Papa Francisko ametuma Rambirambi kufuatia na kifo Neofit wa Bulgaria
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ametuma Ujumbe na salamu za rambi rambi aliomwelekea Yoan, Mkuu wa Kanisa la Varna na Veliki Preslav na Sinodi Takatifu ya Upatriaki wa Kanisa la Kiorthodox la Bulgaria, kuafuatia na kifo cha Neofit. Katika ujumbe huo anabainisha kuwa amesikitika sana kwa kifo cha Patriaki wao mpendwa, Neofit, ambaye alikuwa shuhuda mkuu wa imani ya Kanisa la Kiorthodox la Bulgaria, na anatuma salamu za rambirambi kwake, kwa Sinodi Takatifu anayoiongoza, na kwa Kanisa zima la Kiorthodox la Bulgaria. Patriaki Neofit alitoa huduma yenye thamani kwa Injili na mazungumzo, na licha ya mateso yake mengi alibaki kuwa mtu wa unyenyekevu na furaha, kielelezo cha maisha yaliyowekwa wakfu kwa Bwana na Kanisa lake.
Kwa kuwa Mwili wa Kristo duniani, Kanisa ni lango la kuingia katika uzima wa Bwana Mfufuka, hivyo kwa waamini wa Kikristo, kifo ni alama ya kifungu kutoka kwa ulimwengu huu hadi Uzima wa Milele. Kwa hivyo, ni tumaini letu la maombi kwamba mkuu huyo Neofit sasa anaishi “ambapo hakuna huzuni wala maumivu wala kuugua” . Baba Mtakatifu katika salamu hizo za rambi rambi anamhakikishia Yeye, Sinodi Takatifu na washiriki wote wa Kanisa Kiorthodoksi la Bulgaria kwa ukumbusho wa pekee katika sala zake , kwamba Yesu Kristo, ambaye “alifufuka kutoka katika wafu, alishinda kifo kwa kifo chake na kutupa uzima” awajaze mioyo yao faraja na amani.