Papa:Sayansi na hekima ya watu wa Asilia lazima ilinde sayari pamoja
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 14 Machi 2024 alikutana na Washiriki wa Mkutano unaoendelea kwenye ukumbi wa Casina Pio IV mjini Vatican, ambao unahusu suala la kutambua thamani kubwa ya hekima ya Watu wa Asilia na kukuza ubinadamu fungamani na maendeleo endelevu, uliohamasishwa na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi na Elimi ya Sayansi kijamii, ambapo kutokana na hali ya Papa utokuwa na sauti nzuri, amemuomba Padre Giroli asome kwa niaba yake. Katika hotuba hiyo, anawakaribisha washiriki wa mkutano huo wa maarifa ya watu wa kiasili na sayansi. Mkutano huo unakusudia kuleta pamoja aina hizi mbili za maarifa kwa mtazamo mpana zaidi, tajiri zaidi, wa kibinadamu zaidi kwa baadhi ya masuala muhimu ya dharura, kama vile mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa viumbe hai, vitisho kwa usalama wa chakula na afya, na mengine. Alimshukuru Kansela wa Taasisi hiyo, Kardinali Peter K. Turkson, na Marais wa Vyuo vya Kipapa vya Sayansi na Elimu ya Sayansi Jamii kwa kuendeleza mpango huo: ni mchango unaostahili kutambua thamani kubwa ya hekima ya Watu Asilia na kukuza maendeleo fungamani na endelevu ya binadamu.
Papa anakumbuka kwamba Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa - FAO - pia liliandaa siku za mafunzo kuhusu mifumo ya chakula asilia miaka mitatu iliyopita. Matokeo yake yalikuwa ni Jukwaa linalowaleta pamoja wanasayansi wa kiasili na wasio asilia, wasomi na wataalamu, ili kuanzisha mazungumzo yenye lengo la kuhakikisha ulinzi wa mifumo ya chakula ya watu asilia. Pia katika mwendelezo wa uzoefu huo, alikaribisha kwa shukrani mpango wao wa kuendeleza utafiti huo. Awali kabisa Papa angependa kusema kwamba hii ni fursa ya kukua katika kusikilizana: kusikiliza watu wa kiasili, kujifunza kutoka katika hekima yao na mtindo wao wa maisha, na wakati huo huo kusikiliza wanasayansi, kujifunza kutoka katika mafunzo yao. Zaidi ya hayo, semina hii ya utafiti inatuma ujumbe kwa serikali na mashirika ya kimataifa kutambua na kuheshimu utajiri wa utofauti ndani ya familia kubwa ya binadamu. Katika muundo wa ubinadamu kuna tamaduni tofauti, mila, kiroho, lugha ambazo zinahitaji kulindwa, kwa sababu upotezaji wao ungejumuisha umaskini wa maarifa, utambulisho na kumbukumbu kwa sisi sote.
Kwa sababu hiyo, ni lazima mipango ya utafiti wa kisayansi, na kwa hivyo uwekezaji, uelekezwe zaidi katika kukuza udugu wa binadamu, haki na amani, ili rasilimali zigawanywe kwa njia iliyoratibiwa ili kukabiliana na changamoto za dharura zinazoathiri nyumba ya wote na familia ya watu. Tunatambua kwamba, ili kufikia lengo hili, uongofu unahitajika, maono mbadala kwa yale ambayo leo hii yanasukuma ulimwengu kuelekea kwenye migogoro inayoongezeka. Mikutano kama yao inakwenda katika mwelekeo huo kwani kiukweli, mazungumzo ya wazi kati ya maarifa ya Watu Asilia na sayansi, kati ya jamii za hekima asilia na zile za kisayansi zinaweza kuchangia kushughulikia maswala muhimu, kwa mfano, njia bora zaidi, zile za maji, mabadiliko ya tabianchi, njaa, viumbe hai(bayoanuai) na masuala ambayo, kama tunavyojua, yote yanaunganishwa.
Papa anamshukuru Mungu kuwa, hakuna upungufu wa dalili chanya katika maana hii, kama vile Umoja wa Mataifa ujumuishaji wa maarifa asilia kama sehemu kuu ya Muongo wa Kimataifa wa Sayansi kwa Maendeleo Endelevu. Ishara ya kukuzwa na kuungwa mkono, kuunganisha nguvu pamoja. Kwa sababu hii, katika mazungumzo kati ya maarifa asilia na sayansi, lazima tuwe wazi na kukumbuka kila wakati kwamba utajiri huu wote wa maarifa lazima utumike ili kujifunza kushinda migogoro kwa njia isiyo ya vurugu na kupambana na umaskini na aina mpya za maisha ya utumwa. Mungu, Muumba na Baba wa wanadamu wote na wa kila kitu kilichopo, anatuita leo kuishi na kushuhudia wito wetu wa udugu wa ulimwengu mzima, uhuru, haki, mazungumzo, kukutana baina yao, upendo na amani, kuepuka kuchochea, chuki, migawanyiko, vurugu na vita. Mungu ametufanya kuwa walinzi na sio wakuu wa sayari: sote tumeitwa kwenye uongofu wa ikolojia (taz. Laudato si', 216-221), tumejitolea kuokoa makao yetu ya pamoja na kuishi katika mshikamano wa vizazi ili kulinda maisha ya siku zijazo, vizazi, badala ya kufuja rasilimali na kuongeza ukosefu wa usawa, unyonyaji na uharibifu.
Papa Francsko akiwageukia wawakilishi wa jumuiya za kiasili na wanasayansi, amewashukuru kwa kujitolea kwao na kuwatia moyo wachote kutoka kwa urithi wa hekima wa mababu zao na kutokana na matunda ya utafiti wa maabara yao uhai wa kuendelea kufanya kazi pamoja kwa ajili ya ukweli, uhuru, mazungumzo. haki na amani. Kanisa liko nao washirika wa watu wa kiasili na maarifa yao, na washirika wa sayansi kusaidia udugu na urafiki wa kijamii kukua duniani. Anawasindikiza kwa maombi yake na, kwa kuheshimu imani ya kila mtu, ameomba baraka za Mungu juu yao, na wao pia, kwa njia yao wamwombee.