Umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho Katika Maisha ya Mwamini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 8 Machi 2024 Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume linaendesha majiundo endelevu kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, ili wahudumu wa huruma ya Mungu waweze kuwazamisha waamini katika bahari ya huruma ya Mungu. Kati ya mada zilizotolewa ni pamoja na: Udhibiti, makosa na vikwazo kwa usikivu wa muungamishaji na mwenye kutubu: Haki na wajibu katika Sakramenti ya Kitubio, Uzoefu wa mwenye kukiri dhambi zake: Makundi ya wale wanaotubu: Kesi za kupagawa na pepo wachafu na jinsi ya kuwasaidia waamini; Utambuzi na usindikizaji wa maisha ya kiroho; Akili mnemba ni ushindi au hatari? Mawazo ya kiutendaji juu ya utekelezaji wa huduma ya Maungamo; Kuungama na mwelekeo wa kiroho, “The Ordo Paenitentiae”: tafakari na amana; pamoja na rasilimali kwa ajili ya huduma ya kichungaji ya toba na maungamano ya dhambi: Rehema kamili juu ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa 2025. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024. Huu ni mwaliko kwa waamini katika kipindi hiki cha Kwaresima anasema Baba Mtakatifu Francisko kujikita zaidi katika maisha ya sala, ili kuweza kutambua uwepo endelevu na angavu wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao.
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 8 Machi 2024 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume pamoja na washiriki wa majiundo endelevu. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amejikita katika Sala ya Kutubu amana na utajiri wa watu wa Mungu, Sala inayobeba uzito wa hali ya juu kichungaji na kitaalimungu iliyotungwa na Mtakatifu Alfonsi Maria de’ Liguori, Mwalimu wa Kanisa mintarafu taalimungu maadili, mchungaji aliyekuwa karibu sana na watu wake na kiongozi aliyekuwa na msimamo mzuri wa maisha. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia: Toba na wongofu wa ndani; imani kwa Mwenyezi Mungu na Majuto yasiyo kamili kwa yenyewe hayapati msamaha wa dhambi kubwa, bali huwezesha kuupata katika Sakramenti ya Upatanisho. Mwaka wa Sala kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yawawezeshe waamini kupata huruma ya Mungu katika maisha yao, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kupendwa, kufahamika na hivyo kutukuzwa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, toba na wongofu wa ndani ni matokeo ya utambuzi wa dhambi na mapungufu ya kibinadamu mbele ya upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani, ndiyo chachu inayowasukuma waamini kwenda kutubu dhambi zao kwa kusali ile Sala ya Kutubu: “Mungu wangu, nimetubu sana dhambi zangu, kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza, wachukizwa na dhambi. Basi sitaki kukosa tena, nitafanya kitubio, naomba neema yakon ipate kurudi. Amina. Hapa Muungamaji anatambua huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani na hivyo anatamani kujenga tena ushirika na Mungu na kwamba, hiki ni kielelezo cha toba, wongofu wa ndani na uchungu wa dhambi unaopelekea wongofu na kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu hachoki kusamehe, pengine ni waamini kwa upande wao wanaochoka na kukata tamaa ya kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Katika toba, Mwenyezi Mungu anatajwa kuwa ni mwingi wa huruma na mapendo na anapaswa kupendwa na kupewa kipaumbele cha kwanza kama mwanga wa maisha ya waamini. Huu ni mwaliko wa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani; huku mwamini akiendelea kutafuta ustawi, maendeleo yake katika haki na amani.
Toba ni uchungu wa roho na chuki ya dhambi iliyotendwa pamoja na kusudi la kutotenda dhambi tena baadaye. Toba inapotokana na upendo wa Mungu, anayependwa kuliko vitu vyote, huitwa toba kamili, yaani toba ya mapendo. Toba ya aina hii huondoa makosa madogo; pia hupata msamaha wa dhambi za mauti endapo inakwenda pamoja na kusudi thabiti la kukimbilia maungamano ya Sakramenti mapema iwezekanavyo. Toba isiyo kamili nayo pia ni karama ya Mungu na msukumo wa Roho Mtakatifu na hii ni chimbuko la fikra za ubaya wa dhambi na vitisho vyake ndiyo maana inaitwa toba ya hofu. Majuto yasiyo kamili kwa yenyewe hayapati msamaha wa dhambi kubwa, bali huwezesha kuupata katika Sakramenti ya Upatanisho. Kwa hakika Mungu anasamehe daima, jambo la msingi ni mwamini kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa sababu Mwenyezi Mungu ni huruma yenyewe na hili ndilo jina lake. Huu ni mwaliko kwa Mapadre waungamishaji kuwasaidia waamini kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 iwe ni fursa kwa waamini kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Na kwa njia hii Mwenyezi Mungu ataendelea kupendwa, kufahamika na kutukuzwa.