Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Mjini Venezia: Yaliyojiri
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Venezia, Dominika tarehe 28 Aprili 2024 imenogeshwa na kauli mbiu “Kukaa kwa umoja katika upendo wa Kristo.” Baba Mtakatifu mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu na mara baada ya kusali Sala ya Malkia wa Mbingu, amewashukuru wale wote waliojisadaka usiku na mchana ili kufanikisha hija yake ya kichungaji mjini Venezia. Akamwomba Bikira Maria, awakumbuke na kuwaombea wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali duniani. Baba Mtakatifu ameyaelekeza mawazo yake nchini Haiti ambayo kwa sasa iko katika hali ya hatari na kwamba, watu wanateseka sana kutokana na kuharibika kwa miundombinu ya sekta ya afya, ukosefu wa chakula na maji safi na salama, vurugu, kinzani na mipasuko ya kijamii, mambo yanayopelekea watu wengi kuikimbia nchi ya Haiti. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Uongozi mpya wa kipindi cha mpito, uliosimikwa rasmi tarehe 25 Aprili 2024 huko Port-au-Prince, kwa msaada wa Jumuiya ya Kimataifa, wataisaidia Haiti kuwa na amani na utulivu; mambo msingi kwa wakati huu. Baba Mtakatifu aliyaelekeza mawazo yake nchini Ukraine, Palestina na Israel pamoja na Rohingya bila kuwasahau watu sehemu mbalimbali za dunia wanaoendelea kuteseka kutoka na athari za vita, vurugu na mipasuko ya kijamii. Mwenyezi Mungu, Baba wa amani, aiangazie nyoyo ili waweze kukuza ndani mwao utashi wa majadiliano na upatanisho. Hatimaye aliwashukuru watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Venezia kwa mapokezi na ukarimu waliomwonesha. Baba Mtakatifu amesema, anawabeba ndani ya moyo wake katika sala na hata wao wasisahau kumkumbuka na kumwombea, kwani utume wake si lele mama! Yataka moyo!
Baba Mtakatifu amepata fursa ya kutembelea Gereza na Wanawake la Giudecca lililoko mjini Venezia kama fursa ya kukutana pamoja, kusali, kuonesha ukaribu wa Mungu pamoja na kushirikisha hisia za ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kwamba, ametoka Gerezani humo akiwa amepyaishwa na kuwa ni mtu mwingine kabisa. Baba Mtakatifu anasema kuna watu wameingiza magerezani kwa mateso na machungu, lakini ikumbukwe kwamba kila mwanadamu anabeba ndani mwake: madonda na makovu; ni zawadi yenye thamani kubwa machoni mwa Mungu, tayari kujisadaka na kuwashirikisha wengine. Baba Mtakatifu anasema, gereza ni mahali pagumu sana pa kuishi, magereza mengi yamefurika, kuna uhaba wa miundo mbinu na rasilimali watu na fedha; ni mahali ambapo kumekuwepo na uvunjifu wa haki, amani na utulivu na hivyo kuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko makubwa kwa wafungwa na wale walioko magerezani na mahabusu. Lakini magereza panaweza kugeuka na kuwa ni mahali pa kupyaisha maisha kiutu na kimwili; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu; mahali pa kukuza karama na mapaji ambayo pengine kutokana na hali na mazingira ya wafungwa yalifichwa na sasa yanaweza kuibuliwa na kuanza kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na vijana mjini Venezia amewataka wawe ni mashuhuda wa tunu msingi na furaha ya Injili inayomwonesha Mungu akiwa kijana, na anayewapenda vijana, ili wagundue ndani mwao uzuri, tayari wote kufurahia maisha katika jina la Bwana, changamoto na mwaliko wa kusimama na kuondoka kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili sanjari na kumsaidia binamu yake Elizabeti aliyekuwa mhitaji kwa wakati ule. Rej. Lk 1:39. Vijana wanaalikwa kusimama kwani wameumbwa kwa ajili ya maisha ya mbinguni, wasimame kutoka katika uchungu, tayari kuyainua macho yao mbinguni, tayari kupambana na changamoto za maisha kwa kutambua kwamba, ujana ni zawadi adhimu isiyokuwa na mbadala, na kwamba wanayo dhamana na wajibu wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na kwamba, Sala ya Baba Yetu ni ufunguo wa furaha ya siku, kwani kijana ni Mwana wa Mungu aliye juu mbinguni hata katika vikwazo na changamoto za maisha, vijana wajitahidi kusimama! Vijana wanapoteleza na kuanguka, Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwashika mkono na kuwainua kama alivyofanya kwa Mtakatifu Petro Mtume, Maria Madgalena, Zakayo Mtoza ushuru pamoja na wengine wote, kwani Mwenyezi Mungu anatambua fika udhaifu na unyonge wa binadamu, tayari kuwashika mkono na kuwainua, jambo la msingi ni vijana kujitahidi kuwa waaminifu na wenye imani. Baba Mtakatifu anawahimiza vijana wa kizazi kipya kushirikishana mang’amuzi ya uwepo na upendo wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kamwe wasifanye mambo kipweke pweke wala kibinafsi.
Baba Mtakatifu ametembelea Banda la Maonesho kutoka Vatican yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Kwa macho Yangu.” Maonesho haya yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu pamoja na Idara ya Utawala wa Magereza sanjari na Wizara ya Sheria ya Italia. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa dhamana na mchango wao katika jamii na kwamba, ujumbe wake mahususi kwa wasanii wote popote pale walipo ni kwamba, Ulimwengu mambo leo una haja ya wasanii na kwamba, hapo alipo anajisikia kama yuko nyumbani ndani ya Kanisa la “Maddalena.” Sanaa mara nyingi inakita mizizi yake kama “mji wa kimbilio, hali inayokinzana na vurugu, mifumo mbalimbali ya ubaguzi, ili kutoa utambulisho wa binadamu; tayari kujitambua, kujumuisha, kulinda, kuwaambata na kuwakumbatia wote. Kristo Yesu wakati wa Karamu ya mwisho alikazia sana umuhimu wa wafuasi wake kubaki wakiwa wameungana naye, maneno yanayopata chimbuko lake katika Sala na Zaburi, kwa kutambua kwamba, shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe aliona dhuluma, alitamani kuona haki, na kumbe alisikia kilio. Is 5:7. Kristo Yesu katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 21: 33-44 anazungumzia kuhusu vibarua waovu, kwa kuonesha kazi na uvumilivu mkubwa ulioneshwa na Mwenyezi Mungu na jinsi ambavyo watu wake walivyomkataa. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa huduma ya upendo wa Mungu kwa binadamu, muungano wa dhati na waamini ili wapate kuzaa matunda, vinginevyo watanyauka na hatimaye kukatwa na kutupwa nje.
Mji wa Venezia anasema Baba Mtakatifu Francisko una historia ndefu ya kilimo cha mizabibu, uzalishaji wa divai, utunzaji bora wa mashamba ya mizabibu bila kusahau mchango wa Wamonaki katika mchakato wa uzalishaji wa divai kwa ajili ya jumuiya zao. Ujumbe muhimu katika simulizi hili ni imani kwa Kristo Yesu ni mwaliko kwa waamini kuupokea upendo wa Mungu unaozalisha furaha, kwani Mwenyezi Mungu anawahudumia waja wake na kuwawezesha kuzaa matunda hata kama udongo wa maisha ya waamini tayari ulikwisha choka na kwamba, Mungu anathamini sana uhuru wa watoto wake. Venezia ni mji uliojengwa juu ya bahari na hivyo unahitaji sana utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Na waamini, daima wakiwa wamezamishwa kwenye Maji ya Ubatizo, wanazaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu na hivyo kufanywa kuwa ni sehemu ya Kristo Yesu, Mzabibu wa kweli, ili kupata maisha na uzima wa milele. Kwa hakika, waamini wakibaki wameungana na Kristo Yesu watakuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wake na hivyo wataweza kuzaa zabibu bora inayozalisha divai ya upendo wa Mungu inayoujaza moyo wa mwanadamu furaha na matumaini. Matunda ya muungano huu na Kristo Yesu yanapaswa kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya waamini.