Papa atoa wito wa kusitisha vurugu huko Haiti na kwingineko duniani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 10 Machi 2024 amerudi katika tukio la kimataifa lililoadhimishwa tarehe 8 Machi. Papa amesema: “Siku mbili zilizopita tuliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake. Ningependa kuzungumzia mawazo na kueleza ukaribu wangu kwa wanawake wote, hasa wale ambao hadi yao haiheshimiwi. Bado kuna kazi nyingi ambayo kila mmoja wetu lazima afanye ili hadhi sawa ya wanawake itambulike kikamilifu.” Kwa kuongezea amesema “Ni taasisi za kijamii na kisiasa ambazo zina jukumu la msingi la kulinda na kukuza Hadhi na utu wa kila binadamu, kuwapa wanawake, wabebaji wa maisha, hali muhimu ili kuweza kukaribisha zawadi ya maisha na kuhakikisha watoto wao wanakuwa na hadhi ya kuwepo kwao.”
Kama kawaida yake, Papa Francisko amegeukia mtazamo wa migogoro na vurugu duniani ambapo amesema: “Ninafuatilia kwa wasiwasi na uchungu mgogoro mkubwa unaoathiri Haiti na matukio ya vurugu ambayo yametokea katika siku za hivi karibuni. Niko karibu na Kanisa na watu wapendwa wa Haiti, ambao wamekuwa wakipitia mateso mengi kwa miaka mingi.”
Kwa njia hiyo ameongeza kuwa: “Ninawaalika kusali, kwa maombezi ya Mama Yetu wa Msaada wa Daima, ili kila aina ya vurugu zikome na kila mtu atoe mchango wake katika kuongeza amani na upatanisho nchini, kwa kuungwa mkono upya na Jumuiya ya Kimataifa.”
Baba Mtakatifu kwa kuwa ni Baba wa wote pia amekuwa na mtazamo kwa Ndugu zetu Waislamu ambapo amesema: “Usiku wa leo ndugu Waislamu wataanza mwezi wa Ramadhani: Naeleza ukaribu wangu kwa wote.”
Papa Francisko aidha ametoa salamu kwa mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia ambapo amesema “ Ninawasalimu ninyi nyote mliotoka Roma, Italia na sehemu nyingi za dunia. Hasa, ninawasalimu wanafunzi wa chuo cha Irabia-Izaga huko Pamplona, mahujaji kutoka Madrid, Murcia, Malaga na wale kutoka Mtakatifu Maria - Plainfield - New Jersey. Nawasalimu watoto wa Komunyo ya Kwanza na Kipaimara wa Parokia ya Mama Yetu wa Guadalupe na Mtakatifu Filippo Shahidi huko Roma; waamini wa Reggio Calabria, Quartu Mtakatifu Elena na Castellamonte.
Papa aidha amesema: “Ninakaribisha kwa uchangamfu jumuiya ya Kikatoliki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mjini Roma. Tunaomba kwa ajili ya amani katika nchi hii, pamoja na katika Ukraine inayoteswa na katika Nchi Takatifu. Acha uhasama unaosababisha mateso makubwa miongoni mwa raia ukome haraka iwezekanavyo.” Hatimaye amewatakia Dominika nje, na tafadhali wamwombee na kwaheri ya kuonana.