Pamoja na Pietro,daima
Na Andrea Tornielli
Katika ukimya wa viziwi wa diplomasia, katika mandhari yenye sifa ya kukosekana kwa mpango wa kisiasa na uongozi wenye uwezo wa kuahidi juu ya amani, wakati ulimwengu umeanza mbio za silaha kwa kutenga pesa kwa vyombo vya kisasa vya kifo ambazo zingetosha kuhakikisha mara mbili huduma ya msingi ya afya kwa wakazi wote wa dunia na kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafuzi, sauti ya pekee ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kusihi kunyamazisha silaha na kuomba ujasiri wa kupendelea njia za amani. Anaendelea kuomba kusitishwa kwa mapigano katika Nchi Takatifu, ambako mauaji ya kinyama ya tarehe 7 Oktoba yaliyotekelezwa na magaidi wa Hamas yalifuatwa na yanaendelea kutekelezwa na mauaji ya kutisha huko Gaza.
Anaendelea kuomba kunyamazisha silaha katika mzozo wa kutisha uliozuka katikati mwa Ulaya ya Kikristo, huko Ukraine iliyoharibiwa na kuteswa na milipuko ya jeshi la wavamizi la Urusi. Anaendelea kutoa wito wa kuwepo kwa amani katika sehemu nyingine za dunia ambako mizozo iliyosahaulika ambayo ni sehemu kubwa zaidi ya mzozo wa kimataifa inapigwa vita kwa ghasia zisizoelezeka. Askofu wa Roma anaingia mwaka wa kumi na mbili wa Upapa katika saa ya giza, na hatima ya wanadamu ambao wanatawaliwa bila huruma ya watawala wasio na uwezo wa kutathmini matokeo ya maamuzi yao ambayo yanaonekana kusalimu amri kwa kuepukika kwa vita. Na kwa ufasaha na uhalisia anasema kuwa “anayeiona hali, anayewafikiria watu, ana nguvu zaidi”, yaani, “mwenye ujasiri wa kujadili,” kwa sababu “majadiliano” ni neno la ujasiri”, ambalo haipaswi kuona aibu.
Baba Mtakatifu Francisko, akipinga kutoelewana kwa watu wa karibu na walio mbali, anaendelea kuweka utakatifu wa maisha katika kituo hicho, kuwa karibu na wahanga wasio na hatia na kukemea masilahi chafu ya kiuchumi yanayochochea barabara za vita kwa kujivika unafiki. Kwa kutazama kwa haraka miaka hii kumi na moja iliyopita ya historia kunatufanya tuelewe thamani ya kinabii ya sauti ya Petro. Kengele ya dharura, ilitolewa kwa mara ya kwanza miongo miwili iliyopita, kuhusu vita vya tatu vya dunia vilivyomegeka vipande vipande. Katika Waraka wa kijamii wa Laudato si' (2015, kuhusu Utunzaji Bora wa Mazingira), ambao ulionesha jinsi mabadiliko ya hali ya Tabianchi, uhamiaji, vita na uchumi unaoua ni matukio yaliyounganishwa na yanaweza kushughulikiwa tu kupitia mtazamo wa kimataifa. Waraka mkubwa wa Udugu wa kibinadamu (Fratelli tutti, 2020), ambao ulionesha njia ya kujenga ulimwengu mpya unaotegemea udugu, kwa mara nyingine tena ukiondoa wale wanaojifanya watetezi kwa matumizi mabaya ya jina la Mungu kuhalalisha ugaidi, chuki na vurugu. Na kisha marejeo ya mara kwa mara katika mafundisho yake ya huruma, ambayo yanasuka kiungo kizima cha upapa wa kimisionari.
Katika jamii za kidunia na “kimiminika”(Liquid) bila tena uhakika, hakuna kitu kinachoweza kuchukuliwa kirahisi na uinjilishaji – alifundisha Papa Francisko - huanza tena kutoka katika muhimu, kama tunavyosoma katika Injili ya Furaha( Evangelii gaudium (2013): “Tumegundua tena kwamba hata katika katekesi tangazo la kwanza au kerygma lina jukumu la msingi, ambalo lazima liwe kiini cha shughuli ya uinjilishaji na kila jaribio la upyaishaji wa Kikanisa. [...] Umuhimu wa kerygma unahitaji sifa fulani za tangazo ambalo ni muhimu kila mahali leo hii: kwamba linaonesha upendo wa kuokoa wa Mungu kabla ya wajibu wa kiadili na wa kidini, kwamba haulazimishi ukweli na kwamba unavutia uhuru ambao una maelezo fulani ya furaha, uchangamfu, ari na utimilifu wenye upatanisho ambao haupunguzi mahubiri kwa mafundisho machache ambayo nyakati fulani ni ya kifalsafa zaidi kuliko ya uinjilishaji.”
Hili linahitaji mielekeo fulani kutoka kwa mwinjilishaji ambaye husaidia kukaribisha tangazo vyema zaidi: ukaribu, uwazi kwa mazungumzo, subira, ukarimu wa kukaribishwa usiolaani.” Kwa hiyo ushuhuda wa huruma unawakilisha kipengele cha msingi cha “upendo huu wa Mungi wa kuokoa” ambao ni “kabla ya wajibu wa kimaadili na kidini.” Kwa maneno mengine, wale ambao bado hawajakutana na ukweli wa Kikristo, kama Papa Benedikto XVI alivyokuwa tayari ameona kwa uwazi mnamo Mei 2010, ni vigumu kubaki bila kuvutiwa sana na uthibitisho wa kanuni za maadili na wajibu, kwa kusisitiza vizuizi, orodha za kina za dhambi, hukumu, au rufaa isiyofaa kwa maadili ya zamani. Katika chimbuko la ukaribisho, ukaribu, upole, usindikizaji, katika asili ya jumuiya ya Kikristo yenye uwezo wa kukumbatia na kusikiliza, kuna urejesho wa huruma ambayo imepatikana na inayotafutwa - licha ya mapungufu elfu na kuanguka na kurudishwa.