Sifa Kuu za Mtakatifu Yosefu Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mama Kanisa tarehe 19 Machi 2024 ameadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki, Mume wake Bikira Maria na Baba Mlishi wa Mtoto Yesu, aliyezaliwa kwa kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Mtakatifu Yosefu akamwita jina lake Yesu, maana Yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao na kutambuliwa kisheria kuwa ni Mwana wa Ukoo wa Daudi, Mwana wa Ibrahimu, Baba wa imani. Mtakatifu Yosefu aliteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi mwaminifu wa Nyumba ya Mungu, kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu sanjari na kukubali kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake, kama alivyoambiwa na Malaika wakati akiwa usingizini. Akamchukua Bikira Maria kama mchumba wake. Katika hali ya hatari, alimchukua Mtoto na Mama yake Bikira Maria, wakakimbilia Misri na kukaa huko hata alipofariki Herode, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii akisema, “Kutoka Misri nalimwita mwanangu.” Rej. Mt 1: 1-25; 2: 1-23. Mtakatifu Yosefu ndiye wakili mwaminifu na mwenye busara ambaye Bwana alimweka juu ya watumishi wake. Rej. Lk 12:42. Ni mfano bora katika maisha ya waamini aliyetoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu akailinda na kuitunza Familia Takatifu ya Nazareti kwa kazi ya mikono yake. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 20 Machi 2024 alipenda kuliweka tena Kanisa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Yosefu Mlinzi na Msimamizi wa Kanisa zima. Awe ni mfano bora wa kuigwa kwa wazazi. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Ukraine na Nchi Takatifu wanaoendelea kuteseka kutokana na madhara ya vita sanjari na mipasuko ya kijamii. Waamini na watu wenye mapenzi mema wajifunze kutoka kwa Mtakatifu Yosefu fadhila ya ujasiri na busara, ili waweze kutekeleza kikamilifu dhamana na wajibu wao kama Wabatizwa katika ulimwengu mamboleo.
Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu Yosefu yalizinduliwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 8 Desemba 2020 na kufungwa kwa kishindo hapo tarehe 8 Desemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu” anataja sifa kuu za Mtakatifu Yosefu akisema kwamba ni: “Baba mpendevu, mwenye huruma na mapendo; mtiifu na mwepesi kukubali. Ni Baba aliyebahatika kuwa na kipaji cha ugunduzi na ujasiri, lakini alibaki akiwa amefichwa kwenye vivuli, akawajibika na kuwa ni chanzo cha furaha na sadaka binafsi. Katika moyo wa unyenyekevu, Mtakatifu Yosefu aliyahifadhi mafumbo yote ya maisha yaliyomzunguka Mtoto Yesu na Mama yake Bikira Maria. Yosefu mtu wa busara na haki, alijiaminisha mbele ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu na kuyatekeleza yale yote aliyoambiwa na Bwana. Papa anasema, huyu ni Baba ambaye alibahatika kuwa na karama ya kupokea, ni Baba Mlinzi na hatimaye, Ni Baba mwenye ndoto! Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema kwamba, Mtakatifu Yosefu alishinda vishawishi na uasi wote hata kama vilikuwa ni halali katika maisha yake, akapiga moyo konde, akampenda na kumpokea Bikira Maria na Mtoto Yesu na hatimaye, akawalinda na wakawa salama salimini. Mtakatifu Yosefu hakutafuta sababu yoyote, bali aliyakubali mapenzi ya Mungu katika maisha yake kama kielelezo cha imani. Ni katika mazingira kama haya, Mtakatifu Yosefu anaheshimiwa na Kanisa kama Baba wa mang’amuzi na maisha ya kiroho.
Waamini wanahamasishwa kumkimbilia, pale wanapokumbana na mishale ya mashambulizi, ili kuweza kupokea mapenzi ya Mungu jinsi yalivyo katika maisha. Huu ni mfano bora wa kuigwa kwa Padre anapohamishiwa kwenye Parokia mpya. Jambo la kwanza kwa Padre kama huyu, ni kuhakikisha kwamba, anaipenda Jumuiya yake kama ilivyo kwa sababu ameitwa na kutumwa kuihudumia. Kwa kupenda kwa moyo, ataweza kujifunza undani wa maisha ya watu anaowahudumia na hivyo kuweza kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Parokia. Mtakatifu Yosefu ni Baba mlinzi, hali inayoonesha kiini cha wito na utume wake. Dhamana na wajibu huu ulitekelezwa na Mtakatifu Yosefu katika: kimya kikuu, kwa moyo wa unyenyekevu na uaminifu wote hata pale ambapo kwa akili ya binadamu alishindwa kuufahamu mpango wa Mungu. Alijitahidi kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kutekeleza mpango wake katika maisha, na hivyo kuwa na uhuru wa ndani kama mtumishi mwema na mwaminifu anayetamani ustawi na maendeleo ya wale watu ambao Mwenyezi Mungu amemkabidhi! Dhamana ya kulinda, kama ilivyo kwa kila Padre maana yake ni kuwapenda kwa dhati, watu ambao wamekabidhiwa kwao, kwa kuwatakia mema na furaha, huku wakiwahudumia kwa ukarimu mkuu. Kulinda ni maelekeo ya ndani yanayomwezesha mwamini kuwa na dira, mang’amuzi pamoja na kupima hatua ya kuchukua. Lakini daima anapaswa kuwa makini, huku akikesha na kusali. Huu ni mwelekeo wa kichungaji ambapo, kimsingi mchungaji hapaswi hata kidogo kuwatelekeza Kondoo wake! Daima yuko mbele yao kama kiongozi, ili kuwaonesha njia; yuko kati yao ili kuwafariji na anakwenda nyuma yao, ili kuwapokea na kuwasaidia wale wa mwisho.
Huu ndio mwelekeo wa maisha na utume wa Kipadre kwa ajili ya Jumuiya aliyokabidhiwa na Mama Kanisa. Anapaswa kuwa ni Mlinzi ambaye yuko tayari kufanya marekebisho kwa kusoma alama za nyakati, bila ya kuwa na shingo ngumu. Mapadre wawe wepesi kukubali mabadiliko katika maisha na utume wao, kwa kuzingatia mahitaji msingi ya jumuiya wanayoiongoza na kamwe wasitumbukie katika kishawishi cha kutaka kutawala na hivyo kushindwa kutoa huduma makini! Mtakatifu Yosefu alikuwa ni Baba mwenye ndoto, akabahatika kuwa na upeo mpana kwa kuona mbele zaidi ya kile kilichokuwa kinaonekana machoni! Huu ni mtazamo wa kinabii wenye uwezo wa kuona na kung’amua mpango wa Mungu na lengo linalomsubiri hapo mbeleni. Mtakatifu Yosefu alimwona Bikira Maria kuwa mchumba wake akiwa na Mtoto Yesu. Zaidi sana, aliiona kazi na uwepo wa Mungu katika maisha yake. Akatekeleza dhamana na wajibu wake kama Baba mlishi wa Mtoto Yesu. Kwa kuamini kwake, akashinda hofu na mashaka, akawa ni chombo na shuhuda wa huduma iliyotolewa kwa ukarimu bila kuchoka na zaidi katika hali ya kimya kikuu! Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuwa na ndoto ya upendo kwa jumuiya, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili kuilinda na kuiendeleza, ili kuleta toba na wongofu wa ndani; kwa kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, ili kusaidia jumuiya kukua katika safari ya wafuasi wanaosukumwa na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kugundua ndani mwao, moyo wa sala, utume na unyenyekevu katika kutekeleza mapenzi ya Mungu, huku wakionesha utii na ubunifu. Mapadre wajifunze sanaa ya Ubaba inayotekelezwa katika jumuiya sanjari na huduma za kichungaji wanazokabidhiwa na Mama Kanisa.