Wanawake Katika Kanisa Waumbaji wa Ubinadamu: Mchango Maalum wa Wanawake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Baada ya maadhimisho ya Kongamano la Wanawake Kimataifa, mwezi Machi 2023, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wanawake Waalimu wa Kanisa na Walezi wa Bara la Ulaya, huo ukawa ni mwanzo wa maandalizi ya Kongamano la Wanawake Kimataifa kwa Mwaka 2024 linaloongozwa na kauli mbiu: “Wanawake Katika Kanisa: Waumbaji wa Ubinadamu.” Hili ni Kongamano ambalo limeadhimishwa mjini Roma kuanzia tarehe 7 Machi 2024 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko na linahitimishwa rasmi tarehe 8 Machi 2024. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amewarejesha wanawake hawa kwenye ushuhuda wa utakatifu wa maisha ya watakatifu kumi wanawake ndani ya Kanisa; wanawake wa waumbaji wa ubinadamu, washiriki katika kazi ya uumbaji, ustawi na maendeleo ya wengi pamoja na kudumisha amani. Amekazia kuhusu mtindo wa maisha, malezi na majiundo. Baba Mtakatifu amewataja watakatifu: Josefina Bakhita, Magdalena wa Yesu, Elizabeth Ann Seton, Maria MackKillop, Laura Mantoya, Kateri Tekakwitha, Mama Theresa wa Calcutta, Rafga Pietra Choboq Ar-Rayès, Maria Beltrame Quattrocchi pamoja na Daphrose Mukasanga. Hawa ni wanawake watakatifu kwa nyakati mbalimbali katika maisha na historia ya Kanisa walijizatiti katika huduma ya upendo, elimu, maisha ya sala, kielelezo makini cha utakatifu wa Mungu ulimwenguni. Itakumbukwa kwamba, hawa ni wale wanawake waliokuwa wametengwa katika maisha ya kijamii na utume wa Kanisa, lakini kwa nguvu ya Roho Mtakatifu akaamsha nguvu mpya na maisha ya kiroho, chachu katika mageuzi ndani ya Kanisa.
Kuna wanawake wengi wasiofahamika, lakini wamekuwa mstari wa mbele kuleta mageuzi katika familia na jamii zao kwa njia ya nguvu ya ushuhuda. Mama Kanisa anawahitaji wanawake kama hawa kwani Kanisa lenyewe kimsingi ni “Mama na Mwalimu, Ni Dada na Mchumba, mwaliko kwa Mama Kanisa kuendelea kufanya mang’amuzi, likiwa sikivu kwa Roho Mtakatifu, aminifu na lenye kudumisha ushirika, ili kutambua njia muafaka ili hatimaye kutambua na kuthamini nafasi ya wanawake miongoni mwa watu wa Mungu. Mintarafu utume wa wanawake katika Kanisa, Baba Mtakatifu amekazia zaidi mtindo wa maisha na majiundo. Katika ulimwengu huu ambao umesheheni vita, ghasia, chuki na hasira, kuna haja ya watu wa Mungu kujisikia kuwa wanapendwa na huu ndio mchango maalum kutoka kwa wanawake, wanaofahamu kuunganisha upendo unaosimikwa katika huruma. Kimsingi mwanamke kutokana na uwezo wake wa kipekee wa huruma, uangavu na tabia yake tangu asili ya kutunza anafahamu kwa njia kuu kuwa kwa jamii inayomzunguka: akili na moyo unaopenda na kuunganisha, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa upendo kwani mahali ambapo hakuna upendo, hapo mwanadamu anahangaika kujitafuta.
Kongamano hili ni matunda ya ushirikiano kati ya wanawake na taasisi mbalimbali zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki, kama sehemu ya mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji. Baada ya kusikiliza na kuzama zaidi katika majiundo ya Mafundisho tanzu ya Kanisa, Mafundisho Jamii ya Kanisa; Shuhuda za Utakatifu wa maisha na hasa miongoni mwa wanawake, hapa inaonesha kwamba, utakatifu wa maisha unaoweza kujikita katika medani mbalimbali za maisha na ufahamu, tayari wanawake kumfungulia akili na nyoyo zao Roho Mtakatifu. Hivyo ni vyema zaidi, wanawake kujibidiisha kuwafahamu watakatifu katika utu wao, ili hatimaye, kuweza kumgusa mwanadamu katika umoja wake. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, wanawake ni kati ya watu wanaoteseka sana katika ulimwengu mamboleo kutokana na vita, ukosefu wa haki na usawa pamoja na nyanyaso za kila aina. Hii mbaya zaidi kwa waamini wanaomkiri Kristo Yesu aliyezaliwa na “Mwanamke.” Rej. Gal 4:4. Kuna ubaguzi mkubwa unaotokana na majiundo ya mwanamke, lakini njia bora na makini inayoweza kuleta mabadiliko ni kupitia elimu kwa watoto wa kike. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga.