Sakramenti ya Upatanisho Ni Chemchemi ya Uponyaji na Furaha: Msamaha wa Dhambi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima na kwa mwaka huu ni tarehe 8-9 Machi 2024 na mkazo unawekwa katika maisha ya sala na msamaha wa dhambi. Kila Jimbo linapaswa kufanya maadhimisho haya ili kuwapatia waamini nafasi ya kuweza kuchunguza dhamiri zao, kujuta, kuungama na hatimaye, kutimiza malipizi, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huu ni muda pia wa kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa kuongozwa na Neno la Mungu kutoka katika Sura ya sita ya Waraka wa Mtakatifu Paulo kwa Warumi. Kufa na kuishi pamoja na Kristo ili “kuenenda katika upya wa uzima.” Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” Ijumaa tarehe 8 Machi 2024 ameongoza Ibada hii kwenye Parokia ya “San Pio V” iliyoko Jimbo kuu la Roma. Zaidi ya waamini 1, 500 wamehudhuria Ibada hii, hawa ni wale waliokuwa ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu amewaungamisha waamini tisa na wakati wote wa kipindi cha maungano, Ibada hii ilitawaliwa na: Sala, Zaburi, Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na nyimbo za toba. Hii ni Parokia inayoongozwa na Padre Donato la Pera anayekiri kwamba, kwa hakika hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko imeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za waamini ndani na nje ya Parokia.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amelitaka Kanisa katika maisha na utume wake, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa msamaha ili kuenenda katika upya wa uzima na kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote na kamwe hachoki kusamehe, ingawa binadamu anachoka kuomba msamaha. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayefahamu yale yaliyofichika katika sakafu ya moyo wa mwanadamu na yuko tayari kumponya na kumtaka mwamini anayekimbilia huruma na upendo wa Mungu; waamini wajifunze toba na unyenyekevu kutoka kwa yule mgonjwa mwenye ukoma aliye mwambia Kristo Yesu: “Ukitaka waweza kunitakasa.” Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti. Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya uponyaji na furaha. Baba Mtakatifu anasema, kuenenda katika upya wa uzima kunapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo inayomzamisha mwamini katika mateso, kifo na ufufuko kwa Kristo Yesu kwa wafu. Hii ni safari inayotekelezwa kila siku ya maisha na kwamba, shughuli nyingi katika ulimwengu mamboleo zisiwafanye waamini wakasahau safari hii katika upya wa uzima.
Mwenyezi Mungu katika upya wa maisha ni Baba anayepaswa kupendwa kwani watu wote wa Mungu wanaunganishwa na hivyo kuwa ndugu wa Baba mmoja, hivyo kuna haja ya kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana. Inasikitisha kuona kwamba, wandani wa safari katika upya wa maisha mara nyingi wanageuka na kuwa ni maadui na wapinzani wa maisha. Hii ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na wafuasi wa Kristo. Paulo Mtume anapoiandikia Jumuiya ya waamini wa Roma anasema “Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo.” Rum 7:19. Hii ni changamoto ya kupyaisha ule uzuri asilia aliojipatia mwamini kwa njia ya Ubatizo unayowasaidia kupiga moyo konde na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, bila kusimama na kujikatia tamaa. Maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima ni fursa makini ya kuanza kutembea katika upya wa uzima wa milele, kwa kuambana njia ya upatanisho, kwa kutambaua kwamba, Mwenyezi Mungu anasamehe daima na kwamba, binadamu wakati mwingine anashindwa kuomba msamaha. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Ubatizo anawatakasa na kuanza upya kutembea katika njia ya uzima wa milele inayowachangamotisha kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Itakumbukwa kwamba, Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. “Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu.” Mt 5:8. Hapa waamini wanakumbushwa kwamba, ni Mwenyezi Mungu ambaye anaweza kuona yale yaliyofichika katika sakafu ya moyo wa mwanadamu na kuyaponya na kuyatakasa na kwamba, ni Mwenyezi Mungu anayeweza kumwokoa mwanadamu kutoka katika mateso.
Jambo la msingi kwa waamini ni kujifunza toba na unyenyekevu kama alivyofanya yule Mkoma ili kumwomba Kristo Yesu: “Ukitaka waweza kunitakasa.” Mk 1: 40. Mwenyezi Mungu daima anapenda kupyaisha maisha ya watoto wake, ili waweze kutembea katika upya wa uzima. Kristo Yesu yuko tayari kuinama ili kumwinua yule aliyeteleza na kuanguka dhambini. Hii ni kwa sababu Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti. Waamini wanamjifunza Mungu kwa kusoma Maandiko Matakatifu na Katekesi, lakini, kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, waamini wanamtambua Mungu anayependa na kusamehe: “Nenda na amani, dhambi zako zimeondolewa.” Kuenenda katika upya wa uzima kunapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo na Msamaha wa dhambi. mSakramenti ya wongofu, Kitubio, Ungamo, Msamaha na Upatanisho inayomwonjesha mdhambi huruma, upendo na msamaha wa Mungu, kiini cha maisha ya Kikristo na ufufuko wa moyo kwa kupata msamaha wa dhambi unaomrejeshea mwamini ile furaha ya mwanzo. Madonda Matakatifu ya kristo Yesu yanakuwa ni vyanzo vya huruma, upendo na amani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambaye, kamwe hachoki kusamahe, ingawa mwanadamu anachoka kuomba msamaha. Msamaha wa dhambi unapaswa kuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba, Mapadri waungamishaji ni vyombo vya huruma, upendo na msamaha. Kumbe, wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu. Kwa njia ya toba na maungamo ya dhambi, mwamini anapyaisha maisha yake na hivyo kuwa huru na kumwezesha kukutana na watu wa Mungu, kukuza na kudumisha ukweli na uaminifu katika maisha; na pia katika huduma kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake, tayari kuenenda katika upya wa uzima.