhuda unaofumbata huruma ya Mungu, mwanga na njia inayowaelekeza watu kwa Baba wa milele! Huruma ya Mungu ni sehemu ya mpango wa maisha unaoleta furaha na amani ya ndani! Mapadre wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayoadhimishwa kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Upatanisho! Msamaha ni chombo kilichowekwa kwenye mikono dhaifu, ili kumwezesha mwamini kuachilia mbali hasira, ghadhabu, ukatili na kisasi ili kuishi kwa furaha. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika zaidi ili watoto wake waweze kuwa na afya bora zaidi. Wakati umewadia kwa Mama Kanisa kuitikia kwa mara nyingine tena wito huu wa furaha na msamaha. Ni wakati wa kurejea kwenye msingi wa imani na kubeba madhaifu na mahangaiko ya jirani. Huruma ya Mungu ni msukumo unaowaamsha waamini kwa maisha mapya na hivyo kuwatia ujasiri wa kuangalia wakati ujao kwa matumaini. Msamaha wa dhambi zilizotendwa baada ya Ubatizo hutolewa kwa Sakramenti ya pekee iitwayo: Sakramenti ya uongofu, ungamo, kitubio na upatanisho. Sakramenti hii inaundwa na matendo makuu matatu: Kutubu, Kuungama na Kutimiza Malipizi. Kimsingi, maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho yamefumbata kiini halisi cha Ukristo na Kanisa: Mwana wa Mungu alijifanya mtu ili kutuokoa na aliamua kulihusisha Kanisa kama "chombo cha lazima" katika kazi hii ya wokovu, na ndani yake, wale aliowachagua, akawaita na kuwaweka wawe wahudumu wake.