Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Ulinzi wa Watoto Wadogo: Usalama Na Utakatifu wa Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia “Pontificia Commissione per la Protezione dei Minori (PCPM)”, iliundwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 22 Machi 2014 ili kutoa ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kushirikiana na Makanisa mahalia kwa ajili ya kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia, vitendo ambavyo vimelichafua Kanisa katika miaka ya hivi karibuni. Pamoja na mambo mengine, Tume hii inatoa mwongozo wa kuwalinda watoto wadogo; mchakato wa uponyaji kwa watu walioathirika na nyanyaso za kijinsia; malezi na majiundo makini kwa Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu ya Upadre, Watawa pamoja na viongozi wa Kanisa katika masuala ya elimu. Tume hii ina dhamana ya kutoa elimu kwa familia na jumuiya za Kikristo, kwa kujikita katika taalimungu na tasaufi; sheria za Kanisa pamoja na sheria za kiraia. Tume imekuwa na mchango mkubwa kutokana na shuhuda mbalimbali katika ngazi ya mtu binafsi na Tume katika ujumla wake. Huu ni wito unaosimikwa katika ujasiri na unapata chimbuko lake katika kiini cha Kanisa ili kujitakasa na hivyo kuendelea kukua, ili kuliwezesha Kanisa kuwa ni mahali pa salama kwa watoto wadogo na watu ambao ni dhaifu. Hii ni huduma inayopaswa kutolewa kama timu kwa kujenga madaraja ya ushirikiano ili kuweza kuhudumiana. Kwa mwaka 2024 Tume imejikita katika kuandaa taarifa yake ya Mwaka mintarafu sera na mbinu za kufuata ili kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Hii ni kazi kubwa lakini italisaidia Kanisa kujiandaa vyema ili kukabiliana na changamoto za mbeleni. Kamwe wajumbe wasikate wala kujikatia tamaa, ili hatimaye, kuliwezesha Kanisa kuwa ni mahali ambapo watu wote wanajisikia kuwa wako nyumbani na kwamba, utakatifu wa maisha ya kila mwamini unalindwa na kuthaminiwa.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 7 Machi 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi wa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kama sehemu ya kuhitimisha mkutano mkuu wa mwaka. Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Monsinyo Pierluigi Giroli, kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, Baba Mtakatifu amewataka wajumbe kutekeleza dhamana na utume wao kwa kuwa na hisia kama zile za Kristo Yesu, Viongozi wa Kanisa wanapaswa kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto, Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Memorare: Kumbuka; Itifaki ya fedha kwa ajili ya kuhifadhi, kutoa na kuripoti matumizi ya fedha kwa ajili ya mpango wa kujenga uwezo wa kuwalinda watoto wadogo. Baba Mtakatifu amewataka wajumbe kutekeleza dhamana na utume wao kwa kuwa na hisia kama zile za Kristo Yesu, yaani kwa kuwa na huruma, kiasi cha kugusa madonda ya binadamu, Moyo wake Mtakatifu ulitobolewa kwa mkuki, chemchemi ya huruma na upendo usiokuwa na kifani na kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, akaonesha ukaribu wa Mungu katika mahangaiko ya binadamu na kwa Fumbo la Pasaka amebeba madonda ya binadamu, ameyachukua masikitiko yake na amejitwika huzuni zao. Rej. Isa 53:4. Utume wa Kanisa ni kuwalinda watoto, kuonesha ukarimu kwa waathirika na kwamba, viongozi wa Kanisa wanapaswa kutambua athari za nyanyaso za kijinsia kwa watu wao; kwa kuwasikiliza pamoja na kuwasaidia kujiandalia kesho yenye matumaini. Waathirika lazima wasikilizwe kwa makini na kuhudumiwa, huku wakisaidiana na watu makini.
Baba Mtakatifu amechukua fursa hii, kuwashukuru wajumbe wa Tume kwa huduma yao kwa watu wa Mungu na kwamba, sasa matunda ya kazi yao yanapaswa kuanza kuonekana kwenye Makanisa mahalia. Waendelee kuyashirikisha Makanisa mahalia mbinu zilizokwisha kutambuliwa. Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia ni sehemu ya mbinu mkakati ya kuwahudumia waathirika wa nyanyaso za kijinsia, kwa kuendelea kujikita katika ulinzi na udhibiti wa nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Baba Mtakatifu Francisko amegusia pia kuhusu: Memorare: Kumbuka; Itifaki ya fedha kwa ajili ya kuhifadhi, kutoa na kuripoti matumizi ya fedha kwa ajili ya mpango wa kujenga uwezo wa kuwalinda watoto wadogo. Mfuko huu ambao ulianzishwa tarehe 25 Machi 2023 umeanza kufanya kazi kielelezo cha ukaribu wa Kanisa kwa waathirika na huduma zinazotolewa kwao. Huu ni mwanzo wa ujenzi wa mtandao wa mshikamano na waathirika, ili kuendelea kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, hususan katika maeneo ambayo rasilimali watu na fedha vinapwelea. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe kwa huduma makini wanayoitoa katika kukuza na kudumisha msingi wa haki na kwamba, Kanisa linapaswa kushiriki kikamilifu katika kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni mahali pa ukarimu na usalama.