Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Martín Uriarte Zugazabeitia, Rais wa Jukwaa la Kilimo cha Familia Ulimwenguni, amekazia umuhimu wa wakulima wadogo wadogo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Martín Uriarte Zugazabeitia, Rais wa Jukwaa la Kilimo cha Familia Ulimwenguni, amekazia umuhimu wa wakulima wadogo wadogo.  (AFP or licensors)

Wakulima Wadogo Wadogo ni Nguzo ya Uchumi Na Usalama wa Chakula

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Martín Uriarte Zugazabeitia, Rais wa Jukwaa la Kilimo cha Familia Ulimwenguni, amekazia umuhimu wa wakulima wadogo wadogo, wanaounda mtandao wa mshikamano kwa kazi ya kilimo, huku wakiendelea kuheshimiana na kuthaminiana. Kwa mantiki hii, ni msingi wa kuhakikisha kuwa mifumo ya chakula cha kilimo inakuwa jumuishi zaidi, imara na yenye ufanisi. Wakulima wanaendelea kuathirika na umaskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mkutano wa Nane Kimataifa Kuhusu Kilimo cha Familia kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 21 Machi 2024 huko Vitoria-Gasteiz nchini Hispania, unanogeshwa na kauli mbiu: “Kilimo cha Familia Uendelevu wa Sayari Yetu." Mkutano huu umeandaliwa na Jukwaa la Dunia la Vijijini, na umewakusanya viongozi wa kilimo cha familia kutoka katika mabara matano, wawakilishi wa Serikali, Mashirika na Taasisi za Kimataifa, Vituo vya Utafiti, walaji, vijana pamoja na Mashirika ya Wakulima Wanawake. Mkutano huu, pamoja na mambo mengine unafafanua na kuendelea kuimarisha ahadi zinazohitajika ili kuhakikisha kwamba, kilimo cha familia kinachukua nafasi kubwa katika kukabiliana na changamoto kubwa za Kimataifa kama vile: Athari za mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa viumbe hai sanjari na mchakato wa uendelezaji wa mifumo bora ya chakula ulimwenguni. Miaka mitano ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kilimo cha Familia 2019-2028 (UNDFF), Mkutano wa 8 wa Kimataifa wa Kilimo cha Familia unatoa fursa ya kipekee ya kutafakari mafanikio muhimu, kuchambua changamoto zilizounganishwa, zinazokabili kilimo cha familia ambazo zimekuwa mbaya zaidi katika siku za hivi karibuni. Na hatimaye kubainisha hatua, vipaumbele na chachu ili kunogesha utekelezaji wa Miaka mitano ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kilimo cha Familia 2019-2028,  UNDFF, katika kukabiliana na changamoto hizi zinazokabili sio kilimo tu, bali ubinadamu katika ujumla wake.

Papa Francisko anapongeza mchango wa wanawake katika kilimo
Papa Francisko anapongeza mchango wa wanawake katika kilimo

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Martín Uriarte Zugazabeitia, Rais wa Jukwaa la Kilimo cha Familia Ulimwenguni, amekazia umuhimu wa wakulima wadogo wadogo, wanaounda mtandao wa mshikamano kwa kazi ya kilimo, huku wakiendelea kuheshimiana na kuthaminiana. Kwa mantiki hii, ni msingi wa kuhakikisha kuwa mifumo ya chakula cha kilimo inakuwa jumuishi zaidi, imara na yenye ufanisi. Kwa bahati mbaya, licha ya nafasi yao kubwa katika maendeleo ya watu wao na mchango wao mkubwa katika uzalishaji wa chakula duniani, wakulima wadogo wadogo wanaendelea kuathiriwa na umaskini na ukosefu wa fursa za masoko ya mazao yao ya chakula. Kwa kufahamu changamoto ngumu wanazokabiliana nazo kila siku, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutumia fursa hii kuwatia moyo na kuonesha ukaribu wa Mama Kanisa kwa wakulima wadogo wadogo, kwa kuzingatia: utu na heshima yao kama binadamu; mahitaji yao msingi kiroho, kijamii na kiteknolojia. Licha ya kilimo cha familia kuwa ni chombo mahususi chenye tija, lakini pia ni mahali ambapo panatoa utambulisho wao kwa utu, heshima na ubinadamu wao na wala si kwa sababu tu ya kile wanachozalisha au matokeo ya kazi zao. Hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha vifungo vinavyowaunganisha wanachama wao, mapokeo yao ya kidini, kitamaduni pamoja na shughuli zao za kilimo.

Kilimo cha kifamilia kina mchango mkubwa katika uchumi
Kilimo cha kifamilia kina mchango mkubwa katika uchumi

Baba Mtakatifu anakazia nafasi ya wanawake katika kilimo cha familia. Wanawake vijijini wanajitahidi kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo uhakika wa usalama wa chakula kwa familia zao, msingi madhubuti kwa ukuaji wa uchumi hususan katika nchi zinazoendelea ulimwenguni. Hawa ni wanufaika wakuu lakini pia ni watu wanaochokea na kukoleza maendeleo yanayohitajika. Baba Mtakatifu anakaza kusema, vijana wa kizazi kipya wanayo fursa ya pekee katika kilimo na kwamba, mapinduzi makubwa ya kilimo duniani yanaanza kwa kuwajengea vijana wa kizazi kipya uwezo. Zawadi inayotolewa na vijana inajumuisha kuleta suluhu ya kibunifu ya kushughulikia matatizo ya zamani na ujasiri wa kutozuiliwa na fikra fupi ambazo zinakataa kubadilika. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha ujumbe wake kwa Mkutano wa Nane Kimataifa Kuhusu Kilimo cha Familia, kwa kuwatakia heri na mafanikio mema katika mkutano huu, ili kutambua dhamana na fursa za familia katika kilimo cha familia vijijini, kama sehemu ya mchakato wa kung’oa baa la njaa, upunguzaji wa ukosefu wa usawa sanjari na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.

Wakulima Wadogo wadogo
21 March 2024, 15:30