Papa amewatumia Ujumbe watoto , katika fursa ya kuelekea Siku I ya Watoto Duniani 25 na 26 Mei 2024 jijini Roma. Papa amewatumia Ujumbe watoto , katika fursa ya kuelekea Siku I ya Watoto Duniani 25 na 26 Mei 2024 jijini Roma.  (Vatican Media)

Papa ametuma ujumbe wake katika fursa ya Siku ya Watoto duniani 25-26 Mei 2024

Katika Ujumbe wa Papa kwa ajili ya Siku I ya Watoto Ulimwenguni itakayo adhimishwa jiji Roma 25 na 26 Mei 2024 anasisitiza kutosahau watoto wadogo ambao wameibiwa udogo wao na kwa hiyo mada kuu ya Papa ni thamani ya ushirikishwaji na msamaha kwani urafiki unakua katika uvumilivu ,ujasiri,ubunifu.mawazo na bila kuogopa,wala bila hukumu.

Na Angella Rwezaula – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko ametoa ujumbe wake kwa ajili ya Siku ya I ya Watoto duniani, inayotarajiwa kufanyika mjini Roma tarehe 25 na 26 Mei 2024. Ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican,  ambapo Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana kwa furaha kuu alitangaza tarehe hizo kuwa ni Siku ya Watoto Ulimwenguni, itakayo adhimishwa kwa mara ya kwanza mjini Roma. Maadhimisho haya yataratibiwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Katika ujumbe kuelekea siku hiyo Baba Mtakatifu anabainisha kwamba: “wapendwa watoto kike na kiume inakaribia siku yenu ya Kwanza ya Ulimwengu ambayo itakuwa jijini Roma tarehe 25 na 26 Mei Ijayo. Kwa njia hiyo nimefikiria kuwatumia ujumbe, na ninayo furaha kwamba mnaweza kuupokea na kuwashukuru wote ambao watajitahidi kufanya kila njia muweze kuupokea. Ninawaelekea awali ya yote binafsi, wewe, Mpendwa mtoto msichana na wewe mpendwa mtoto mvulana, kwa sababu “wewe ni mwenye thamani”machoni pa Mungu (Is,43,4), kama Biblia inavyotufundisha na kama Yesu mara nyingi alivyojionesha. Na wakati huo huo, ujumbe huu ninawatumia wote, kwa sababu wote ni muhimu, na kwa sababu pamoja, wa karibu na wa mbali, mnaonesha shauku ya kila mmoja ya kukua na kujipyaisha. Mkumbuke kuwa sisi wote ni watoto na ndugu, na hakuna anayeweza kuishi bila mtu ambaye anamweka duniani na wala kukua bila kuwa na wengine ambao ni kutoa upendo na wa kupokea upendo (rej. Fratelli tutti, 95).

Hivyo ninyi nyote, wasichana na wavulana, furaha ya wazazi wenu na familia zenu, pia ni furaha ya ubinadamu na ya Kanisa, ambalo kila mmoja wenu ni kama kiungo katika mnyororo mrefu sana, uliotoka zamani hadi wakati ujao na ambao unashughulikia Dunia nzima. Ndiyo sababu ninapendekeza kwamba msikilize kwa makini historia za watu wazima: za mama zenu, baba, babu na bibi! Na wakati huo huo tusiwasahau wale ambao miongoni mwenu bado ni wadogo sana, ambao tayari wanajikuta wanapambana na magonjwa na shida, hospitalini au nyumbani, wale ambao ni waathriwa wa vita na vurugu, wale wanaoangaika na njaa na kiu, wanaoishi mitaani, wale wanaolazimishwa kuwa askari au kukimbia kama wakimbizi, kutengwa na wazazi wao, wale ambao hawawezi kwenda shule, wale ambao ni waathiriwa wa magenge ya uhalifu, madawa ya kulevya au aina nyingine za utumwa na unyanyasaji. Kwa kifupi, wale watoto wote ambao utoto wao bado unaibiwa kikatili leo hii. Wasikilize, au tuseme, tuwasikilize, kwa sababu katika mateso yao wanazungumza nasi juu ya ukweli, kwa macho yaliyotakaswa na machozi na kwa tamaa hiyo ya uthabiti ya mema ambayo huzaliwa ndani ya mioyo ya wale ambao wameona kweli jinsi uovu ulivyo mbaya.

Baba Mtakatifu Francisko anendelea katika ujumbe huo akiwalekea watoto kwamba “Rafiki zangu wadogo, ili kujipyaisha sisi wenyewe na ulimwengu, haitoshi kuwa tuko pamoja sisi kwa sisi, ni lazima kuunganishwa na Yesu. Tunapokea ujasiri mwingi kutoka kwake: yuko karibu daima, Roho yake hututangulia na inatusindikiza kwenye njia za ulimwengu. Yesu anatuambia: “Tazama, ninayafanya yote mapya” (rej. Uf 21:5); ni maneno ambayo nilichagua kama Kauli mbiu ya Siku yenu ya Kwanza ya Watoto Duniani. Maneno haya yanatualika kuwa wepesi kama watoto katika kushika mambo mapya yanayoletwa na Roho ndani yetu na kutuzunguka. Tukiwa na Yesu tunaweza kuota ubinadamu mpya na kujitolea kwa ajili ya  jamii yenye udugu na makini zaidi kwa nyumba yetu ya pamoja, tukianza na mambo rahisi, kama vile kusalimia wengine, kuomba ruhusa, kuomba msamaha, kusema asante. Dunia inabadilishwa kwanza kupitia na vitu vidogo, bila kuona aibu kuchukua hatua ndogo tu. Kwa hakika, udogo wetu unatukumbusha kwamba sisi ni dhaifu na kwamba tunahitajiana sisi kwa sisi, kama viungo vya mwili mmoja (taz. Rm 12:5; 1Kor 12:26).

Na kuna zaidi. Kiukweli, watoto wapendwa wasichana na wavulana, hatuwezi hata kuwa na furaha peke yetu, kwa sababu furaha inakua kwa kiwango ambacho tunashirikishana: inazaliwa na shukrani kwa zawadi ambazo tumepokea na ambazo sisi hushiriki na wengine. Tunapoweka  kile tulichopokea tu kwa ajili yetu wenyewe, au hata kutupatia hasira ili kupata hicho au zawadi hiyo, kiukweli tunasahau kwamba zawadi kubwa zaidi ni sisi wenyewe, kwa kila mmoja wetu: sisi ni “zawadi kutoka kwa Mungu.” Zawadi nyingine ndiyo, ni muhimu, lakini ni kuwa pamoja tu. Tusipozitumia kwa hilo tutakuwa haturidhiki na hazitatutosha kamwe. Walakini, ikiwa mko pamoja kila kitu ni tofauti! Fikirieni  kuhusu marafiki zenu: jinsi ya ajabu ya kuwa pamoja nao, nyumbani, shuleni, katika parokia, katika mikutano, kila mahali; kucheza, kuimba, kugundua mambo mapya, kufurahia, wote pamoja, bila kumwacha mtu yeyote nyuma. Urafiki ni mzuri na hukua hivyo tu, katika kushiriki na kusameheana, kwa uvumilivu, ujasiri, ubunifu na maono, bila woga na bila ubaguzi.

Katika hili, Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza tena kwamba “Na sasa ninataka kuwapa siri muhimu: ili kuwa na furaha ya kweli kunahitaji kusali, kuomba sana, kila siku, kwa sababu sala inatuunganisha moja kwa moja na Mungu, inajaza mioyo yetu na mwanga na joto na inatusaidia kufanya kila kitu kwa uaminifu na Utulivu. Yesu pia alisali kwa Baba kila wakati. Na je mnajua alimwitaje? Katika lugha yake alimuita tu Abba, ambayo ina maana ya Baba (rej Mk 14:36). Hebu tufanye pia hivyo! Daima tutahisi yuko karibu nasi. Yesu mwenyewe alituahidi hili alipotuambia: “Walipo wawili na  watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo hapo katikati yao” (rej. Mt 18:20).

Wapendwa, wasichana na wavulana, mnajua kwamba  mwezi Mei kutakuwa na wengi wetu jijini Roma, sawa na ninyi, ambao watakuja kutoka duniani kote! Na kwa hivyo, ili kujitayarisha vyema, ninapendekeza kwamba muombe kwa kutumia maneno yale yale ambayo Yesu alitufundisha ya: Baba yetu. Sali sala hii  kila asubuhi na kila jioni, na kisha pia na familia yenu, na wazazi wenu, kaka, dada na babu na bibi. Lakini sio kama aina ya mtindo, hapana! Ni kufikiri juu ya maneno ambayo Yesu alitufundisha. Yesu anatuita na anataka tuwe wahusika wakuu pamoja Naye wa Siku hii ya Ulimwengu, wajenzi wa ulimwengu mpya, wa kibinadamu zaidi, wa haki na amani. Yeye aliyejitoa Msalabani ili kutukusanya sisi sote katika upendo, Yeye aliyeshinda kifo na kutupatanisha na Baba, anataka kuendeleza kazi yake ndani ya Kanisa, kwa njia yetu. Fikirini juu yake, hasa ninyi mnaojitayarisha kupokea Komunyo yenu ya Kwanza. Wapendwa, Mungu, ambaye ametupenda siku zote (taz. Yer 1:5), ana  mtazamo  kwetu wa baba mwenye upendo zaidi na mama wapole zaidi. Hatusahau kamwe (rej. Isa 49:15) na kila siku hutusindikiza na kutufanya upya kwa Roho wake.

Pamoja na Maria Mtakatifu na Mtakatifu Joseph tuombe kwa maneno haya: Njoo, Roho Mtakatifu, utuoneshe uzuri wako unaonekana katika nyuso za wasichana na wavulana wa dunia. Njoo Yesu, ufanyaye yote kuwa mapya, kwamba wewe ndiwe njia inayotuongoza kwa Baba, njoo ukae nasi. Amina.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umetiwa saini mjini Roma tarehe 2 Machi 2024 kwa ajili ya Watoto wote duniani katika kuelekea Siku yao ya I ya Watoto tarehe 25 na 26 Mei 2024.

Ujumbe wa Papa kwa watoto katika fursa ya Siku ya I kimataifa ya Watoto
02 March 2024, 13:53