Papa ameongoza Misa ya Coena domini katika gereza la wanawake
Na Angela Rwezaula – Vatican.
Maadhimisho ya fumbo Kuu la Pasaka kwa kwaida linaanza na maadhimisho ya Karamu kuu ya mwisho ambayo ni siku ya Alhamisi Kuu, kabla ya Bwana kukamatwa na kuanza mateso hadi kusulibiwa na kufa msalabani siku ya Ijumaa. Ni katika muktadha huo ambapo Alhamisi Kuu tarehe 28 Machi 2024, alasiri Baba Mtakatifu Francisko alikwenda katika Gereza la Wanawake la Rebbia jijini Roma, kuadhimisha Misa ya Coena Domini yaani Karamu Kuu na ibada ya kuosha miguu kwa wafungwa.
Wakati wa mahubiri yake yasiyotayarishwa, Baba Mtakatifu alianza kusema kuwa “Wakati huu wa karamu kuu ya jioni, kuna vipindi viwili vinavutia umakini wetu. Kuoshwa kwa miguu ya Yesu: Yesu anajinyenyekeza, kwa ishara hiina Yesu anatufanya tuelewe kile alichokuwa amesema: “Sikuja kutumikiwa, bali kutumikia”. Kwa njia hiyo “anatufundisha njia ya utumishi. Kipindi kingine cha kusikitisha ni usaliti wa Yuda ambaye hana uwezo wa kuendelea na upendo, na kisha pesa, ubinafsi unampeleka kwenye jambo hili baya. Lakini Yesu anasamehe kila kitu.”
Baba Mtakatifu akiendelea alisema “Yesu anasamehe daima. Anaomba tu kwamba tuombe msamaha. Siku moja, nilisikia bibi mzee mwenye busara, bibi mzee, kutoka kwa watu ... Alisema hivi: “Yesu hachoki kusamehe: Sisi ndio tunachoka kuomba msamaha.” Kwa njia hiyo Papa alisema: “Leo tuombe neema ya Bwana ili asituchoke. Kwa sababu daima, sisi sote tuna kushindwa kidogo, na kushindwa pakubwa lakini kila mtu ana historia yake mwenyewe. Lakini Bwana hutungoja kila wakati, kwa mikono iliyo wazi, na hachoki kusamehe.” Papa kwa kusisitiza juu ya siku hiyo amesema “Leo hii tutafanya kama Yesu alivyofanya: ile ya kuosha miguu. Ni ishara inayovutia hisia kwenye wito wa huduma. Tuombe Bwana atukuze, sisi sote, katika wito wa huduma. Asante.”Alihitimisha mahubiri hayo mafupi.
Baada ya hapo ilifuata ishara ya kuosha miguu ambapo Baba Mtakatifu amewaosha miguu Wanawake 12 ambao wanatoka mataifa tofauti: kuanzia na Italia, Bulgaria, Nigeria, Ukraine, Urusi, Peru, Venezuela na Bosnia na wana umri wa kati ya miaka 40 na 50.Takriban watu 200 walihudhuria Misa hiyo.
Ndugu msomaji kwa ufupi adhimisho Kuu hili linalodumu kwa muda wa siku tatu ni kuanzia Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Takatifu inayotandalia makuu ya ufufko wa Bwana. Kwa hiyo Alhamisi Kuu, Mama Kanisa anaadhimisha mambo makuu matatu: kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja Takatifu na Amri Kuu ya mapendo. Ni kiku kwa hakika ya kuwaenzi Mapadre kwa huduma yao. Leo hii hatuma budi kuwaombea mapadre wetu. Na siku Ijumaa kuu inakumbusha mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na kifo chake, hadi Jumamosi kuu ya ukimya tukiwa tunatazamia Pasaka ya Bwana, ufufuko wa Bwana.