Dhamana na Wajibu wa Wanawake Katika Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake ili waweze kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Bila mchango wa wanawake, Kanisa litapoteza nguvu yake ya kujipyaisha tena. Dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa unajidhihirisha wazi kwa njia ya Bikira Maria, Nyota ya Uinjilishaji mpya. Kumbe, Kanisa linapaswa kushikamana pamoja na “wanawake wa shoka” ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanarithisha: imani, tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kitamaduni na kijamii kwa watoto wao. Itakumbukwa kwamba, wanaume na wanawake, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wapendane na kukamilishana; bila kuwadharau, kuwabeza na kuwanyanyasa wanawake. Wanawake washirikishwe pia katika malezi na majiundo ya Majandokasisi. Sauti ya wanawake, inapaswa kusikilizwa ndani ya Kanisa. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wanasema, wanawake ni rasilimali muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake washirikishwe katika mchakato wa kufanya maamuzi katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria awe ni mfano bora katika shule ya ufuasi wa Kristo Yesu. Vijana wawe ni nyota ya Msamaria mwema kwa njia ya huduma; nyota ya umisionari, matumaini na majadiliano ya: Kitamaduni, kidini na kiekumene. Kimsingi, Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, dhamana na utume wa wanawake katika Kanisa hauna budi kuimarishwa, kwa kukazia zaidi makuzi, malezi na majiundo ya awali, endelevu na fungamani, ili kuondokana na mfumo dume unaowanyima wanawake haki zao msingi. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni mambo muhimu katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna haja ya kutambua kwamba, kuna usawa na utofauti, kama kielelezo makini kinachotafuta uwiano mzuri unaojikita katika mahusiano dhidi ya utamaduni wa mfumo dume unaoendelea kumkandamiza mwanamke. Kuna haja ya kuvuka kishawishi cha kudhani kwamba, wote ni sawa sawa, kwa kushindwa kutambua tofauti, katika utambulisho wa mtu na asili yake, kwani mwanamke na mwanaume wanakamilishana. Pili, Baba Mtakatifu anasema, uwezo wa mwanamke kuzaa ni kanuni na utambulisho maalum kwa wanawake ambao wamejaliwa uwezo wa kuendeleza zawadi ya maisha, kwa kuilinda na kuidumisha. Kanisa linapenda kuwapongeza wanawake kwa mchango wao katika medani mbali mbali za maisha ya mwandamu; kwani wamekuwa mstari wa mbele katika masuala ya elimu na majiundo; shughuli na mikakati mbalimbali ya kichungaji na kwamba, wanawake wanaonesha sura ya huruma ya Mungu kwa binadamu. Ni watu wanaojisadaka kwa njia ya huduma, kwa kuonesha ukarimu, kimsingi, wanawake ni sawa na tumbo la Kanisa linalopokea na kuzaa maisha. Tatu, Baba Mtakatifu Francisko anajaribu kuangalia mwili wa mwanamke kati ya tamaduni na bayolojia, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanamke mwili unaopendeza, lakini pia umesheheni madonda ambayo wakati mwingine yamesababishwa na dhuluma pamoja na nyanyaso. Mwili wa mwanamke ni kielelezo cha maisha, lakini kwa bahati mbaya, unaharibiwa hata na wale ambao walipaswa kuwalinda na kuwasindikiza katika maisha! Kuna mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, biashara ya ngono na vitendo vya ukeketaji; mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuyavalia njuga, ili kusitisha vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya wanawake duniani, kiasi cha kuwageuza kuwa kama bidhaa inayouzwa sokoni, bila kusahau umaskini unaosababisha wanawake wengi kuishi katika mazingira magumu na hatarishi; kiasi hata cha kunyanyaswa, kielelezo cha utamaduni usiojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine.
Nne, Baba Mtakatifu anapopembua kuhusu wanawake na dini: mwelekeo wa kutafuta ushiriki katika maisha na utume wa Kanisa anakiri kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wanawake wanashiriki kwa ukamilifu zaidi katika utekelezaji wa dira na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani na nje ya Kanisa. Wanawake ni wadau wakuu katika kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ni watu wenye utajiri mkubwa, wanaoweza kusaidia upatikanaji wa amani na utulivu; wito na utume maalum kwa wanawake. Ziwepo juhudi za makusudi ili kuwahamasisha wanawake kushiriki katika maisha ya hadhara, katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa: mahali panapotolewa maamuzi na utekelezaji wa mikakati na sera mbali mbali; kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha ya kifamilia. Wanawake wasaidiwe kufanya maamuzi machungu katika maisha, kwa kuwajibika barabara katika jamii na katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 15-16 Aprili 2024 ameongoza mkutano wa Makardinali washauri tisa ili kuendelea na mjadala ulioanzishwa mwezi Desemba 2023 kuhusu dhamana na wajibu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Katika mkutano huu, Baraza la Makardinali Washauri limegusia kuhusu dhamana na mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Tafakari hii imechangiwa na Sr. Regina da Costa Pedro wa Shirika la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, aliyewashirikisha Makardinali uzoefu na mang’amuzi ya wanawake kutoka nchini Brazili. Professa Stella Mora, anayefundisha Kitivo cha Taalimungu, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian kilichoko mjini Roma amefanya upembuzi wa kina kuhusu tamaduni na utambuzi wa mchango wa wanawake, sehemu mbalimbali za dunia.
Kardinali Mario Grech pamoja na Monsinyo Piero Coda walijadili kuhusu maadhimisho ya awamu ya kwanza ya Sinodi yaliyohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican na jinsi ya kutekelez Katiba ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, akaridhia ichapishwe Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba ilianza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989.
Katiba ya Kitume “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” inapaswa kuanza kutekelezwa na majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki. Hii imekuwa pia ni fursa ya kupembua kwa umakini mkubwa hali hali ya maisha na utume wa Kanisa katika baadhi ya nchi, hali ya kisiasa, kiuchumi na Kikanisa. Umekuwa pia ni muda wa kusali na kuombea amani duniani. Baba Mtakatifu ameonesha wasiwasi mkubwa kwa kile kinachoendelea sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, kuna haja ya Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika kulinda na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, amendeleo na mafao ya wengi. Mkutano mwingine wa Makardinali Washauri utafanyika Mwezi Juni 2024.