Katekesi ya Papa Kuhusu Fadhila Na Mizizi ya Dhambi:Fadhila ni tabia ya uhuru!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 13 Machi 2024 ameendeleza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi ambapo katika katekesi zake tumekisha uona wivu, utepetevu, uchoyo, majivuno na kiburi Ni katika muktadha huo ambao kwa waamini na mahujaji waliofika katika katekesi yake, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican iliyosomwa kwa niaba yake na Monsinyo Pierluigi Giroli, kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican amesema baada ya kuhitimisha muhtasari wa mizizi, wakati umefika wa kugeuza mitazamo yetu kwenye picha ya ulinganifu, ambayo inapingana na uzoefu wa uovu. Moyo wa mwanadamu unaweza kuingiza tamaa mbaya, unaweza kusikiliza majaribu yenye madhara yaliyojificha kwa nguo za kushawishi, lakini pia unaweza kupinga yote haya. Ingawa hii inaweza kuwa ya kuchosha, mwanadamu ameumbwa kwa ajili ya wema, ambao kiukweli huufanikisha, na pia anaweza kufanya sanaa hii, kuhakikisha kwamba tabia fulani inakuwa ya kudumu ndani yake. Tafakari juu ya uwezekano huu wa ajabu wetu huunda sura ya kawaida ya falsafa ya maadili: sura ya fadhila.
Wanafalsafa Waroma waliiita virtus, na wanafalsafa Wagiriki waliiita aretè. Neno la Kilatini linaakisi zaidi ya yote kwamba mtu mwema ni mwenye nguvu, jasiri, mwenye uwezo wa nidhamu na kujinyima moyoni; kwa hiyo zoezi la fadhila ni tunda la kuota kwa muda mrefu, ambalo linahitaji juhudi na hata mateso. Neno la Kigiriki, aretè, linaonesha kitu ambacho ni bora zaidi, kitu kinachotokea, ambacho huamsha sifa ya kupendeza. Kwa hiyo mtu mwema ni yule ambaye hajipotoshi bali ni mwaminifu kwa wito wake na anajitambua kikamilifu. Tutakuwa tumekosea ikiwa tungefikiri kwamba watakatifu ni tofauti na ubinadamu: aina ya mzunguko finyu ya mabingwa wanaoishi nje ya mipaka ya mitindo zetu. Watakatifu, katika mtazamo huo ambao tumetoka kuutambulisha hivi punde kuhusiana na fadhila, badala yake ni wale ambao wanakuwa wenyewe kikamilifu, wanaotambua wito wa kila mtu.
Katika katekesi hiyo Baba Mtakatifu anaendelea kukazia kuwa “Ungekuwa ulimwengu wenye furaha kama nini ambamo haki, heshima, ufadhili wa pande zote, mawazo mapana, na tumaini vingekuwa hali ya kawaida ya pamoja, na badala yake sio kuwa na hitilafu! Hii ndiyo sababu sura ya matendo ya fadhila, katika nyakati hizi za kutisha ambapo mara nyingi tunashughulika na watu wabaya zaidi, inapaswa kugunduliwa upya na kutekelezwa na kila mtu. Katika ulimwengu wenye ulemavu lazima tukumbuke umbo ambalo tuliumbwa nalo, sura ya Mungu ambayo imetiwa chapa ndani yetu milele.
Lakini tunawezaje kufafanua dhana ya fadhila? Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatupatia ufafanuzi sahihi na kwa ufupi: “Fadhila ni tabia ya mazoea na thabiti ya kutenda mema” (N. 1803). Kwa hivyo si jambo jema lililoboreshwa na kwa kiasi fulani, ambalo hunyesha kutoka angani kwa njia ya matukio. Historia inatuambia kwamba hata wahalifu, katika wakati wa uwazi, wamefanya matendo mema; hakika matendo haya yameandikwa katika “kitabu cha Mungu”, lakini fadhila ni kitu kingine. Ni nzuri inayotokana na kukomaa polepole kwa mtu, mpaka inakuwa tabia ya ndani. Fadhila ni Habitus -tabia ya uhuru.
Ikiwa tuko huru katika kila tendo, na kila wakati tunapoitwa kuchagua kati ya mema na mabaya, wema ndio unaoturuhusu kuwa na tabia kuelekea uchaguzi sahihi. Ikiwa wema ni zawadi nzuri sana, swali linatokea mara moja: inawezaje kupatikana? Jibu la swali hili si rahisi, ni ngumu. Kwa Mkristo, msaada wa kwanza ni neema ya Mungu. Kwa hakika, Roho Mtakatifu hutenda kazi ndani yetu sisi tuliobatizwa, akifanya kazi katika nafsi zetu ili kuiongoza kwenye maisha ya fadhila. Ni Wakristo wangapi wamefikia utakatifu kwa machozi, wakitambua kwamba hawakuweza kushinda baadhi ya udhaifu wao! Lakini walipata uzoefu kwamba Mungu alikamilisha kazi hiyo njema ambayo kwao ilikuwa ni mchoro tu. Neema daima hutangulia kujitolea kwetu kimaadili.
Zaidi ya hayo, hatupaswi kamwe kusahau fundisho lenye thamani sana ambalo lilikuja kwetu kutokana na hekima ya watu wa kale, ambayo hutuambia kwamba fadhila hukua na unaweza kusitawisha. Na kwa hili kutokea, zawadi ya kwanza ya Roho kuomba ni hekima. Mwanadamu sio eneo la bure kwa ushindi wa raha, hisia, silika, tamaa, bila kuwa na uwezo wa kufanya chochote dhidi ya nguvu hizi, wakati mwingine za machafuko, zinazokaa ndani yake. Zawadi ya thamani sana tuliyo nayo ya kuwa na nia iliyo wazi, ni hekima inayojua jinsi ya kujifunza kutokana na makosa ili kuelekeza maisha vizuri. Kisha tunahitaji nia nzuri: uwezo wa kuchagua mema, kujitengeneza wenyewe na mazoezi ya kiriho, kuepuka kupita kiasi. Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu anabainisha kuwa hivi ndivyo tunavyoanza safari yetu kupitia fadhila, katika ulimwengu huu tulivu ambao unaonekana kuwa wenye changamoto, lakini wenye maamuzi ya furaha yetu.